24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali kugharamia matibabu ya majeruhi ajali ya moto Morogoro

Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Rais John Magufuli amesema serikali itagharamia matibabu ya majeruhi wa ajali ya lori lililolipuka na kuwa moto mkoani Morogoro jana Jumamosi Agosti 10.

Aidha, Rais Magufuli pia amewataka Watanzania kutokuwa majaji na wepesi wa kuhukumu bila kufahamu chanzo cha ajali hiyo.

Rais Magufuli amesema hayo leo Jumapili Agosti 11, wakati alipowatembelea baadhi ya majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

“Niwaombe Watanzania tuendelee kuwaombea huu si wakati wa kulaumu kwa sababu nimesikia wengine wanasema walikuwa wameenda kuiba mafuta.

“Tusihukumu bila kufahamu chanzo kwa sababu kuna mmoja amesema alikuwa kwenye lori jingine alivyoona ajali akashuka ili akatoe msaada lakini aliungua, kwa hiyo si wote walikwenda kuiba mafuta wengine walikwenda kutoa msaada.

“Yupo mwingine alikuwa anasema anasafiri kwenda Mtwara wakazuiwa, akaungua. Sisi tusiwe majaji kwa sababu si kila mmoja alikuwa anakwenda kuiba mafuta wengine walikuwa wanapita njia tu,” amesema Rais Magufuli.

Aidha, akiwa hospitalini hapo Rais Magufuli alipokea taarifa kuwa majeruhi waliofikishwa Muhimbili walikuwa 46 ambapo watatu kati yao wamefariki huku wengine 15 wakiendelea na matibabu mkoani Morogoro.

Rais Magufuli pia amewashukuru madktari na wauguzi hospitalini hapo kwa kuwahudumia wagonjwa hao kwa njia mbalimbali na kuokoa maisha yao ambao wengi wao wameungua vibaya.

“Muhimbili imebadilika sana huduma ni nzuri najua mna changamoto nyingi sana serikali tunatakiwa kuzitatua lakini tunaomba mjitahidi hivyo hivyo,” amesema.

Akiwa hospitalini hapo, Rais Magufuli amewatembelea majeruhi hao na kuwapatia Sh 500,000 kila mmoja na madaktari na wauguzi wanaowahudumia wagonjwa hao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles