Na Farida Ramadhani WFM – Dodoma
Serikali imeeleza kuwa itaendelea kuboresha maslahi ya watumishi wa umma na kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zinazowakabili Watumishi ili kutimiza ahadi ya Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) alipokuwa akifungua Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo.
Nchemba alisema baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita ni pamoja na kulipa malimbikizo ya mishahara kwa watumishi wa umma ambapo zaidi ya Sh bilioni 34 zimeshalipwa.
“Serikali imetoa mikopo ya vyombo vya usafiri ya jumla ya takribani Sh bilioni 79 ikiwa ni utekelezaji wa Waraka wa Watumishi wa Serikali Na. 3 wa mwaka 2011 kuhusu utaratibu wa kukopesha fedha taslimu watumishi wa Serikali ili kuwawezesha kununua magari/pikipiki, samani na matengenezo ya magari na pikipiki,” alisema Dk. Nchemba.
Alisema Serkali imefanyia kazi suala la nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma, viwango vya posho ya kujikimu na posho ya kufanya kazi baada ya masaa ya kazi pamoja na kupandisha vyeo watumishi.
Aidha, aliwataka watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango kufanyakazi kwa weledi, uzoefu, ubobezi, maadili na ukomavu katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuwa Wizara hiyo ni miongoni mwa Wizara nyeti za Serikali kutokana na muundo na majukumu yake.
“Hii ndio fursa ya kujimulika, kabla hatujaanza kuwanyooshea kidole wale tunaowapelekea fedha lazima sisi tuoneshe kwamba tunaweza kutunza fedha na tuonekane hivyo kwamba tunaweza kutunza fedha za umma”, alibainisha Dk. Nchemba.
Alisema kwa kuwa Wizara hiyo ni moyo wa Serikali ni vyema watumishi wa Wizara ya Fedha wakawa mfano wa kubana matumizi kwa kuepuka matumizi yasiyo ya lazima kama ambavyo imekuwa ikisisitiza kwa Wizara na Taasisi nyingine kuhusu masula ya matumizi bora ya fedha za umma.
“Masuala mengi, na muhimu ya kitaifa yanaratibiwa na Wizara ya Fedha na Mipango, hususan miradi mikubwa ya kimkakati inayohitaji utafutaji wa rasilimali fedha, ni lazima wataalamu wetu washirikishwe katika kufanikisha masuala ya kitaifa,” alifafanua Nchemba.
Aliwataka watumishi wa Wizara hiyo kutumia vizuri fursa mafunzo ya muda mfupi na mrefu inayotolewa na Wizara hiyo ikiwa ni pamoja na fursa ya ufadhili wa masomo zinazotolewa na nchi wahisani ili kujiendeleza na kupata maarifa zaidi.
“Mpango wa mafunzo ni lazima uzingatiwe na uwe shirikishi kwa watumishi wakati wa maandalizi na utekelezaji wake, mpango wa mafunzo siyo hiari ya kiongozi, ni haki ya mtumishi, hivyo, kila mtumishi apewe nafasi, hasa wale wa mikoani,” alifafanua Nchemba.
Alisema hatarajii kusikia watumishi wenye vyeo vya chini kubaguliwa katika fursa za mafunzo kwa kuwa kila mtumishi ana mchango katika taasisi, hivyo kila mtumishi apewe nafasi ya kuongeza maarifa na ujuzi.
Aliagiza Wizara hiyo iwe inafanya vikao mara kwa mara na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango ili kujenga jukwaa la kujadli na kubadilishana taarifa kuhusu masuala mbalimbali ya kiutendaji na kupatiwa taarifa ya utekelezaji wa vikao hivyo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Hassan Chande (Mb) alitoa rai kwa watumishi wa Wizara hiyo kufanyakazi kwa bidii kwa maendeleo ya nchi huku akieleza kuwa kufanyakazi pia ni ibada.
Aliwapongeza watumishi na watendaji wote wa Wizara kwa kufanyakazi kwa juhudi na kubainisha kuwa anaamini baraza hilo litaleta matokeo chanya yanayohitajika katika jamii.
2.
3.
Manaibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Amina Shaaban na Bw. Lawrence Mafuru na baadhi ya wakuu wa Idara na Vitango wa Wizara hiyo wakiimba wimbo wa umoja na mshikamano katika Baraza la Wafanyakazi lililofanyika jijini Dodoma.