NA SHERMARX NGAHEMERA
NI ukweli kuwa binadamu huwa hawataki kupata vya bure au vilivyo rahisi na kutokana na ukweli huo, huwa hawathamini vile vya hali hiyo na hivyo kufanya maisha yao kuwa ya gharama kubwa bila sababu ya msingi.
Katika uvuvi, unahitaji chombo cha kusafiria hadi bahari kuu na hapo unashusha nyavu zako kwa mtindo wa kokoro na kuvua kwa kuzivuta na kupata bila kukosa samaki wengi na wa kila namna, wakubwa kwa wadogo.
Lakini wahenga wanasema palipo na samaki hakuna wavuvi, kwani wengi hawathamini shughuli hiyo ambayo wanaoshiriki wanapata faida kubwa na kuendelea.
Nchi za Japan, Norway na Iceland zina uhakika wa maisha kutokana na uvuvi endelevu.
Tanzania ina ukanda unaopakana na bahari takribani urefu wa kilomita 1,451 na kuna ushahidi tosha kuwa ukanda huu una utajiri mkubwa wa samaki wa kila aina, ambao kama tungekuwa wajasiri na kufanya ujasiriamali wa uvuvi, ingekuwa nchi ya utajiri mkubwa.
Kama ilivyo nchi ya rasilimali nyingi, tumelala usingizi wa pono, hatujali rasilimali hiyo kwa hata kukodisha tu, ila tumejaa kulalamika kuwa sisi ni masikini na hivyo tusaidiwe. Tumeaminishwa na tumekubali upotofu huo.
Ukiachia hayo, tunazo kilomita 400 za kuingia baharaini kama eneo letu la kiuchumi na hapo tunapakana na Seychelles kutokana na kazi kubwa aliyofanya Profesa Anna Tibaijuka wakati akiwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi na kuomba Umoja wa Mataifa watambue hilo, nayo ikaridhia na hivyo kufanya uhakika wa maisha yetu duniani kama nchi kuwa imara na kuonewa wivu na wengi.
Isitoshe kwenye bahari kuna rasilimali nyingi za madini ukiachia mafuta na gesi asilia na hivyo kwa teknolojia ya kileo, yanaweza kuvunwa na kutajirisha nchi. Kama hatuna teknolojia, hata kukodisha tunashindwa?
Ninapata furaha kusikia Serikali ya awamu hii imeliona hilo na kupanga mikakati ya kulifufua shirika letu adhimu la samaki lililokuwa linaitwa Tanzania Fishing Company (TAFICO).
Inasemekana wizara imekamilisha Waraka wa Baraza la Mawaziri kwa mapendekezo ya kutunga Sheria Mpya ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO).
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Uvuvi, William ole Nasha, wakati akijibu swali la Mbunge wa Morogoro Kusini, Prosper Mbena wa CCM. Vizuri sana na hongera kwa Serikali kwa kuliona hilo.
Shirika hilo liongezewe majukumu ikiwa pamoja na kutoa leseni ili wizara iwe kwenye sera na udhibiti na hivyo kuwa kali zaidi pale TAFICO inapokosea.
Mbena alihoji Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kufufua TAFICO.
Waziri Nasha alisema Serikali inaona umuhimu wa kufufua TAFICO ili sekta ya uvuvi iweze kuchangia ipasavyo katika ajenda ya uchumi wa viwanda.
“Suala hilo linafanyika kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu ili kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali za uvuvi zilizopo, ikiwa ni pamoja na uvuvi wa bahari kuu,” alisema.
Ninasema hilo lisibakie hapo bali liendelezwe zaidi.