29.8 C
Dar es Salaam
Monday, October 7, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali: Fastjet lipeni deni la bil 6.6/-

LEONARD MANG’OHA NA TUNU NASSOR -DAR ES SALAAM

SERIKALI imeitaka Kampuni ya Ndege ya Fastjet kulipa deni la Sh bilioni 6.6 inazodaiwa.

 Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari alisema kampuni hiyo inapaswa kulipa deni hilo ili hatua nyingine zifuate.

Alisema kampuni hiyo inadaiwa zaidi ya Sh bilioni 6.6 na wadau mbalimbali waliokuwa wakiwapa huduma, zikiwamo Sh bilioni 2.1 wanazodaiwa na TCAA na Sh bilioni 2.1 za Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA).

“Baada ya kutoa notisi, Fastjet imeanza kulipa madeni hasa tuliyokuwa tukiwadai ambapo imelipa zile Sh milioni 760 na Dola 54,000,” alisema Johari.

Alisema pamoja na kulipa deni hilo, bado wanadaiwa na TCAA Dola za Marekani 156,000, TAA Sh bilioni 2.1, Swissport Sh bilioni 2.1, Kampuni ya Airco ya Mwanza Sh bilioni 1.1 na Cardico Sh milioni 286.

Kutokana na hali hiyo, TCAA imesema itaendelea kuishikilia ndege ya Shirika la Fastjet hadi hapo itakapomaliza kulipa madeni inayodaiwa.

Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Fastjet kulalamika kunyimwa kibali cha kuingiza ndege nchini huku iliyokuwapo awali ikizuiwa kuruka kwa madai ya kupata hitilafu za mara kwa mara.

Alisisitiza kuwa wataendelea kuishikilia ndege ya kampuni hiyo hadi hapo Fastjet watakapomaliza kulipa madeni yote.

“Tunasema ndege haitaondoka kwa sababu imezaa madeni na hawa wagavi wanaofanya kazi na Fastjet ni Watanzania.

“Kwa mujibu wa sheria namba 10 (1) inasema kuwa tutafuta usajili wa ndege iwapo madeni yote yatalipwa,” alisema Johari.

Kuhusu madai ya TCAA kuinyima Fastjet kibali cha kuingiza ndege, Johari alisema wamepokea nyaraka hizo kwa njia ya barua pepe Desemba 24, mwaka huu saa tisa alasiri kipindi ambacho kilikuwa ni kuelekea sikukuu.

Aliongeza katika notisi waliyoitoa kwa kampuni hiyo, TCAA iliitaka kampuni hiyo kupeleka andiko litakalothibitisha uwezo wake wa kifedha wa kujiendesha baada ya mabadiliko kutokea.

“Wawe na meneja mwajibikaji (accountable manager) ambaye ni mtaalamu na mzoefu wa kusimamia shughuli za ndege hizo na pia wanatakiwa kuwa na ndege.

“Hata hivyo Desemba 24 tulipata maombi ya kutaka kuleta ndege mbili ambapo mojawapo ni ile tuliyoikataa ambayo tuliamua kuishusha kutokana na kuwa mbovu,” alisema.

 Alisema kwa sababu kipindi hicho kilikuwa cha sikukuu walishindwa kuyafanyia kazi, hivyo walitarajia kuanza kupitia maombi jana.

“Desemba 24, tulipokea barua kutoka kwa Mwenyekiti Mtendaji wa Fastjet, Lawrence Masha akimteua Lawrence Masha kuwa Meneja Mwendeshaji (Accountable Manager),” alisema.

Juzi Masha aliwaeleza waandishi wa habari jinsi Serikali ilivyomzuia kuingiza ndege nchini.

Masha alisema bado ana matumaini kwamba baada ya kumalizika kwa Sikukuu ya Krismasi huenda mambo yakawa sawa.

Alisema bado kwa sasa wana subira na imani na Serikali kuwa italiweka jambo hilo sawa ili kuruhusu biashara za kampuni hiyo ziweze kuendelea nchini.

“Nina matumaini baada ya kumalizika kwa Sikukuu ya Krismasi huenda mambo yakawa mazuri,” alisema.

Desemba 17, mwaka huu TCAA ilitoa notisi ya siku 28 ya nia ya kuifutia leseni Fastjet na kuitaka kujieleza kwanini isifutiwe leseni ya kuendesha biashara hiyo nchini.

Baadhi ya sababu zilizotajwa na TCAA ni pamoja na kutokuwa na ndege baada ya moja kati ya mbili zilizosajiliwa nchini kuharibika na kupelekwa nje ya nchi kwa matengenezo, huku moja ikizuiwa na mamlaka hiyo.

Ndege hiyo ilizuiwa baada ya kampuni iliyowakodishia Fastjet kuitaka irudishwe kwa kile walichodai inafanya kazi bila wao kupata chochote.

Johari alisema kutokana na uamuzi huo wa mkodishaji kutaka arejeshewe ndege yake, alilazimika kuizuia kama ambavyo sheria ya usafiri wa anga inavyoelekeza.

Alisema ndege ambayo imesajiliwa nchini kwa sasa wameizuia hadi hapo madeni ya kampuni hiyo yatakapolipwa.

Johari alisema baada ya kampuni hiyo kukosa ndege ililazimika kuazima ndege nyingine moja kutoka Afrika Kusini ili iendelee kutoa huduma nchini.

Hata hivyo, alisema ndege hiyo pia ilizuiwa na mamlaka hiyo tangu juzi baada ya kubainika kuwa ni mbovu.

Nyingine ni kampuni hiyo kutokuwa na Meneja Uwajibikaji ambaye ni lazima awe mtaalamu wa masuala ya kiufundi ya ndege, kushindwa kuwasilisha andiko linaloonesha kubadilishwa umiliki kutoka kwa mmiliki wa awali ambayo ni kampuni kutoka nchini Uingereza kwenda kwa wafanyabiashara wazawa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles