MOJA ya habari zilizokuwapo katika ukurasa wa nne wa gazeti hili katika toleo la jana ilizungumzia hatua ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Kampuni ya kimataifa ya kupakua na kupakia makasha Tanzania (TICTS) kusaini mkataba mpya baada ya majadiliano yaliyochukua miezi saba kufikia makubaliano.
Kwamba katika marekebisho hayo, mkataba huo mpya umesainiwa baada ya Rais Dk. John Magufuli kutembelea Bandari ya Dar es Salaam na kutoa maagizo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, kushughulikia upungufu wa TICTS ili waendelee na shughuli hizo.
Baada ya kusaini, Profesa Mbarawa alisema mkataba huo mpya umeondoa masharti hasi yaliyokuwa yanabana maslahi kwa Tanzania na kwa sasa TICTS watalipa kodi ya mwaka ya Dola milioni 14 za Marekani kutoka Dola milioni saba za Marekani za mkataba wa awali na itakuwa ikiongezeka kwa asilimia tatu kila mwaka.
Pia kodi ya makasha itakuwa Dola 20 za Marekani kutoka Dola 13 za Marekani katika mkataba wa awali na itakuwa ikiongezeka kila mwaka kwa asilimia nne na wamerekebisha kipengele cha utendaji wa kazi na sasa kila baada ya muda TICTS wanatakiwa kuonyesha utendaji wao, ikiwamo upakuaji na upakiaji wa makontena.
Pamoja na mambo mengine, sisi wa MTANZANIA Jumamosi tunaipongeza Serikali kwa kuufumua mkataba huo, kwa sababu kwa muda mrefu sasa ulipigiwa kelele kwamba ulikuwa wa kinyonyaji, huku utendaji wa TICTS nao ukituhumiwa kuhusika na upotevu wa mizigo ya wateja na makontena yakiwa yamefunguliwa na kuibiwa baadhi ya mizigo, pia ilicheleweshwa kupakuliwa na kupakiwa.
Licha ya kuipongeza Serikali kwa hatua hiyo, lakini pia tunaishauri isiishie kwa TICTS peke yake, bali ifumue baadhi ya mikataba mingine isiyo na tija kwa Taifa ambayo taasisi zake zinatajwa kuingia na kampuni za ndani au za nje ya nchi.
Kwa sababu kwa muda mrefu sasa imeendelea kuiumiza nchi na kwa kuwa  kutia saini mikataba hiyo si kwamba kila kitu kimekwisha, ndiyo maana tunaamini mikataba yote isiyokuwa na manufaa itapitiwa upya na vipengele au maeneo yote ya kinyonyaji yatatafutiwa mwarobaini ili nchi ifaidike.
Pia tunaamini alichosema Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, ni sahihi, kwamba mkataba wa TICTS uliofumuliwa ni miongoni mwa mikataba iliyosaidia kujua kuna umuhimu wa kupitiwa kwa mikataba mingi inayoonekana kutokuwa na manufaa.