30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali ihakikishe mimba za ovyo shuleni zinakoma

pregnantELIMU na afya ni miongoni mwa huduma zenye umuhimu mkubwa na wa pekee kwa ustawi na maendeleo ya maisha ya mwanadamu.

Katika kutambua umuhimu wa huduma hizi, Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ilianzisha mipango mbalimbali katika maeneo haya nyeti na katika huduma za jamii.

Ni katika kipindi cha uongozi wake; maradhi, ujinga na umasikini vilitangazwa kuwa maadui wakubwa wa maendeleo ya Taifa letu.

Jitihada za kupambana na maadui hawa hazikuwa kwa maneno tu, bali ziliwekwa katika matendo zaidi. Mfano mzuri hapa ni kwamba katika sekta ya elimu, ulianzishwa mpango wa elimu kwa wote uliofahamika kama UPE (Universal Primary Education) kwa lengo la kuhakikisha kuwa watu wanapata elimu, hususan elimu ya msingi.

Mpango huu ulitoa fursa kwa watoto wote wa Kitanzania kupata elimu ya msingi inayofanana bila kujali hali za kiuchumi za wazazi wao.

Suala hili la usawa katika elimu liliwezekana kwa sababu shule zote zilimilikiwa na Serikali, hivyo kutoa elimu kama huduma.

Hivyo ndivyo hali ilivyokuwa wakati wa uongozi wa serikali ya awamu ya kwanza.

Lakini katikati mwa miaka ya 80 mambo yalianza kubadilika. Sera za uchangiaji gharama katika huduma za afya na elimu zilianzishwa ili kuendana na matakwa ya mabepari ambao walizitaka serikali zetu zifanye hivyo ili ziweze kupata misaada ya kifedha.

Hapa ndipo tulipoanza kushuhudia kuanzishwa kwa shule na taasisi nyingi za elimu zinazomilikiwa na watu au taasisi binafsi; na huduma zake muhimu kuanza kuuzwa kama bidhaa nyingine zinavyouzwa sokoni.

Tunasema hii ndiyo kasoro ambayo inamgharimu mlalahoi wa enzi hizi, kasoro ambayo Serikali ya awamu ya Tano haina budi kuiondoa kwa masilahi mapana ya Taifa.

Aidha, kuna uzembe katika kushughulikia wale wanaowapa mimba wanafunzi na kuwafanya wanafunzi hao wasiendelee na masomo.

Kwa mfano, toleo la jana la gazeti hili tuliripoti kuwa wanafunzi 238 wa shule za msingi na sekondari mkoani Kilimanjaro wamekatisha masomo baada ya kubainika kuwa ni wajauzito tangu Januari hadi Agosti, mwaka huu. Idadi hii ni ya mkoa mmoja tu kwa muda wa miezi minane tu!

Serikali mkoani humo imeliagiza jeshi la polisi kuacha kufanyakazi kwa mazoea na kuhakikisha linawakamata watuhumiwa wote waliohusika kuwapa ujauzito wanafunzi hao, na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki, wakati wa sherehe za kuwapongeza na kuwakabidhi zawadi maofisa 34 wa jeshi la polisi waliohitimu kozi za uongozi juzi mkoani humo.

Tunasema huu ni mkoa mmoja wa nchi. Hali ya Tanzania kwa ujumla itakuwa ni mbaya.

Tunasema Serikali haina budi kulisimamia hili ili mimba za ovyo kwa wanafunzi lifike mwisho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles