SERIKALI KUDHIBITI URASIMU VIBALI VYA UWEKEZAJI

0
677
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage

Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam

SERIKALI imesema itadhibiti urasimu katika utoaji wa vibali vya uwekezaji ili kufikia ajenda yake ya viwanda.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam juzi na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage wakati wa mkutano wa 58 wa mwaka wa Chama cha Waajiri Nchini (ATE).

“Serikali inayo taarifa na inajua kwa muda mrefu malalamiko ya wawekezaji kuwa si tozo na kodi bali ni urasimu uliojengeka katika ofisi nyingi za Serikali, tunalishughulikia ili kutengeneza mazingira mazuri na bora ya uwekezaji,” alisema.

Mwijage alisema dhamira ya Serikali ni kutengeneza ajira kwa wananchi na kupunguza makali ya maisha kwa kuimarisha kipato cha mtu mmoja mmoja.

“Asilimia 60 ya dhamira ya Serikali katika uanzishwaji wa viwanda nchini ni kupambana na tatizo la ajira na umasikini, ila Serikali haitajenga viwanda ila itaongoza na kuonyesha njia kwa waajiri na sekta binafsi kwa ujumla kuvijenga,” alisema.

Akijibu hoja za waajiri kuhusu upunguzaji wa wafanyakazi katika sekta binafsi, alisema mdororo wa uchumi ni wa dunia nzima na si Tanzania peke yake na kutaka wawekezaji kujipanga baada ya Serikali kupitia bajeti ya mwaka 2017/2018.

Pia alisema Serikali ipo tayari kuendelea kushirikiana na sekta binafsi na waajiri kwa ujumla ili kupunguza gharama za kufanya biashara na uwekezaji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa ATE, Almasi Maige, alisema waajiri wana manung’uniko juu ya tozo ya ujuzi ya kutoka asilimia tano kwenda asilimia 4.5 na kwenda kufadhili Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

Alisema ni muhimu kwa Serikali kulitazama jambo hilo kwa jicho la kipekee kwa sababu linaongeza gharama ya ulipaji wa mishahara kwa wafanyakazi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Dk. Aggrey Mlimuka, alisema waajiri wanaona tozo hiyo ni kama kodi iliyojificha na inaendelea kuwaumiza kwa kiasi kikubwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here