23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali isikilize kilio cha NGO’s isiwapuuze

ASHA BANI

OKTOBA 12 mwaka huu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, kwa kutumia mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 38 cha sheria ya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), alitangaza kanuni za sheria ya mashirika yasiyo ya Kiserikali (marekebisho ya mwaka 2018).

Tamko hilo la Serikali lilitolewa ili lisomeke kwa pamoja na Kanuni za Mashirika yasiyo ya Serikali ya 2004 GN. Na. 152/2004, ambazo zilitajwa kama kanuni kuu.

Katika kanuni hizo kulikuwa na vipengele vingi ambavyo kwa namna moja ama nyingine vinaweza kuminya uhuru wa NGO katika kutoa maoni, kukosoa Serikali na hata jamii endapo inafanya mambo kinyume na taratibu au haki za binadamu na utawala bora nchini.

Kuna kipengele cha uwazi wa kifedha na uwajibikaji ambacho kinayataka mashirika yasiyo ya kiserikali kuweka wazi shughuli zautafutaji fedha ikiwa ni pamoja na vyanzo vya fedha hizo au rasilimali zinazopatikana.

Matumizi ya fedha au rasilimali zilizopatikana, kusudi la fedha au rasilimali, shughuli zitakazofanywa kutoka kwenye fedha au rasilimali zilizopatikana.

Pia kuna kipengele ambacho kinaeleza kuwa mashirika yasiyo ya Serikali ambayo yamepata fedha zaidi ya shilingi milioni ishirini yanapaswa kuchapisha mara mbili kwa mwaka fedha zilizopokelewa na matumizi yake katika magazeti mbalimbali na njia nyingine za vyombo vya habari ambavyo vinaweza kupatikana kwa urahisi kwa wanufaika na walengwa.

Pia kulikuwa na kifungu kinachomtaka mfadhili au wafadhili anayetoa fedha hizo kuwasilishwa kwenye hazina na msajili kabla ya siku kumi tangu tarehe ya kuingia mkataba huo au makubaliano ili kuweza kuidhinishwa na kutangaza kwa msajili wa mashirika yasiyo ya Serikali rasilimali nyingine zozote zilizopokelewa taslimu au kwa aina nyingine kabla yakufanya manunuzi yake.

Kulikuwa na kipengele cha uwazi wa kifedha nauwajibikaji ambapo mashirika yasiyo ya kiserikali yatalazimika kuendeleza na kuzingatia kwa uwazi na kanuni zilizopo za kifedha ambazo zinaendana na kanuni za udhibiti bora wa kifedha.

Pia kutokuingilia mikataba ambayo inaminya uhuru wa nchi na haki za watu na kufanya kazi kulingana na sheria za nchi pia.

Kanuni hizo mpya zimeongeza sehemu ya nne katika kanuni za Sheria ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2004 ambayo sasa inajulikana kama sehemu ya IV inayojulikana kama uwazi wa kifedha na uwajibikaji.

Katika kanuni hizo Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), uliunga mkono kwa kueleza kuwa zina lengo lakuhakikisha uwazi wa kifedha na uwajibikaji unafanyika si jambo baya.

Kutokana na hali hiyo, ndiyo sababu zilizoelezwa na mratibu wa mtandao wa THRDC, Onesmo Olengurumwa wa kuwaunganisha wanachama wake  na wadau mbalimbali katika mkutano kwa ajili ya kukuza ufahamu kati yao kuhusu maudhui ya kanuni hizo.

Hata hivyo, katika mapitio ya kanuni na sheria hizo, Azaki zimetoa maoni ya changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na masikitiko yao katika vipengele kadhaa vya kanuni na kuiomba Serikali kukaa pamoja kuweza kujadili na kubadili baadhi ya kanuni ambazo kwa namna moja ama nyingine zinaonyesha kuwakandamiza.

Ni kweli linaweza kutokea hilo hasa pale kwenye kipengele cha kufuata utaratibu wa fedha zao kupitia kwa msajili kuhakikiwa na hata kueleza matumizi ya fedha hizo.

Si jambo baya lakini kwa mujibu wa wanachama wa Azaki, jambo hilo linaweza kuzuia au kuwaogopesha wafadhili kushindwa kusaidia Azaki mbalimbali kutoka na pia na vifungu ambavyo vinaendelea kuminya uhuru nademokrasia ya asasi hizo.

Vifungu hivyo ni pamoja na kutaka pia kuelezea fedha hizo zinatumikaje na vinakuwa na malengo gani hata ikiwa kama kuna mikutano ya kuweza kuikosoa Serikali kwa kile ambacho inafanya sidhani kama itaweza kuidhinishwa kuingizwa kwa fedha hizo.

Lakini pia ukisoma vizuri marekebisho ya kanuni hizo kuna vipengele ambavyo vinapinga ukiukwaji wa haki ya faragha ya mashirika na kama haijafanyika hivyo Serikali ina mamlaka ya kuyaambia mashirika kuwa yamevunja kanuni.

Kutokana na vipengele hivyo ambavyo kwa namna moja ama nyingine vitaweza kuminya uhuru wa mashirika hayo, waliandaa mijadala mbalimbali iliyofanyika Dodoma, Arusha na Lindi na kuja na mapendekezo mbalimbali yatakayopelekwa kwa Waziri kuhusu mwonekano wa kanuni kwa ujumla, madhara yake kwa sekta ya NGOs na mapendekezo kwamapungufu yaliyoonyeshwa.

Hivyo basi pasipo kupuuza mapendekezo watakayopeleka serikalini ni vyema Serikali ikasikiliza kilio cha NGO na kuweza kukaa nao kama wadau wakaweza kupitia kanuni moja baada ya nyingine ikiwa ni ishara ya kuonyesha afya ya demokrasia katika Serikali yetu.

Mashirika haya yana umuhimu wake katika taifa katika kukosoa Serikali pale ambapo inakosea, katika kutetea haki za binadamu, kusisitiza amani na utawala bora hivyo ni vyema wakasikilizwa kama kuna vipengele ambavyo wanaona wafadhili wanaweza kujitoa kwa kutokuwapa fedha basi Serikali isisite kuviondoa au kama kuna vipengele ambavyo vinanyima uhuru wa faragha basi Serikali haitapendeza kuacha kuwasikiliza kwa maana ni haki yao pia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles