SERIKALI imeshauriwa kuboresha masilahi ya watoa huduma za afya ili wafanye kazi kwa moyo na kuepuka kukimbilia nje ya nchi kutafuta masilahi mazuri zaidi.
Wakizungumza katika semina ya haki afya na jinsi ya kuwasilisha malalamiko kwa njia ya ujumbe mfupi kupitia simu ya kiganjani iliyoandaliwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) iliyokutanisha makundi mbalimbali kutoka Mkoa wa Mwanza juzi, baadhi ya washiriki walisema endapo Serikali itaboresha masilahi ya watoa huduma za afya, itapunguza tatizo la wataalamu wa afya kwa kiasi fulani na hivyo kuwashawishi wale walioko nje nao kurejea.
Mmoja wa washiriki hao, Fatuma Mnahwate, alisema huduma zimekuwa duni kutokana na madaktari wengi kukimbilia nje na kushauri iwapo wataboreshewa masilahi yao, wengi watabaki nchini.
“Ili kuboresha upatikanaji wa haki afya, pia Serikali ifanye ukaguzi wa mara kwa mara katika vituo vya kutoa huduma za afya hasa vijijini ambako wananchi wengi wanaishi huko na adhabu kali zitolewe kwa wafanyakazi wanaoenda kinyume na maadili ya kazi zao,” alisema Fatuma Mnahwate.
Kwa upande wake, Mtafiti kutoka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Julius Siza, alisema asilimia 40 ya madaktari wanaishi na kufanya kazi nje ya nchi, hali inayozorotesha utoaji wa huduma.
Akizungumza na MTANZANIA, Mratibu wa Mifumo ya Habari na Mawasiliano wa THBUB, Wilfred Warioba, alisema lengo la semina hiyo ni kuwezesha makundi maalumu kupata elimu ya haki afya na kujua jinsi ya kuwasilisha malalamiko katika ofisi zao kwa njia ya ujumbe mfupi.
Alisema wametoa semina hiyo kupitia Mradi wa Matumizi ya Teknolojia ya simu ya kiganjani katika kuwasilisha malalamiko THBUB kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Sweden (Sida) kupitia Mtandao wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika kukuza demokrasia kwa njia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT For Democracy East Africa).
“Tulianza kuutekeleza mradi huu mwaka 2013, tunatarajia kuukamilisha mwaka huu, hadi sasa tumepata mafanikio mengi ikiwamo kuwafikia watu wengi hasa vijana,” alisema.