25.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI HAIFANYI LA MAANA UVUVI BAHARINI

coastal-east-africa-threats-07302012hi_114886

Na JOSEPH LINO,

UVUVI ni sekta muhimu kiuchumi nchini inayoweza kuleta mapinduzi katika sekta ya viwanda ili kufikia dira ya Serikali ya kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa kati ifikapo 2025.

Kuzidiwa na rasilimali za aina mbalimbali kunaifanya Tanzania kukosa mwelekeo wa matumizi sahihi ya rasilimali hizo na nyingine kutopewa kipaumbele na hivyo kumilikiwa na maharamia. Ndicho kilichotokea kwenye sekta ya uvuvi katika Bahari ya Hindi.

Bahari ya Hindi imetamalaki kwa kila aina ya samaki na wanyama, lakini Serikali haiijali rasilimali hiyo ambayo mtaji unaohitajika ni kidogo sana, lakini matokeo yake ni makubwa. Zao moja la samaki wa jodari (tuna) ni biashara ya dola bilioni 2 kwa mwaka, lakini hatupati chochote zaidi ya dola 600,000 kwa miaka mitatu ya huruma ya Umoja wa Ulaya (EU) kusimamia rasilimali hiyo. Tumelaaniwa na nini? Hatuoni utajiri huo ambao unahitaji kuleta wavu na meli na kuchota na kuondoka? Haihitaji pembejeo wala madawa. Tunageuza macho na kutazama upande mwingine. Mbaya zaidi tunatumia fedha zetu za kigeni kwenda kununua vibua kule Oman na Ghuba.

Tanzania  ukiacha vyanzo vingine vya mapato kama madini, kilimo na utalii, samaki wake wanaweza kuchangia kipato kikubwa kutokana na wingi, ubora,  ukubwa na wingi wa aina, ingeleta faida kubwa kwa wote wanaoshiriki na hasa ikijulikana kuwa kuna mahitaji ya ajira, mazalio ya samaki wengi ni Tanzania na ukanda wa pwani wa kilomita zaidi ya 1,414.

Kutokuwapo uwekezaji wa uvuvi KATIKA bahari yetu ni laana kubwa ambayo tumetupiwa na Mungu wakati yeye anatupenda sana. Jibu, kwa uzembe huo ni samaki wetu wengi kama rasilimali kuvuliwa kwa wizi na maharamia kutoka nje.

Salum Rehani, Mbunge wa Uzini Zanzibar (CCM), anafafanua kuwa sekta hii ambayo bado inahitaji kupewa kipaumbele wakati huu wa mchakato kuwa nchi ya uchumi wa kati unaotokana na viwanda, lazima izingatiwe vilivyo na Serikali ya Awamu ya Tano ili tuweze kufanikiwa katika azma yetu ya taifa.

Kwa maelezo yake, anasema nchi inafanya makosa makubwa kudharau uvuvi na kudai uwekezaji unaohitajika si mkubwa sana ila ni udumavu wa kufikiri na woga kusafiri na kutafuta riziki baharini. Huo uoga lazima uishe ili kuweza kufaidi rasilimali hiyo ambayo inasubiri kuchukuliwa.

“Kwa mfano kuwa meli moja inaweza kuvua kaa wakubwa aina ya lobster takribani tani 200 kwa kipindi cha miezi mitatu.

“Tani moja inauzwa dola za Marekani 25,000 au 30,000, kiwango ambacho meli iliyovua kwa miezi mitatu ina uwezo wa kuingiza dola milioni 45 au 52 kwa kipindi hicho. Hii ni pesa ya mara mbili au tatu ya fedha ambazo zinakusanywa pale bandarini,” anaelezea.

Anaendelea kusema kuwa, meli moja  inaweza kutengeneza ajira zaidi ya watu 10,000 hadi 30,000 kwa miezi matatu.

“Tunafuta ajira wakati zipo wazi wazi, tunatafuta viwanda wakati samaki wapo, tunahifadhi ya samaki ambayo haijavuliwa, Tanzania ina uwezo wa  kuvua samaki takribani tani 20,000 kwa meli, ambazo zinaweza kuchakatwa ndani ya mwaka moja.

“Kipato chake ni kikubwa, kinachotakiwa ni kubadilisha fikira zetu kwa kuangalia namna ya kuwekeza sekta ya samaki kiviwanda”.

Anasema Bahari ya Tanzania inakuwa na meli 200 kwa wakati mmoja ambazo  zinavua samaki, fikiria kiwango cha samaki wetu wanaotoroshwa kiwizi kwenda nje.

“Kwa mwaka tunapata Sh bilioni 3 au 4 kwa leseni tu. Je, hizo zina faida gani kuwaruhusu wavua samaki kwa fedha chache?” anasema Rehani.

Takwimu zinaonesha kuwa, samaki jodari (tuna) wa thamani zaidi ya dola bilioni mbili huvuliwa Bahari ya Tanzania na Msumbiji.

Rehani anaelezea kuwa, sekta ya kuwekeza kwenda viwanda ndio hili jibu, ambayo miundombinu ni rahisi kama majokofu, vifaa vya kuchakata.

“Fursa ipo wazi, tumerogwa wapi wakati hapa hakuna tahadhari, tunaweza kukodi meli kwa dola milioni 12 au 15 kwa miezi mitatu ambayo tunapata faida ya dola milioni 45 au zaid.”

Anaendelea kusema; “Tumeshindwa kukodi meli ya dola 200,000 kulinda na kuwakamata watu hawa, ulinzi hakuna ambapo tunalindiwa na watu wa kimaitafa bahari yetu.”

Anasema fursa iliyopo kwenye sekta hii inaweza ikaondoa matatizo yaliyopo kuanzia wafugaji, ajira na kuchangia uchumi wa nchi kutokana na uvuaji samaki kwenye bahari yetu. “Tanzania imebahatika kuwa na maeneo makubwa ya uvuvi ambayo yanaweza kuleta tija na mabaidliko,” anasema Rehani.

Rehani anaelezea kuwa, kuna samaki wengi kwenye bahari ya Tanzania na kinachosaidia ni mkondo wa bahari kutoka Msumbiji ambao umezunguka bahari ya Mediterranean kwenda Msumbiji na Bahari ya Pacific.

“Hali hii kwetu inaisaidia nchi yetu kwa sababu ya ubaridi, samaki wanakusanyika maeneo ya bahari yetu, na kwa sababu wenzetu wanatuona kuwa na chakula baharini kwa ajili ya samaki, chakula hicho kinakuja upande wetu kwahiyo tunakuwa na samaki wengi,” anasema Rehani.

Anafafanua kuwa, Tanzania inakusanya samaki wengi ambao hawavuliwi, hasa kipindi ambacho tumetoa ushauri Waziri kufunga kutoa leseni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles