29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 20, 2021

SERENGETI BOYS TAYARI KWA MAPAMBANO GABON

Na ZAINAB IDDY, DAR ES SALAAM

MWISHONI mwa wiki ijayo timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, inatarajiwa kuanza kutupa karata yake ya kuipeperusha bendera ya Tanzania katika michuano ya Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17, ambayo imepangwa kufanyika nchini Gabon.

Timu hiyo iliyokuwa chini ya kocha mzawa Bakari Shime itafungua dimba na Mali Mei 15 katika mji wa Libreville Gabon .

Kabla ya kwenda Gabon katika mashindano hayo, Serengeti ilikwenda kuweka kambi nchini Morocco, ambapo ilicheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Gabon, ambao ni wenyeji wa michuano hiyo ya vijana  waliyoibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kuendeleza wimbi la ushindi katika michezo yake ya kirafiki kuelekea Kombe la Afrika kwa vijana.

Mbali na kambi hiyo, Serengeti ilikwenda kujichimbia nchini  Cameroon  kwa muda wa wiki mbili, nakupata nafasi ya kujipima dhidi ya  wenyeji wao Cameroon mchezo wa kwanza wakishinda 1-0, huku wa marudiano kwa mara ya kwanza wakipoteza kwa kufungwa 1-0.

Michezo mingine ya kirafiki ni ile waliyokuwa nyumbani (Tanzania) ni ule dhidi ya Burundi mara mbili, ambapo mechi zote zilipigwa Uwanja wa Kaitaba, Bukoba mkoani Kagera. Katika mechi ya kwanza, Serengeti Boys ilishinda 3-0, kabla ya kushinda mchezo wa pili 2-0.

Mtihani mkubwa kwa Serengeti Boys ulikuwa mchezo dhidi ya Ghana, maarufu kama Black Starlets, uliochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam. Ghana ni moja ya timu ambazo zimefuzu kwenye Kombe la Afrika kwa vijana. Katika mchezo huo, Ghana walitangulia kupata mabao mawili, lakini Serengeti  Boys, pasipo kukata tamaa, walirudisha mabao yote mawili dakika za mwisho.

Serengeti wamefikaje Gabon?

Safari ya kwenda Gabon haikuwa fupi, ilianza mwaka 2014, mara tu baada ya mashindano ya Copa Coca Cola, ambayo kwa kipindi hicho yalihusisha vijana wenye umri chini ya miaka 15. Ingawa pia ilionekana kuwa safari ndefu iliyohitaji umakini na mikakati mikubwa na zaidi ilihitaji wachezaji kujituma kwa nia ya kulipigania taifa lao.

Chini ya kocha Bakari Shime ‘Mchawi Mweusi’, Serengeti ilianza safari ya kwenda Gabon pale ilipoibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Shelisheli katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Mchezo wa marudio ulishuhudiwa Serengeti wakiibuka na ushindi wa mabao 6-0 na hivyo kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 9-0, baadaye walitoka sare ya kufungana bao 1-1 na Afrika Kusini ugenini, kabla ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0  kwenye Uwanja wa Taifa.

Kuwatoa Afrika Kusini kuliiwezesha Serengeti kuingia raundi ya pili ya michuano hiyo kwa kukutana na Congo Brazzaville, ambapo walipata ushindi wa mabao 3-2 kwenye Uwanja wa Taifa , wakati mechi ya marudiano iliyochezwa nchini Congo, ndipo wenyeji waliposhinda bao 1-0 na kuyafanya matokeo ya jumla kuwa mabao 3-3, huku Congo wakisonga mbele kwa bao la ugenini, kabla ya TFF kuibuka na hoja ya kijeba aliyedanganya umri.

Serengeti Boys ilijikuta ikirejeshwa kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17, ikiwa ni baada ya kushinda rufaa yake dhidi ya Congo Brazzaville iliyomtumia mchezaji aliyezidi umri.

‘Kijeba’ Langa Lesse Bercy aliyedaiwa kucheza Ligi ya Congo,  ndiye aliyefunga bao pekee lililoivusha timu yake ambayo katika mchezo wa kwanza ilishindwa mabao 3-2, kabla ya kuja kuiondoa kwa jumla ya mabao 3-3, huku wakipita kwa bao la ugenini.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liliwasilisha malalamiko kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ya kuchezeshwa Langa, ndipo CAF walipokitaka Chama cha Soka Congo, (FECOFOOT) kimpeleke mchezaji huyo Misri (makao makuu ya CAF) kufanyiwa vipimo vya MRI ili kuthibitisha umri wake.

Hata hivyo, Congo walishindwa kufanya hivyo mara tatu na kuipa nafasi Tanzania kusonga mbele, huku ikipangwa kundi B pamoja na timu za Angola, Mali na Niger, wakati kundi A likiwa na timu za Gabon,Guinea na Cameroon.

Katika mashindano hayo washindi wawili wa kila kundi wataliwakilisha Bara la Afrika katika fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika India, Oktoba mwaka huu, wakati awali ilipangwa kuchezwa nchini Madagascar, lakini Taifa hilo halikuwa tayari kwa miundombinu hivyo kunyang’anywa uenyeji.

Serengeti Boys ina kila sababu ya kuwatoa Watanzania kimasomaso, kutokana na maandalizi waliyopata na hususan mechi za kirafiki walizocheza. Wachezaji wameonyesha kujiamini uwanjani na utayari wa kukabiliana na timu yoyote.

Kikosi cha Serengeti Boys

Makipa:

1.   Kelvin Deogratius Kayego,

2.   Ramadhani Awm Kambwili

3.   Samwel Edward Brazio.

 

Mebeki wa Pembeni:

4.Kibwana Ally Shomari,

5.Israel Patrick Mwenda,

6.Nickson Clement Kibabage.

 

Mabeki wa Kati:

7.Dickson Nickson Job

8.Ally Hussein Msengi na

9. Issa Abdi Makamba

 

Viungo wa Kuzuia:

10. Kelvin Nashon Naftal

11. Ally Hamis Ng’anzi na

12. Shaban Zuberi Ada

 

Mawinga:

13.Syprian Benedictor Mtesigwa na

14.Said  Mussa Bakary

15.Abdul Hamis Suleiman

 

Viungo wa kushambulia:

16 Asad Ali Juma

17. Mohammed Abdallah Rashid na

18. Muhsin Malima Makame

19. Mathias Juan

 

Washambuliaji:

20.Ibrahim Abdallah Ali

21.Enrick Vitaris Nkosi

22.Rashid Mohammed Chambo

23.Yohana Oscar Mkomola

 

Benchi la ufundi

Kocha mkuu: Bakari Shime

Kocha msaidizi: Oscar Mirambo

Kocha wa makipa: Muhalami Sultan

Daktari: Sheky Mgazija

Dokta wa viungo: Gomez Dardenne

Mtunza vifaa: Edward Venance

Mshauri wa benchi la Ufundi:Kim Poulsen

 

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,594FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles