23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali kufungia maabara 700

Na VERONICA ROMWALD

 – DAR ES SALAAM

SERIKALI imetangaza kuwafungia baadhi ya wamiliki wa maabara binafsi ambao hawajatii agizo la sheria la kusajili vituo vyao hadi Januari 15 mwaka huu.

Akizungumza Dar es Salaam jana,  Mkurugenzi wa Huduma za Tiba katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima alisema hawatasita kuzifungia maabara hizo na kuwafikisha mahakamani wamiliki.

Dk Gwajima ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi wa maabara binafsi za afya nchini (PHLB) alisema hadi kufikia Septemba, 2018, walikuwa wanazitambua maabara 641 zinazojitegemea na 719 zilizoshikizwa kwenye vituo vya tiba vya watu binafsi vya ngazi mbalimbali.

“Hatutasita kuzifungia maabara ambazo wamiliki wake hawatalipa malimbikizo ya ada na tozo zote wanazodaiwa, tumeshakamilisha kuyachambua madeni yao, sasa tunayadadavua kulingana na madaraja yao, ambayo ni Class A, B na C,” alibainisha.

Aliongeza “Tutawawajibisha kwa mujibu wa sheria….tunawataka wapige hesabu za madeni ya nyuma, wajisalimishe wenyewe, walifanya biashara, wamepata faida.

“Lazima watupe fedha za tozo wanazotakiwa kulipa kisheria, tunahitaji hizo fedha, waende wakalipie kwa njia ya benki, watuletee risiti halali,” alisema.

Aidha alisema bodi hiyo imebaini baadhi ya wamiliki wa maabara binafsi hususan zilizoshikizwa ndiyo ambao hawafuati maadili ya uwajibikaji kisheria.

“Tumebaini wamiliki wengi wasiotekeleza sheria ya umiliki wa maabara binafsi wanatokea miongoni mwa wanaomiliki maabara zilizoshikizwa, yaani zilizomo ndani ya vituo vya tiba ngazi mbalimbali.

“Aidha katika kundi hili, wapo watu ambao kimsingi huwezi kuwatarajia kutokana na elimu zao, kazi zao na imani zao kwa jamii inayowazunguka (wao wanajijua). hii haivumiliki kabisa.

Kwa kuwa mimi nilikuwa mstari wa mbele kuwafikia wale wamiliki wa maabara binafsi walioripotiwa kwamba eti wameshindikana, nimewafikia baadhi yao na kusikiliza hoja zao na kubaini hazina mashiko kabisa.

“Hoja yao ya msingi wanadai wanapolipia kusajili kituo cha tiba huwa wanadhani tayari na maabara imejumuishwa humo.

“Utetezi huu si wa kweli kwani sheria ya kusimamia umiliki wa vituo binafsi vya tiba iko wazi na ina bodi yake na hii ya kusimamia umiliki wa maabara binafsi nayo iko wazi na ina bodi yake na siku zote wamekuwa wakielimishwa na mimi nimeshiriki mara  nyingi kutoa elimu hiyo,” alisema.

Dk Gwajima alisema hadi kufikia Septemba 2018, kati ya vituo vya tiba 1713 vya watu binafsi vyenye maabara ndani ni maabara 1012 sawa na asilimia 58 ndizo zilizotimiza wajibu wa kujiandikisha kwenye bodi na kutekeleza matakwa yote kisheria.

“Ili kuepuka adhabu ni vema kila mmiliki ahakikishe amekidhi vigezo vyote vya kumiliki maabara binafsi kama ambavyo amekuwa akielekezwa na wataalamu walioko kila halmashauri na mikoa husika.

“Kila mmiliki ahakikishe amelipa ada na tozo stahiki zikiwemo malimbikizo ya nyuma na faini zote stahiki na amepata risiti halali za malipo hayo,” alisisitiza Dk. Gwajima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles