Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Serikali imewahakikishia wakulima na wamiliki wa viwanda vya kukoboa Kahawa nchini kuwa itatengeneza utararibu wa kuuza kahawa ili kuwa na mfumo wa uwazi wenye bei itakayomnufaisha mkulima kwa kuchagua bei anayoitaka.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) alipofanya ziara ya ukaguzi katika Kiwanda cha Kupokea na Kukoboa Kahawa aina ya “Arabica” (Mbinga Coffee Curing Company) kilichopo Mbinga, mkoani Ruvuma Septemba 20, 2024.
“Lazima tuongeze tija kwa wazalishaji wa kahawa. Hivyo, niwahakikishie kuwa Serikali itaendelea kutoa miche ya ruzuku ya kahawa ambayo inazalishwa na TACRI, tutaanzisha mfumo wa ruzuku za pembejeo, tutachimba visima kusaidia wakulima na kujenga ghala la kuhifadhi kahawa zao,” amesema Waziri Bashe.
Kuhusu wafanyabiashara wanyonyaji kwa wakulima (kangomba), Serikali itachukua hatua dhidi ya unyonyaji huo kwa wakulima. Waziri Bashe amesema kuwa ushirika imara siyo unaonyonya wakulima; na hivyo wakulima kupitia vyama vya ushirika na waliopo katika vikundi mbalimbali washiriki katika mfumo wa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) linalosimamia mnada wa kijiditali ili kuwaongezea uhakika wa masoko, uhuru wa kuamua bei, uhakika wa malipo yao pamoja na kuchochea ushindani.
Aidha, Waziri Bashe amehamasisha wazalishaji wa Kahawa nchini kama vile aina ya Mbinga Café kuwa na kampeni bunifu za kunadi upekee / utofauti wa kubidhaisha Kahawa zao ili kuvutia biashara. Ametolea mifano kama vile hadithi au simulizi kuhusu Kahawa ya kampuni fulani, au viungo / ladha / virutubisho vilivyomo kwenye Kahawa husika.
Mbinga Coffee Curing Company inamilikiwa na Vyama vya Ushirika 28 vinavyolima Kahawa nchini kwa asilimia 56.54, huku Serikali ikimiliki asilimia 43.46 ambapo kiwanda chake kilianza ukoboaji wa Kahawa mwaka 1989. Kiwanda kina uwezo wa kukoboa tani 10 kwa saa moja, na uwezo wa kukoboa tani 30,000 kwa mwaka.