22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 18, 2021

SERENGETI BOYS IMEBEBA MADENI YA TFF

Na ZAINAB IDDY-DAR ES SALAAM


HIVI karibuni tumeshuhudia kampuni ya udalali ya Yono, ikizifungia ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na kukamata basi la timu ya taifa ambalo kwa sasa ilinatumiwa na vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ kwa kosa la kutolipa malimbikizo ya kodi inayodaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Sakata la TFF na TRA lilianza Desemba 4, 2015 pale TRA Mkoa wa Ilala ulipozizuia fedha kwenye akaunti zote za shirikisho hilo kwa madai ya kutaka walipwe kiasi cha Sh bilioni 1.6 ikiwa ni kodi kwa kipindi cha 2010 – 2013.

Fedha hizo zinatajwa kuwa ni zile za makato kwenye mishahara (PAYE) ya walimu wa kigeni, Jan Poulsen, Kim Poulsen na Jacob Michelson pamoja na ongezeko la thamani (VAT) kwenye mchezo wa Timu ya Taifa (Taifa Stars) dhidi ya Brazil uliofanyika mwaka 2010.

Wakati TFF ikionekana ina madeni lukuki ya TRA pamoja na kukosa ofisi za kufanyia kazi zake, imekwenda kuwaweka kambi ya mwezi mmoja wachezaji 23 wa Serengeti Boys nchini Morocco kujiandaa na michezo ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wa umri huo nchini Gabon, Mei 14, mwaka huu.

Ikiwa kambini, Serengeti Boys itacheza mechi za kirafiki zisizopungua mbili dhidi ya wenyeji Morocco kati ya Tunisia au Misri, huku Mei mosi ikienda Younde, Cameroon kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya wenyeji wao kabla yakuelekea Gabon Mei 7.

Kabla ya kwenda kuweka kambi Morocco, Serengeti Boys iliyopangwa kundi B pamoja na timu za Mali, Niger na Angola, ilicheza michezo mitatu ya kirafiki ya kimataifa ambayo ni dhidi ya Burundi ‘Intamba Murugamba’ na kushinda mabao 3-0, kabla ya kurudiana tena Aprili 1 na kushinda 2-0, mechi zote mbili zilipigwa Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, kabla ya kulazimishwa sare ya 2-2 na Ghana ‘Black Starlets’ Aprili 3 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hii inaonyesha wazi TFF imeamua kuibeba timu hii pasipokujali wana madeni ya kiasi gani na vipi wadau wa soka wanawazungumzia, baada ya hivi sasa ofisi zao kuwa katika vijiwe vya kahawa.

Inakumbukwa kuwa Serengeti Boys inayonolewa na kocha Bakari Shime, anayesaidiana na mshauri wa benchi la ufundi Poulsen, ilianza kuundwa kwa kufanyika utafutaji wa vipaji vya soka katika mikoa mbalimbali hapa nchini  kwa kuwapa kazi jopo la majaji na kuwaweka pamoja kwa zaidi ya miaka miwili sasa na hata ilipoanza harakati ya kutafuta nafasi ya kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, gharama zote zilibebwa na TFF.

Kulingana na hali ya madeni inayoiandama TFF, walikuwa na uwezo wa kuvunja kambi ya mwezi mmoja ya Morocco na kiasi cha zaidi ya bilioni moja kitachotumika kingeweza kupunguza madeni yanayoikabili.

Lakini kwa kuwa TFF chini ya Rais Jamal Malinzi wanahitaji kuibadilisha Tanzania hasa kwenye soka la vijana, wameona ni heri waendelee kuwa na ofisi katika vijiwe vya kahawa au chini ya miti ili kutimiza ndoto za vijana hao na Watanzania kwa ujumla juu ya kushiriki mashindano makubwa Afrika.

Hili ni jambo kubwa la thamani lililoonyeshwa na TFF kwa Serengeti Boys, hivyo nao lazima waonyeshe jinsi ya kuilinda heshima ya shirikisho hilo na taifa kwa ujumla.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,220FollowersFollow
521,000SubscribersSubscribe

Latest Articles