29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

Serengeti Boys hakuna kulala Taifa linawaangalieni

serengeti-boys-ushindi

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM

FURAHA, faraja na matumaini ya Watanzania katika soka yamebaki kwa timu ya taifa ya vijana ya chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Boys) ambayo inawania kufuzu kucheza fainali za Afrika zitakazofanyika jijini Antananarivo, Madagascar kati ya Aprili 2-16, 2017.

Ni fahari  ya kila Mtanzania kuona timu hiyo inavuka hatua nyingine katika michezo ya awali ya kufuzu fainali hizo kwa matumaini ya kuibuka bingwa wa michuano hiyo mwakani.

Mbali na michezo mingine kufanya vibaya, lakini matarajio hayo yanatokana na timu ya Taifa “Taifa Stars” kufanya vibaya zaidi katika michezo ya kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani, ambapo hadi sasa hakuna uwezekano wa kufanya vizuri.

Kwani kwa sasa Stars ndiyo inashika mkia katika kundi G, linaloongozwa na Misri, ikifuatiwa na Nigeria.

Kufanya vizuri kwa timu ya Serengeti Boys imeonekana kuwa kichocheo kizuri cha kurejesha matumaini hayo kwao.

Katika hilo tayari Serengeti Boys imethibitisha kwamba inaweza kufika mbali baada ya matokeo ya michezo ya awali ambayo kwa kiasi kikubwa yanawafuta machozi Watanzania wengi waliovunjika moya na mapenzi ya soka.

Baada ya kuibwaga nje timu ya vijana ya Shelisheli kwa jumla ya mabao 9-0 na kutoa sare ya bao 1-1 dhidi ya timu ya vijana ya Afrika Kusini, imeonekana huenda safari hii mambo yakawa mazuri.

Lakini Kocha Mkuu wa timu hiyo, Bakari Shime, amesema kwamba matokeo ya sare yalitokana na ugeni wa mazingira na safu ya ushambuliaji ya timu hiyo kuwa butu.

Shime anaongeza kwamba tatizo hilo haliwezi kurudisha nyuma matumaini na matarajio ya Watanzania katika kuamini juu ya mafanikio ya timu hiyo.

Kocha huyo anasema kwamba  hadi sasa hakuna majeruhi katika kikosi chake na kazi yake ni kufanya vizuri zaidi katika michuano hiyo.

“Hali ya hewa na mazingira yalichangia kufanya vibaya katika mchezo dhidi ya Afrika Kusini, lakini tuna matumaini ya kufanya vizuri kwenye uwanja wa nyumbani.

“Haitakuwa kazi rahisi, lakini hatuna jinsi, tutapambana kadri tuwezavyo kuhakikisha tunafanikisha matumaini na matarajio ya Watanzania,” anasema Shime.

Shime anasema kwamba maboresho makubwa anayotakiwa kuyafanya yanahusu safu ya ushambuliaji ambayo ghafla imeonekana kupungua makali.

“Kila eneo linahitaji maboresho, lakini safu ya ulinzi ni sehemu ambayo inatakiwa kufanyiwa mkazo wa kuhakikisha inarudi katika uhalisia wake,” anasema Shime.

Shime anasema kwamba mafanikio ya timu hiyo yanatokana na kujituma kwao na mapenzi ya Watanzania ambao wameonesha kufarijika na kiwango chao.

Agosti 21 mwaka huu timu hiyo itacheza mchezo wa marudio dhidi ya timu ya Afrika Kusini katika Uwanja Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo utakuwa muhimu kwa Serengeti Boys, ambayo itakuwa ikitafuta pointi tatu ili kuweza kusogea karibu na mawazo ya Watanzania wanaoamini kwamba hiyo ndiyo timu ya mafanikio kwao.

Mshindi wa jumla kati ya Serengeti Boys na Afrika Kusini atacheza na mshindi kati ya Namibia na Congo-Brazzaville.

Shime, anasema kwamba; “Ushindani utakuwa mkubwa, lakini mimi nimelenga kushinda michezo yote iliyo mbele yangu. Si kwamba napigania kufuzu kwenda Madagascar tu kwenye fainali za Afrika, la hasha, nataka timu hii niipeleke Kombe la Dunia la vijana.”

Fainali za Kombe la Dunia mwakani zitapigwa India na Serengeti Boys ikifuzu kucheza fainali za Afrika na kuingia nusu fainali itashiriki fainali hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles