30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI IKUNE KICHWA TIMU YA KUPAMBANA NA BARRICK

Na EVANS MAGEGE,

KAMPUNI ya Barrick Gold Corporation kupitia mshirika wake Acacia, imeonekana kutaka kupeleleza ili kuwafahamu watu ambao watateuliwa na Rais Dk. John Magufuli kuunda timu ya kuiwakilisha Tanzania kwenye mazungumzo ya kutatua mgogoro wa mchanga wenye madini (makinikia).

Mazingira ya kuwapo kwa mpango huo si tu yanatafsirika, bali yanajidhihirisha  kupitia kauli aliyoitoa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Acacia, Brad Gordon wakati wa mkutano wa wanahisa uliofanyika kwa simu Alhamisi ya wiki hii.

Akijibu swali la mwanahisa aliyetaka kujua Acacia imejipangaje kuelekea kwenye mazungumzo na Serikali, Gordon alisema kampuni hiyo imejipanga sawasawa kuanzia kwenye kuunda timu ambayo itakuja kufanya mazungumzo hapa nchini.

Mbali na kuunda timu, Gordon pia aliwapa picha ya timu ya Tanzania ambayo itakutana na Barrick kwenye mazungumzo.

Gordon ambaye alikuwa akijibu swali la mwanahisa aliyetaka kujua kama tayari wamekwishaifahamu timu ya Tanzania itakayoshiriki kwenye mazungumzo hayo, alisema anaamini itaongozwa na Rais Magufuli.

Zaidi alisema wengine ambao anahisi watashiriki katika mazungumzo hayo ni pamoja na maofisa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Mbali na hilo la timu, hatua ya wanahisa kutaka kufahamu pia namna ya mazungumzo hayo yatakavyofanyika, imetoa taswira ya kuangalia namna ya kujipanga pindi yatakapoanza.

Ingawa haijawekwa wazi idadi ya watu watakaounda timu kwa kila upande, lakini udadisi mfupi uliofanywa na MTANZANIA Jumapili umebaini kuwa lengo la Acacia kutaka kufahamu mapema timu ya itakayoiwakilisha nchi, ni kujua nguvu na udhaifu wa si tu mjumbe mmoja mmoja bali timu nzima.

Kutokana na uzoefu wa changamoto ambazo imewahi kukumbana nazo kwenye uwekezaji wake katika nchi kama za Dominica, Argentina, Pakistani, Australia, Canada, Chile, Papua New Guinea, Peru, Saudi Arabia na Zambia, kampuni hiyo imekuwa na utamaduni wa kujizatiti kwa kutumia watu wenye utaalamu, ujuzi mkubwa wa kujenga hoja za kujilinda na wenye uzoefu wa miaka mingi.

Wabobezi wa masuala ya diplomasia wanasema historia inaonyesha kwamba mara nyingi Barrick wanapokumbwa na changamoto kwenye uwekezaji wake katika mataifa mbalimbali, imekuwa ikipendelea kutumia mbinu ya mazungumzo ili kupata suluhu.

Inaelezwa wanapokuwa ndani ya mazungumzo, hutumia mbinu inayojulikana kama ‘The Diplomatic-War Strategy’ (Mkakati wa Kujilinda Kidiplomasia) ambao una msingi wa falsafa ya makubaliano yenye manufaa (Negotiate While Advancing).

Kwa msingi huo, ukiachilia mbali mgawanyo wa majukumu ya bodi zinazounda Barrick Gold Corporation, mgawanyo wa menejimenti za aidha Barrick yenyewe au kampuni tanzu, zimesheheni wabobezi katika masuala ya siasa za kimataifa, washawishi wa mikataba na sheria, wabobezi katika masuala ya uchumi na watu waliofanikiwa kibiashara.

Kwa mujibu wa tovuti ya Barrick, bodi yake ya wakurugenzi inaundwa na vigogo 12 ambao ni wazoefu wa masuala ya kimataifa.

Pia ujumbe huo wa bodi unaundwa na watu ambao ni wazoefu wa mambo ya ushauri kuhusu menejimenti, jiografia, siasa na mambo mengine ya kimkakati yanayoathiri utendaji wa kampuni hiyo.

Bodi hiyo ya washauri inaundwa na mawaziri na mawaziri wakuu wastaafu kutoka nchi mbalimbali duniani na hasa mataifa makubwa.

Mwenyekiti wa bodi hiyo ni Brian Mulroney, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Canada (1984-1993) na wajumbe ni Jose Aznar, ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu wa Hispania (1996-2004) na Spika wa zamani wa Bunge la Marekani, Newt Gingrich (1995-1999).

Ikumbukwe kwamba Gingrich ndiye aliyesimamia hoja ya kutaka kumwondoa Rais Bill Clinton wa Marekani mwaka 1998 kufuatia kashfa ya kuwa na mahusianao ya kimapenzi na aliyekuwa mtumishi wa Ikulu ya nchi hiyo, Monica Lewinsky. Hata hivyo rais huyo alichomoka kwenye kashfa hiyo iliyolitikisa taifa hilo.

Wajumbe wengine ni John Baird ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Canada (2011-2015), Waziri wa Ulinzi wa zamani wa Marekani, William Cohen (1997-2001) na Karl-Theodor ambaye naye amewahi kuwa Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani (2009-2011).

Wengine ni Mwenyekiti Mtendaji wa Barrick, Profesa John Thornton ambaye alikuja nchini na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli Jumanne iliyopita.

Katika hatua nyingine, upekuzi wa taarifa uliofanywa na MTANZANIA Jumapili juu ya mwenendo wa mazungumzo ya kutataua changamoto zilizowahi kutokea baina ya Barrick na Serikali za nchi mbalimbali, umebaini kuwa mara nyingi kampuni hiyo ina utaratibu wa kuficha majina ya watu wanaounda timu zinazoiwakilisha katika usuluhishi wa migogoro.

Lakini pamoja na utamaduni huo, MTANZANIA Jumapili limenasa wasifu wa baadhi ya wajumbe wanaotajwa kuongoza timu za Barrick kwenye usuluhishi wa migogoro ya mikataba ya uchimbaji madini, ikiwamo katika mgodi wa Pueblo Viejo.

Mmoja wa watu anayetajwa kuiwakilisha Barrick katika mazungumzo hayo nchini Dominica, ni mbobezi katika masuala ya kibenki na fedha, ambaye ametumikia sekta hiyo kwa zaidi ya miaka 30 katika taasisi mbalimbali nchini humo na kimataifa.

Tovuti ya Dominican today imewahi kuwakariri maofisa wa juu wa Serikali ya nchi hiyo wakisema kuwa wakati wa mazungumzo ya kutafuta suluhu katika mgodi wa Pueblo Viejo, Serikali yao iliwakilishwa na wahandisi wa migodi, Wizara ya Nishati na Madini na Mamlaka ya Kukusanya Mapato.

Hata hivyo, mtandao huo ulishindwa kuwaweka wazi watu walioiwakilisha Barrick katika mazungumzo hayo.

Kwa misingi hiyo, Tanzania huenda sasa ikatakiwa kujipanga kwa kuunda timu ambayo itakuwa na watu wenye kariba kama wale wa Barrick.

Hata hivyo, duru za mambo kutoka kwenye mifumo ya Serikali, zimelidokeza MTANZANIA Jumapili kuwa Tanzania ina hazina kubwa ya watu ambao hawafahamiki sana, lakini ni wabobezi wazuri katika masuala ya diplomasia, uchumi, sheria na wengine.

Inaelezwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa zamani, Andrew Chenge na Profesa wa Miamba, Sospeter Mhongo ni watu ambao wangefaa kujumuishwa kwenye timu hiyo ya mazungumzo kutokana na utaalamu wao na uzoefu, lakini kwa sababu ya changamoto ya kutajwa katika sakata hili huenda wakawa wameikosa sifa hiyo.

Ingawa hakuna chombo chochote cha Serikali ambacho kimekwishaeleza juu ya timu ambayo itaundwa kushiriki katika mzungumzo hayo, zipo hisia kwamba miongoni mwa ambao watajumuishwa ni baadhi ya wajumbe walioshiriki katika uchunguzi wa kamati mbili zilizoundwa na Rais Magufuli.

Machi mwaka huu, Serikali ilizuia makontena zaidi ya 200 kwenye Bandari ya Dar es Salaam ili kuchunguza mchanga wa madini ambao ulikuwa unasafirishwa nje ya nchi kuchenjuliwa.

Mchanga huo ulikuwa ni mali ya Acacia, ambayo ni kampuni mshirika wa Barrick Gold Corporation.

Baada ya zuio la mchanga huo, Rais Magufuli aliteua kamati mbili kuchunguza mchanga huo, na kamati ya kwanza iliyokuwa inaundwa na wanasayansi, ilibaini kiasi kikubwa cha madini ambayo yangeibwa.

Kamati ya pili iliyoundwa na wachumi na wanasheria, ilibaini zaidi ya Sh trilioni 100 zimeibwa kupitia usafirishaji wa makinikia, huku sheria nyingi za madini zikikutwa na kasoro inayotoa upenyo wa wawekezaji kutorosha madini.

Baada ya ripoti ya pili kuwasilishwa, Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation ambaye ni mmiliki mkubwa wa Kampuni ya Acacia Mining Limited, wakiwa na hisa asilimia 64, Profesa John Thornton, alikuja nchini na kukutana na Rais Magufuli. Walifanya mazungumzo na kukubaliana kuunda timu mbili za majadiliano.

Timu hizo zitahusisha Serikali ya Tanzania na wawakilishi wa Kampuni ya Barrick kutoka Canada na Marekani na watafanya majadiliano ambayo yatahusu namna ya kufikia mwafaka katika suala la kusafirisha makinikia nje ya nchi kwa faida ya pande zote mbili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles