32.2 C
Dar es Salaam
Thursday, February 2, 2023

Contact us: [email protected]

  Serengeti Boys yanusa fainali Afrika

serengeti Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

TIMU ya soka ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, jana iliutumia vyema uwanja wake nyumbani baada ya kutoa kipigo cha mabao 3-2 dhidi ya Congo Brazzaville katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Matokeo hayo yameiweka Serengeti Boys katika wakati mgumu kutokana na kuruhusu kufungwa mabao mawili nyumbani kwenye michuano hiyo ya kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Vijana, zitakazofanyika mwakani nchini Madagascar.

Kikosi hicho kinachonolewa na kocha, Bakari Shime, kitahitaji matokeo ya sare au ushindi katika mchezo wa marudiano utakaochezwa ugenini ili kufuzu fainali hizo.

Katika mchezo wa jana, Serengeti Boys walicheza kwa kujiamini zaidi kipindi cha kwanza na kupata nafasi nyingi za wazi lakini washambuliaji wake hawakuwa makini kufunga.

Hata hivyo, dakika ya 39 Yohana Mkomola aliifungia Serengeti bao la kuongoza baada ya kupiga shuti kali la umbali wa mita 30 na mpira kutinga wavuni.

Dakika ya 42 kabla ya mapumziko, Mkomola aliongeza bao la pili baada ya kupiga shuti akiwa ndani ya eneo la hatari akiunganisha pasi safi ya Asad Ally.

Timu zote zilifanya mabadiliko kipindi cha pili, lakini yaliinufaisha zaidi Congo Brazzaville ambao walipata bao la kwanza dakika ya 74 kwa mkwaju wa penalti iliyopigwa na Langalesse Percy.

Mwamuzi Nelson Emile Fred kutoka nchini Shelisheli, aliamuru penalti hiyo ipigwe baada ya Israel Patrick wa Serengeti kumfanyia madhambi Mboungou Prestige wa Congo.

Bao hilo liliwafanya Serengeti kuzidisha mashambulizi langoni kwa Congo na kufanikiwa kufunga bao la tatu dakika ya 82 kupitia kwa Issa Makamba aliyeungaisha mpira wa kona iliyochongwa na Asad Juma.

Congo nao walikuja juu na kufanikiwa kupata bao la pili dakika za nyongeza lililofungwa na Bopoumela Chardon, aliyewapiga chenga mabeki wa Serengeti na kuujaza mpira wa wavuni.

Kikosi cha Serengeti kilifanikiwa kutinga raundi ya pili ya michuano hiyo baada ya kuiondosha Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 3-1, ikiwa ni matokeo ya sare 1-1 ugenini na ushindi wa 2-0 nyumbani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles