24.8 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali Kenya yakiri deni la Sh trilioni 100 mzigo

NAIROBI, KENYA

HATIMAYE Serikali ya Kenya imeeleza hofu yake kuwa huenda ikashindwa kulipa madeni yake ya kigeni, ikisema mapato yake ni madogo kulinganisha na deni la Sh trilioni 5.3 za Kenya (zaidi ya Sh trilioni 106 za Tanzania).

Kwa mujibu wa hati kuhusu Mkakati wa Usimamizi wa Madeni ya Serikali (MTDMS) 2019, Waziri wa Fedha Henry Rotich amependekeza kupunguzwa kwa ukopaji kutoka nje ili kupunguza hofu ya kushindwa kulipa madeni ya sasa.

Rotich alisema kupungua kwa kiwango cha mapato ya kigeni ndiko kulikokwamisha juhudi za nchi kulipa madeni yake yaliyofikia Sh trilioni 5.3 za Kenya mwishoni mwa mwaka 2018.

Kwa hivyo, kupitia hati hiyo iliyowasilishwa bungeni Alhamisi iliyopita na Kiongozi wa Wengi, Aden Duale, Waziri Rotich alipendekeza katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2019/2020, mikopo ya kigeni idhibitiwe ili isipite asilimia 38 ya mapato ya kigeni huku yale ya ndani yakiongezwa hadi asilimia 62.

Mbinu nyingine ambayo Hazina inapanga kutumia kupunguza mzigo wa madeni, ni kutenganisha ukopaji kutoka nje na ule wa ndani, ili kutoathiri uwezo wa sekta binafsi kupata mikopo katika soko la fedha.

“Tunapendekeza kudhibiti mikopo kutoka nje kuwa asilimia 38 ya mapato kutoka nje na asilimia 62 kwa mikopo kutoka humu nchini,” alisema Rotich katika stakabadhi hiyo iliyowasilishwa bungeni sambamba na bajeti ya 2019/20 ya Sh trilioni 2.7 za Kenya (zaidi ya Sh trilioni 54 za Tanzania).

Kufikia sasa Kenya inadaiwa zaidi ya Sh trilioni 52 za Tanzania inazotakiwa ilipe haraka iwezekanavyo, kiwango ambacho ni nusu ya zaidi ya Sh trilioni 106 jumla ya fedha zote inazodaiwa.

Kupunguzwa kwa kiwango cha mikopo kutoka nje inayolipiwa riba ya juu, kunaashiria kuwa Waziri Rotich anapanga kuzuia mikopo kupitia hati ya dhamana ya Eurobond.

Miaka ya 2015 na 2017 mrengo wa upinzani wa  NASA ulipinga mikopo hii ukidai kuwa Sh bil 275 za Kenya zilizokopwa kwa njia hii zilifujwa au kuibwa.

Serikali ilijitetea kuwa imekuwa vigumu kwake kupata mikopo ya riba ya chini kwa sababu Kenya inaorodheshwa kama taifa lenye mapato ya kadiri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles