MIONGONI mwa habari zilizokuwapo toleo la jana la gazeti hili katika ukurasa wa pili, ilisema watumishi wa umma 450 wamerudishwa kazini baada ya kushinda rufaa zao.
Taarifa ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Laurean Ndumbaro, ilisema watumishi hao wameshinda rufaa zao baada ya kuondolewa kwa madai ya kutumia vyeti feki na wataandikiwa barua za kurudishwa kazini.
Kwa mujibu wa Dk. Ndumbaro, wengi walioshinda rufaa hizo walikuwa wanawake walioolewa na kubadili majina yao na kuanza kuyatumia ya waume zao.
Pia Dk. Ndumbaro alisema Serikali imesitisha mishahara kwa watumishi wa umma waliotakiwa kuwasilisha vyeti vyao kwa uhakiki, lakini hadi sasa hawakufanya hivyo.
Pamoja na mambo mengine, sisi wa MTANZANIA Jumamosi tunaona kwamba Serikali imetenda haki kuwarudisha watumishi hao waliokata rufaa kwa sababu licha ya mchakato wa kuwabaini waliotumia vyeti feki kuwa na nia njema, lakini ulikuwa na kasoro, ikiwamo kuwaorodhesha walio na vyeti visivyokamilika na wengine kuwekwa kimakosa, ambao katika ripoti ya kwanza walitajwa baada ya kuchelewa au kupuuza kuwasilisha nyaraka zao.
Pia tunaamini baada ya rufaa za watumishi hao kujibiwa na kurudishwa kazini, ripoti mpya ya watumishi wenye vyeti feki waliopo katika wizara mbalimbali na taasisi zake itatolewa kama ilivyoahidiwa, kwa sababu Dk. Ndumbaro alinukuliwa siku za nyuma akisema ilichelewa kwa kuwa Serikali haikutaka kasoro hizo zijirudie.
Wakati Dk. Ndumbaro na wenzake wizarani hapo wakiendelea na mchakato huo wa kumalizia ripoti mpya ya watumishi wenye vyeti feki baada ya ile ya awali iliyotolewa Aprili 28, mwaka huu na Waziri wa Utumishi, Angella Kairuki na kumkabidhi Rais Dk. John Magufuli majina 9,932 ya wenye vyeti feki, tunaamini Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, litawakamata wote wanaotumia vyeti feki na kuwachukulia hatua za kisheria, ikiwamo kupelekwa mahakamani badala ya kuwaomba kujisalimisha wao wenyewe.
Kwa sababu licha ya Necta kuwa ndiyo yenye dhamana ya kutoa vyeti vyote vya watahiniwa wanaomaliza mitihani ya Taifa nchini, lakini inachelewa kuwakamata wanaotumia vyeti feki na kusababisha tatizo hilo kuongezeka na kuwasumbua kwa kipindi kirefu sasa.
Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde, kuongezeka kwa tatizo hilo kuliwalazimu mwaka 2008 kubadili utaratibu na mfumo wa utoaji wa vyeti vya kumaliza elimu ya sekondari.
Kwamba tangu wakati huo, utaratibu waliouweka ni lazima vyeti hivyo viwekwe picha ya mtahiniwa na kwa jinsi mfumo wao ulivyo, ni lazima mtu yeyote anayemiliki cheti feki watambaini.
Hata hivyo, sisi tunaamini Necta wamechelewa hilo, licha ya wao wenyewe kusema wamefanya jitihada mbalimbali kuvidhibiti vyeti hivyo kwa kuweka mfumo mpya na utaratibu mpya.
Kwa sababu tunaamini kwamba, hadi sasa hivi kuna idadi ya baadhi ya watu wanamiliki vyeti feki na wanavitumia kuombea nafasi mbalimbali za kazi katika ofisi za Serikali, kampuni binafsi au kuombea nafasi za kujiunga na vyuo vikuu.
Pia tunaishauri iangalie chanzo na ukubwa wa tatizo lenyewe kwa sababu pengine watu wengine wamepewa vyeti hivyo na baadhi ya watumishi wa Necta wasio waaminifu na waadilifu wa kazi zao.
Pia tunaaamini kuwa, tatizo hilo ni kubwa kwa sababu pengine ndilo linalosababisha baadhi ya watumishi wasio na sifa za kufanya kazi fulani fulani katika ofisi binafsi au serikalini kutokana na kughushi vyeti vyao vya kitaaluma, huku wenye sifa za kufanya hivyo wakikosa kazi na kuendelea kusota mitaani.
Kama hivyo ndivyo, pia tunawaomba waajiri wote kwa maana Serikali, sekta binafsi, wakuu wa vyuo na wale wa shule za sekondari na wananchi kwa ujumla wao kutoa ushirikiano katika kupambana kudhibiti vyeti vya shule na vyuo na nyaraka nyingine bandia, licha ya ukweli kwamba si kila mtu ana utaalamu wa kuvitambua, kwa sababu wanaovighushi wamekuwa makini na wajanja.