27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali inataka vyombo vya habari viwe huru-Nape

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, amesema Serikali inakusudia vyombo vya habari vifanye kazi kwa uhuru nakwamba haitaviingilia kwenye uhuru wao.

Waziri Nape amebainisha hayo Februari 16, 2023 wakati wa ziara yake aliyoifanya katika ofisi za Mwananchi Communication, Tabata jijini Dar es Salaam.

“Serikali itasimamia na kulinda uhuru wa kujieleza. Itahakikisha inafanya kila linalowezekana kulinda haki hiyo,” amesema Nape.

Waziri Nape amesema, Marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari yaliowasilishwa bungeni Februari 10, 2023, yanalenga kuimarisha uhuru wa kujieleza nchini.

Pia amesema, serikali inataka kuwa mlezi wa uhuru wa kujieleza “serikali haitaki kuingilia biashara ya vyombo vya habari.

“Inachotaka ni kuwa mlezi wa uhuru wa kujieleza na tunataka wamiliki wa vyombo vya habari, waendeshe biashara zao kama ilivyo kwa tasnia nyingine kama wanasheria, madaktari na wengine,” amesema Nape.

Amesema, wakati ilipotungwa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya Mwaka 2016, kulikuwa na vilio vingi.

“Tusingeweza kuendelea na vilio hivyo, hivyo tumependekeza baadhi ya mabadiliko kwenye sheria hiyo,” amesema Nape.

Na kwamba, muswada huo ukipitishwa kwa taratibu za bunge na kutiwa saini na rais kuwa sheria kamili, utasaidia kuleta mageuzi makubwa kwenye tasnia ya habari nchini.

Amesema baada ya muswada kusomwa bungeni, sasa utakabidhiwa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ambapo itakuwa na jukumu la kuwaita tena wadau wa masuala ya habari kwa ajili ya kuwasikiliza, kisha kamati hiyo ya bunge itapeleka maoni ya wadau bungeni kabla ya Bunge kuanza kujadili maoni ya serikali kuhusu sheria hiyo.

“Tulifanya mazungumzo ya kutosha kwa mwaka mzima kati ya serikali na wadau juu ya maboresho ya ile sheria, na yale tuliyokubaliana, tumeyazingatia kama serikali kwenye mapendekezo yetu bungeni,” amesema Nape.

Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), Bakari Machumu, amesema mchakato kuelekea sheria hiyo, umekuwa wa majadiliano zaidi kati ya serikali na wadau waha habari.

“Kuna mapendekezo ambayo tuliyapeleka, yamesomwa. Kwa hiyo, tunachoangalia kwa sasa ni kwenda mbele kujua nini kimewekwa na kitajadiliwa kwa njia ipi,” amesema Machumu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles