25.4 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali imeanza vema mabadiliko sheria ya habari-ACT

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Ado Shaibu amesema Serikali imeanza na mguu mzuri kuelekea Mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016.

Kiongozi huyo, ametoa kauli hiyo Februari 14, 2023, ikiwa ni siku tano kupita baada ya serikali kuwasilisha mapendekezo ya marekebisho vipengele vya sheria hiyo bungeni kwa ajili ya kufanyia marekebisho.

Amesema, hatua ya serikali kuwasilisha mapendekezo hayo yaliyobeba sehemu ya mabadiliko ya sheria hiyo, inaakisi kuelekea katika uhuru wa kweli wa habari nchini.

“Nimepitia muswada huo kwa haraka, kwa namna yake umegusa baadhi ya mambo ambayo wanahabari walikuwa wanalalamikia na kweli yalikuwa yana ukakasi mkubwa ikiwa ni pamoja.

“Miongoni ni lile la Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) kupunguziwa mamlaka ya kuhukumu vyombo vya habari, hapa unaona wazi dhamira ya kufanya vyombo vya habari kuwa huru inaonekana. Pia nimeona marekebisho kuhusu kupunguzwa kwa faini,” amesema Ado.

Hata hivyo, ameshauri wadau wa habari kupitia muswada huo kwa makini, ili kujiridhisha kwa namna ambayo vyombo vya habari vitakuwa imara ziadi ya ilivyo sasa.

“Pamoja na kwamba muswada umesomwa kwa mara ya kwanza, bado wadau wa habari wanapaswa kuupitia kwa makini zaidi kipingele kwa kipengele ili kujiridhisha.

“Jambo hili likipita, itachukua muda mrefu kufanya marekebisho mengine. Hii ni fursa ambayo serikali imewapa na wanapaswa kuitumia vizuri,” amesema Ado.

Pia ameshauru wadau wa habari kukutana na wabunge kwa nyakati tofauti kwa ajili ya kufafanua zaidi kile wanachokihitaji kwa kuwa, ndio watunga sheria.

“Nashauru wadau wa habari wajitahidi kuwaeleza wabunge dhamira halisi na nini thamani ya kuwa na vyombo vya habari huru.

“Nasema hivyo kwa kuwa, wabunge ndio watunga sheria, wanapokuwa na ufahamu mkubwa kuhusu mabadiliko haya, wanaweza kusaidia kwa kiwango kikubwa kutunga sheria zitazolea uhuru wa habari kwa muda mrefu,” amesema.

Akizungumzia mchakato huo, Ado amesema serikali yoyote dunia haiwezi kutamba kuwa, inaenzi demokrasia huku ikiminya Uhuru wa Vyombo vya Habari.

“Haiwezekani kuwa na demokrasia kama hakuna uhuru wa habari. Hivi vitu viwili vinategemeana, mahala ambapo demokrasia inastawi, tunatarajia uhuru wa habari nao utakuwa umeshamiri na sehemu ambayo uhuru wa habari umeshamiri, demokrasia nayo inashamiri.

“Uhuru wa Vyombo vya Habari na maendeleo ya taifa ni chanda na pete. Nchi ikiendeshwa gizani, nchi ikiendeshwa bila uwazi, nchi ikikosa uhuru wa habari, nchi hiyo haiwezi kuwa na maendeleo ya kweli,” amesema.

Ado amesema, jambo ambalo baadhi ya watawala hasa wa Afrika hawalielewi, wanadhani kuwa habari ni adui kwao na ni adui kwa serikali.

“Utaona katika nchi nyingi za Afrika jitihada zimekuwa zikifanywa na serikali kuzuia uhuru wa habari, serikali zimekuwa zikiweka sheria kuhakikisha vyombo vya habari vimekuwa havifurukuti.

“Ukweli ni kwamba uhuru wa habari unasaidia sana serikali kutekeleza wajibu wake, unalisaidia sana taifa kusonga mbele,” amesema Ado.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile.

Deodatus Balile, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) amesema, tayari muswada huo ameupitia na kwamba, yeye na wadau wengine wa habari wanapanga kukutana ili kuuchambua kwa pamoja ili kuwa na kauli moja.

“Sisi kama wadau wa habari, tupo wengi na si TEF peke yake, tunashauriana kufanya kikao cha pamoja kama tulivyoanza mwanzo, basi tuwe na kauli moja inayotuunganisha,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles