Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Serikali imeandaa mapendekezo ya kutungwa kwa sheria mpya ya usimamizi wa maafa ili kuweka mfumo wa udhibiti na uratibu wa maafa kwa ajili ya hatua za kuzuia na kupunguza madhara ya majanga, kujiandaa kukabili na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea.
Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria iliyokutana katika Ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma kujadili Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene amesema kutungwa kwa sheria hiyo ni kuifuta sheria iliyopo sasa ya mwaka mwaka 2015 sura ya 242.
Simbachawene alieleza kwamba awali masuala ya maafa hayakuwa na mfumo wa kisheria wa uratibu hali ambayo imekuwa ikisababisha mgongano wa majukumu hivyo kutungwa kwa sheria hiyo kutaainisha madaraka, wajibu, maamuzi, utunzaji wa rasilimali na muono unaozingatia taarifa za hali ya hewa.
“Awali masuala ya maafa yalikuwa na daraja fulani la watu, masuala ya kisheria yalikuwa kama yako juu hata ikitokea maafa ngazi ya Wilaya au Kijiji wanasema tumuone Mkuu wa Wilaya sasa tunataka sheria iseme yanapotokea maafa ijulikane kamati gani inahusika na kuweka mfumo wa ugatuaji kuanzia; madaraka, maamuzi na utunzaji wa rasilimali,” amesema Simbachawene.
Pia ameongeza kwamba sababu nyingine ya kutunga sheria mpya ya Usimamizi wa Maafa ni kuimarisha mfumo wa kiutendaji wakati wa maafa na upatikanaji wa taarifa na takwimu za matukio ya maafa na kuweka mfumo mpya wa kitaasisi unaozingatia mfumo wa kiutawala utakaowezesha ushiriki wa wadau wote muhimu kabla, wakati na baada ya maafa kutokea nchini.
“Eneo lingine ni kuhakikisha kamati hizi zinakuwa za kitendaji na siyo bodi ambapo itasaidia katika kutafuta ufumbuzi yanapotokea maafa pamoja na kuwezesha kurejesha hali ya awali baada ya madhara ya majanga kujitokeza,” amesema.
Aidha alieleza kwamba utungwaji wa sheria utasaidia kutumia taarifa za hali ya hewa na majanga ambapo kamati zitatakiwa kukutana pamoja na utunzaji wa rasilimali ambazo hutumika kukabili na kurejesha hali pamoja na kuzingatia usalama wa wananchi na mali zao.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Najma Giga aliipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuendelea kushirikiana na Kamati kuhakikisha sheria mpya inatungwa kama hatua ya kuzuia na kukabili maafa ambayo husabababisha athari kubwa.
Naye mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Zainabu Katimba alishauri uundwaji wa Kamati Elekezi ya Kitaifa uzingatie sekta badala ya Wizara ambayo huwa na usimamizi wa jumla wa utekelezaji wa maafa.