Serikali, Barrick wamefungua ukurasa mpya

0
1272

Mwandishi Wetu

HATIMAYE uamuzi wa Rais Dk. John Magufuli wa kuzuia kuuzwa kwa makinikia kwa Kampuni ya Barrick miaka michache iliyopita umezaa matunda.

Tunakumbuka wakati Rais Magufuli anaagiza kusitishwa mauzo ya makinikia hayo, kuliibuka maneno mengi kutoka ndani na nje ya nchi kuhusu hatima ya kampuni hiyo kubwa na maarufu duniani inayojishughulisha na uchimbaji wa dhahabu.

Baadhi ya watu walihoji kama uamuzi huo wa Serikali ulikuwa sahihi au laa na wengine kufikia kusema kuwa Serikali haitapa kitu chochote kutoka kwa kampuni hiyo.

Lakini hayo yote baada ya vikao vizito kati ya Serikali na wawekezaji, mambo yamebadilika na Serikali imeweza kupata fungu ambalo miaka yote halikuwapo.

Haya ni matunda mazuri yaliyotokana na msimamo wa Rais Magufuli kuhusu umuhimu wa rasilimali za nchi kuwanufaisha wazawa, badala  ya kuwaachia mashimo au kulipwa mrabaha mdogo wakati mabilioni yakiondoka nchini kila siku.

Juzi mjini Dodoma, Serikali ilipokea hundi ya Dola za Marekani milioni 100  ambazo ni sawa na Sh bilioni 250 kutoka Kampuni ya Barrick.

Fedha hizi ni sehemu ya malipo ya awali ya Dola milioni 300  sawa na Sh bilioni 750 zinazotarajiwa kulipwa kwa Serikali na kampuni hiyo.

Mwenyekiti wa timu ya Serikali ya majadiliano na Barrick ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, anasema  tukio hilo ni  mwanzo wa makubaliano ya mkataba wa msingi kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni hiyo yaliyofikiwa Desemba 19, mwaka jana na kusainiwa rasmi Januari 24, mwaka huu.

Anasema pande husika zimekubaliana mpango wa malipo wa bakaa ya kiasi cha Dola za Marekani milioni 200, na anatumaini pande zote mbili zinazohusika katika makubaliano, yaani kampuni za madini kwa upande mmoja na Serikali kwa upande mwingine zitaheshimu makubaliano na kuhakikisha yanatekekelezwa.

Kabudi anasema Serikali ya Tanzania imedhamiria kwa dhati kutekeleza makubaliano hayo, ndiyo maana hivi karibuni iliruhusu makontena na makinikia ya madini 277 kusafirishwa.

Tunaamini Barrick ni mdau muhimu katika sekta hii, sasa itakuwa imefungua milango na kufanya shughuli zake kwa mujibu wa makubaliano yaliyopo na kuaondoa kasoro zote.

Tunatambua  usu maeneo muhimu kwenye makubaliano baina ya kampuni ya Barrick na Serikali, ni pamoja na kampuni hiyo kukukubali kutoa Dola milioni 5 za Marekani (Sh milioni 115.7) kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa mtambo wa kuchaka madini nchini (smelter) na kuanzisha ushirikiano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kutoa hadi Dola milioni 10 (Sh zaidi ya Sh bilioni 23.135) kwa kipindi cha miaka 10 kwa utoaji mafunzo yanayohusu sekta ya madini.

Masuala muhimu yaliyokubalika na kila upande ni kuunda Shirika la Madini la Twiga lenye umiliki wa pamoja  litakalofanya kazi nchini kwa  kusimamia uendeshaji wa migodi ya Bulyanhulu, Buzwagi, North Mara na mingine.

Sisi MTANZANIA, tunaipongeza Serikali  na Barrick kwa kufikia uamuzi huu ambao umefungua milango karika sekta hii.

Tunaamini kuanzia sasa, kila upande utatekeleza kwa asilimia mia moja makubaliano haya.

Tunampongeza Rais Dk. Magufuli kwa uamuzi wake mgumu aliochukua bila kuogopa maneno mengi yaliyokuwa yanasemwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here