Na Amina Omari, TANGA
WAZIRI wa Fedha, Dk. Philip Mpango, ameziagiza benki zote nchini kuwachunguza watumishi ambao si waadilifu na katika benki kudhibiti wimbi la wahalifu ambao umekuwa ukitokeza kila wakati kwa kuwahusisha wafanyakazi wa benki nchini.
Hayo aliyasema Tanga jana alipokuwa akizindua tawi la Benki ya Kiislamu ya Amana.
Alisema Serikali haitasita kuzichukulia hatua kali za sheria benki zote zitakazobainika kuwalinda watendaji wao ambao si waadilifu.
Waziri alilitaka Jeshi la Polisi kuongeza nguvu za upelelezi kudhibiti wimbi la uhalifu wa benki ambao umekuwa ukijitokeza mara kwa mara nchini.
“Imekuwapo tabia kwa baadhi ya wafanyakazi wa mabenki kushirikiana na wahalifu kwa kutoa siri mteja anapotoka kutoa fedha nyingi benki.
“Sasa ni lazima benki zote zianze na kufanya ukaguzi na uchunguzi kwa wafanyakazi wake,” alisema Dk. Mpango
Aliwataka Watanzania kuacha kukimbilia kukopa kwenye taasisi zinazotoa riba kubwa ambazo zimekuwa zikitaifisha mali zao mteja anaposhindwa kulipa fedha alizochukua.
Awali akizungumzi kuhusiana na benki ya Amana, Dk. Mpango, alisema benki hiyo itakuwa mkombozi kwa wananchi ambao walikuwa wanashindwa kutumia benki nyingine kutokana na kuwapo mfumo wa riba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Amana, Dk. Muhsin Masoud, alisema wamejikita kutoa huduma za benki za kisasa kwa kuzingatia mfumo wa maadili ya dini ya kiislamu kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Alisema tangu ilipoanzishwa benki hiyo dhamana yake imekuwa na kufikia zaidi ya Sh bilioni 192.
“Tayari uwezeshaji wa biashara kupitia sekta mbalimbali zimeweza kufikia Sh bilioni 143 kwa sekta tofauti za uchumi hapa nchini,” alisema Dk. Masoud.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella, aliishauri benki hiyo kutumia fursa za miradi mikubwa ya uchumi inayotarajiwa kuwekezwa mkoani Tanga kwa kusogeza huduma zao karibu.