30.8 C
Dar es Salaam
Saturday, January 28, 2023

Contact us: [email protected]

SERENGETI BOYS MSILEWE SIFA MNA SAFARI NDEFU                     

Na MARTIN MAZUGWA


ILIKUWA ni ndoto ya kila Mtanzania kuiona timu hii ya vijana ikifika mbali hasa ukizingatia ilifanyiwa maandalizi ya nguvu kuanzia kambi ambayo ilionyesha kuwa kuna kitu cha ziada kwa vijana hao ambao wamekusanywa kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania.

Licha ya kuwa katika kiwango bora hivi sasa na kusifiwa kwa kazi waliyoifanya, isiwe sababu ya wao kulewa sifa na kujiamini kupita kiasi kuwa kitendo cha kwenda Gabon, kisiwafanye wabweteke na kujiona wamemaliza kila kitu wakumbuke kuwa wana safari ndefu katika mashindano hayo ambayo yametoa nyota wengi wanaokipiga barani Ulaya pamoja na Afrika,  kama Andre Ayew, John Boye pamoja na mlinda na mlango wa Simba, Daniel Agyei.

Safari hii ngumu iliyokuwa ya machozi na damu, ilihitaji moyo wa chuma na maombi kwa kila mpenda soka na asiyependa mpira wa miguu kuwaombea vijana hawa waweze kufanikiwa katika jambo ambalo walilipanga hatimaye dua zilifika na timu imepata nafasi ya kushiriki fainali za mataifa ya Afrika kwa vijana kwa mara ya kwanza.

Vijana hawa wamekuwa wakipewa sifa kwa kitendo cha kuzifunga timu bora za vijana kama bingwa mtetezi Afrika Kusini ‘Amajimbos’ kwa mabao  3-1, ikianza kupata ushindi wa mabao 2-0 nyumbani kabla ya kwenda kutoa sare ugenini ya bao 1-1 na kuwaondoa mashindanoni vijana hao wa rais Jacob Zuma.

Uwezo huo unadhihirisha kuwa vijana wana uwezo mkubwa kinachotakiwa kufanywa hivi sasa ni kuandaliwa vyema kisaikolojia, ili wasilewe sifa na kushindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa na wao pamoja na Watanzania kwa ujumla.

Mbali na kufanya vizuri huko katika michezo ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana, lakini pia kikosi hiki kilipata mwaliko kutoka Chama cha Soka nchini India na kilionyesha uwezo mkubwa na kufanya vizuri katika mashindano hayo kwa kupata sare ya bao 1-1 na Marekani, lakini ikapata sare ya mabao 2-2 dhidi ya Korea, kabla ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya India ambao walikuwa wenyeji.

Licha ya kufanya vizuri vijana hawa walikutana na milima na mabonde, ikiwamo kukutana na dhahama kucheza na watu waliowazidi umri kama vile Langa Bercy raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambaye mara baada ya kugundulika ana umri mkubwa na nchi yake ilishindwa kumpeleka akafanyiwe vipimo vya mifupa (MRI) ili kubaini umri wake halisi.

Ni muda mwafaka wa vijana hawa kuidhihirishia dunia kuwa Tanzania ina vipaji murua vya mchezo wa soka, pia yoso  hawa wanapaswa kujituma na kutumia mashindano haya kama daraja la kutimiza ndoto zao za kwenda kucheza soka nje ya bara la Afrika, ili kutanua wigo wa soka la Tanzania.

Kikosi hiki cha kocha Oscar Milambo, kilichobaki ni kuwekwa chini na kujengwa kisaikolojia kwani tayari vijana wana morali ya hali ya juu kuelekea katika fainali hizo, wakosolewe wanapokosea na wasipakwe mafuta kwa mgongo wa chupa kama kweli tunataka wafike mbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles