Serikali kufungua mashamba 16 ya mboga mboga na maua yaliyotelekezwa

0
287

Na Upendo Mosha,Arusha

Serikali imesema itayafungua mashamba 16 ya mboga mboga na maua yaliotelekezwa na wawekezaji katika mkoa wa Arusha kutokana kushindwa kulipa mikopo waliyokopa katika taasisi mbalimbali za kifedha.

Waziri wa Kilimo, Prof Adolf Mkenda. ameyasema hayo wakati wa ziara ya kuyatembelea mashamba hayo, jijini Arusha, ambapo amesema serikali itaanda utaratibu wa kuyarejesha katika uzalishaji kama ulivyokuwa awali pasipo kuathiri upande wowote.

“Serikali itahakikisha inayafungua mashamba yote 16 ya maua nimeelezwa yaliofungwa kwa sababu nyingi Ila kubwa ni mikopo ..serikali itayafungua bila kuathiri upande wowote benki wanazo taratibu zao Ila mashamba haya hayawezi kubaki bila kazi ni hasara kubwa sana tunapata,”amesema Prof. Mkenda.

Amesema kutelekezwa kwa mashamba hayo kumesabaisha upotevu wa mapato pamoja na ajira hivyo serikali haitakuwa tayari kuona yakiendelea kutekelezwa na kugeuka kuwa kichaka.

“Mauaridi hatuuzi tena nje na mikopo hailipwi kutokana na mashamba haya kutelekezwa baada ya wawekezaji kukopa mikopo ya kimagumashi na kukimbia cha muhimu ni kuhakikisha mashamba yanaendelea na uzalishaji maana waliokopa wanajulikana,” amesema.

Mbali na hilo ameshangazwa na namna wawekezaji hao walivyoshindwa kulipa mikopo hiyo jambo ambalo alisema huenda kukawa na mchezo mchafu katika utoaji wa mikopo hiyo.

“Haiingii akilini kampuni ilikuwa ikifanya faida na kushindwa kulipa ghafla kunauwezekano mkubwa kuna mchezo mchafu tutaona cha kufanya katika hili ..lakini kubwa tutayafungua na kutafuta wawekezaji wengine na biashara hii iendelee tuendelee kupata fedha”alisema

Akizungumzia suala la masoko bidhaa za mazao yanayoenda chini Kenya,alisema serikali inaunga mkono suala hilo kwa lengo la wakulima kupata masoko ya mazao yao.

“Ni vema na haki mazao yanayozalishwa hapa nchini kwenda Kenya maana wakulima wanahitaji soko,matunda yauzwe popote pale mpaka hapo tutakapotatua changamoto ya ukosefu wa masoko,” amesema.

Aidha, amesema wizara hiyo itahakikisha inatafuta ufumbuzi wa changamoto za masoko na usafirishaji wa bidhaa zinazotokana na mazao mbalimbali hapa nchini sambamba na kuhamasisha uzalishaji.

“Tunafahamu mnakabiliwa na changamoto nyingi za kibiashara Ila tunaomba muendelee na kazi hii itasaidia kuongezeka kwa uzalishaji…tunauhakika wawekezaji watakuja wengi na sisi tunapambana Kama wizara uzalishaji ukue katika mazao yote,” amesema.

Akizungumzia suala la mazao mbalimbali kuharibika ikiwemo nyanya katika msimu mbalimbali,aliiitaka taasisi ya uzalishaji wa mbogamboga na matunda (TAHA) kuja na mpango mkakati utakaweza kutoa ufumbuzi wa tatizo hilo na kwamba serikali itaiwezeasha.

“Kumekuwa na sababu nyingi za kitaalamu zinazosababisha nyanya na matunda yetu kutokuwa na vigezo vya kuongezeea thamani na kipindi cha msimu kutupwa barabarani tunaomba mfanye kazi hilo suala serikali itawawezesha lengo letu ni kuhakikisha tunaongeza thamani mazao yetu,”amesema.

Awali, akizungumzia sakata la kufungwa kwa masamba 16 ya kilimo cha maua na mbogamboga, Mkurugenzi mtendaji taasisi ya uzalishaji wa mbogamboga na matunda (TAHA), Dkt Jacqueline Mkindi,alisema ufungwaji wa mashamba hayo umesababisha hasara kubwa kwa taifa ikiwemo ukosefu wa ajira zaidi ya 6000

“Mashamba takiribani 10 ya maua na mashamba sita ya mbogamboga yamefungwa walichukua mkopo wakashidwa kurudisha na soko la maua duniani liliyumba lakini katika kilimo cha mbogamboga sababu ninmazingira magumu ya kibishara nchini”alisema

Alisema mbali na kupotea kwa ajira pia serikali imekuwa ikipoteza zaidi ya Dola milioni 24 kwa mwaka Jambo ambalo aliiomba serikali kuharakisha mchakato wa kuyachukua na kukabidhi wawekezaji wenye uwezo wa kuyaendesha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here