25.2 C
Dar es Salaam
Friday, August 12, 2022

Serikali  kuanzisha kituo kimoja kulipia kodi zote

matunda-copyNA HARRIETH MANDARI-Mkuranga, Pwani.

ILI  kufanikisha azma ya Viwanda ya  Rais  wa awamu ya tano, Dk John Magufuli ni muhimu kwa serikali kuweka mazingira mazuri  kwa wawekezaji  hasa kwa upande wa  upatikananji wa ardhi, upatikananji wa leseni za biashara hasa za vinywaji, na chakula ambazo kumekuwa na urasimu ambao husababisha zoezi la upatikananji vibali   kuchukua muda mrefu  na hivyo imekuwa inaleta usumbufu kwa wawekezji.

Tangu aingie madarakini Novemba 5, Rais Magufuli  alitoa dira na mwelekeo wake juu ya kuipeleka Tanzania  kwenye maendeleo ya viwanda na uchumi wa kati, moja ya msisitizo aliotoa ni kwa serikali yake kuhakikisha kwamba inaandaa mazingira mazuri kwa ajili ya wawekezaji wake hasa wa ndani.

Wiki iliyopita, Rais Magufuli alizindua viwanda vinavyomilikiwa na kampuni ya Bakhresa Food Producion Ltd.  cha kusindika matunda kilichopo Mwandege wilayani Mkuranga, Mkoani Pwani,  ambapo aliendelea kusisitiza nia ya Tanzania kuhakikisha wawekezaji wanapata mazingira mazuri ya kuwekeza bila urasimu usio wa lazima kwa nia ya kuchochea maendeleo ya uchumi nchini kupitia sekta hiyo.

Akizungumza mara baada ya uzinduzi huo, Dk Magufui aliwataka wafanyabiashara wengine nchini kuanzisha viwanda vingi vya aina mbalimbali kama ilivyo kwa Bakhressa  ambapo kwa kufanya hivyo kumewezesha kutoa ajira nyingi kwa Watanzania na pia kuwainua kwa kuwapatia soko la uhakika wakulima hasa wa matunda nchini.

“Tangu niingie madarakani hiki ndio kiwanda cha kwanza kukizindua na kwa mwenendo mzuri wa kiwanda hiki, mazao ya wakulima hayatakuwa yanaharibika tena kwani wataendelea kupata soko la uhakika,”alisema.

Akaongeza kuwa amefurahi kuona kiwanda kinatumia matunda yanayolimwa na wakulima  nchini na kwamba  serikali inataka Watanzania wapate ajira kupitia sekta ya viwanda kwa asilimia 40.

“Kwa sasa sekta ya viwanda inachangia pato la taifa kwa asilima 7.3 na sisi tunataka ifikie asilimia 15,”aliongeza.

Aidha katika hatua nyingine, Rais Magufuli alimuomba Mwenyekiti wa Makampuni ya Bakhresa kuangalia uwezekano wa kufanya uwekezaji kama huo katika maeneno mengine ya kikanda ili kutoa fursa zaidi kwa wananchi wanaoishi katika maeneo hayo kupata soko la uhakika wa bidhaa zao.

Naye Waziri wa Viwanda,  Biashara  na Uwekekzaji, Chalres Mwijage  aliwataka wawekezaji wengine wazawa kuwekeza kwenye sekta mbalimbali ili kuinua nchi kiuchumi.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa kampuni ya Bakhresa, Yusuph Bakhresa aliipongeza serikali kwa kutoa ushirikiano mzuri kwa wafanyabiashara wenye viwanda nchini, hali ambayo amesema itasaidia kufikia lengo la serikali ya awamu ya tano ya kuwa na uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

Kwa upande wa changamoto kiutendaji, Yusuph alisema urasimu na tozo kubwa bandarini wakati wa kuingiza  vifungashio vya vinywaji hivyo hasa makasha ya kuhifadhia juisi ni changamoto kubwa katika uzalishaji.

“Kumekuwa na utozaji wa kodi kubwa katika makasha ya kuhifadhia viywaji ambayo huwa tunaagiza kutoka nchi za nje, jambo ambalo linaleta usumbufu kiutendaji,”alisema.

Naye Meneja mawasiliano wa kampuni ya Azam, Hussein Ally alisema kiwanda hicho kimeweza kutoa ajira 600 kwa Watanzania,  ambapo kati ya hizo wenye ajira za kudumu ni  380.

Akaongeza kuwa kiasi cha dola milioni 120 zimewekezwa katika viwanda hivyo nchini.

“Katika kipindi cha nyuma tulikuwa na wataalamu mbalimbali kutoka nchi za nje lakini tumepunguza na kwa sasa tunao wataalalmu 40 tu,”alisema.

Kampuni ya Azam ina jumla ya viwanda 13 ambapo viwanda 11 vipo  mkoani Dar es Salaam na vingine viwili vipo mkoani Pwani. Katika kipindi cha mwaka 2015/16, kampuni hiyo imelipa kodi kiasi cha shilingi bilioni 54.

Naye Mkuu wa mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alisema kufikia mwaka 2015, Mkoa wa pwani utakua ukanda wa viwanda ambapo hadi sasa kuna viwanda 53  kimojawapo kikiwemo kiwanda cha vigae kinachozalisha bidhaa zao kwa wingi na kilicho kikubwa kuliko vyote Afrika ya Mashariki .

Changamoto nyingine zilizoainishwa katika uzalishaji wa viwanda hivyo ni pamoja na kutokuwa na umeme wa uhakika, urasimu wakati wa kuingiza sukari ya viwandani katika bandari ya Dar es Salaam na watoza kodi kuwa wengi ambao kiutendaji wanafanya kazi aina ile ile.

Rais Magufuli aliahidi kulifanyia kazi kwa kuweka utaratibu ambao tozo zote zitatozwa mahali pamoja’One stop centre’ badala ya watoza kodi mbalimbali kwenda kutoza kodi kila  wakati   hali ambayo imekuwa ikileta usumbufu kwa wafanyabiashara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,526FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles