28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

SERIKALI, KAMATI YA BAJETI KUJADILI ONGEZEKO BEI YA PETROLI

Na MAREGESI PAUL-DODOMA

SERIKALI imekubali kukutana na Kamati ya Bunge ya Bajeti ili kuangalia jinsi ya kuongeza Sh 50 katika bei ya petroli na dizeli ili zipatikane fedha za kutekeleza miradi ya maji nchini.

Makubaliano hayo yalifikiwa bungeni juzi, wakati wabunge walipokuwa wakihitimisha mjadala wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji, iliyowasilishwa mwanzoni mwa wiki na Waziri wa Wizara hiyo, Gerson Lwenge.

Katika maelezo yake bungeni, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashantu Kijaji, alisema Serikali ililazimika kufikia uamuzi huo baada ya wabunge kuonyesha umuhimu wa kuongezwa kwa tozo hiyo katika mafuta, ili kukabiliana na uhaba wa maji nchini.

“Wabunge, maji ni muhimu na ni siasa, kama alivyosema Selasini wakati akichangia hapa.

“Kuhusu pendekezo la kuongeza tozo la shilingi 50 kwa kila lita ya mafuta, tutakaa sisi, Wizara ya Maji na Umwagiliaji pamoja na Kamati ya Bunge ya Bajeti, ili tuangalie njia sahihi ya kupata fedha za kutatua kero hiyo,” alisema Dk. Kijaji.

Awali, wakati mjadala huo ukihitimishwa, Mbunge wa Hanang, Dk. Mary Nagu (CCM), aliitaka Serikali ieleze jinsi itakavyopata fedha za kukabiliana na uhaba wa maji, huku akiwataka wabunge wenzake wamuunge mkono katika hoja hiyo.

Naye Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini, aliunga mkono hoja hiyo kwa kuwa hakukuwa na sababu za kupunguza fedha za maendeleo za bajeti hiyo kutoka zaidi ya Sh bilioni 900 zilizopitishwa na Bunge katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2016/2017 hadi Sh bilioni zaidi ya 600 za mwaka huu wa bajeti.

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu, Cecilia Paleso (Chadema), aliunga mkono hoja hiyo na kusema hakuna njia mbadala ya kupata fedha za kutatua kero ya maji nchini kama tozo ya Sh 50 haitaongezwa katika mafuta hayo.

Naye Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), alisema lazima Serikali ikubali kuongeza fedha hizo ili kuwaondolea kero ya maji wanawake ambao ndio waathirika wakubwa.

Wabunge wengine walioonyesha kutoridhishwa na uhaba wa maji nchini kabla Bunge halijapitisha bajeti ya wizara hiyo, ni Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF) na Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia (CCM).

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,085FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles