SERA RAFIKI ZA UWEKEZAJI NI MUHIMU KWA UCHUMI

0
373

Na Justin Damian


PAMOJA na nia ya kutaka kujikwamua kiuchumi, Tanzania bado ni nchi maskini duniani. Bajeti ya Serikali bado inategemea wafadhili pamoja na mikopo kwa kiasi kikubwa.

Utegemezi huu umekuwa na changamoto kubwa kwa kuwa  mipango mingi ya maendeleo inashindwa kutekelezwa kwa wakati kutokana na ukosefu wa fedha.

Jitihada za kuifanya nchi kujitegemea kupitia vyanzo vya ndani bado ni changamaoto pia. Ripoti ya hali ya uchumi iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania kwa mwezi Machi inaonyesha ukusanyaji mapato kupitia kodi haukufanya vizuri.

Kwa mujimu wa taarifa hiyo, katika kipindi cha mwezi Machi, serikali ilijiwekea malengo ya kukusanya shilingi bilioni 492.8 kutoka kwenye bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi, lakini badala yake ilifanikikwa kukusanya shilingi bilioni 408.6 ikiwa na maana kuwa ilishindwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 84.2.

Serikiali ililenga kukusanya shilingi bilioni 626.3 lakini makusanya halisi yalikuwa ni shilingi bilioni 559.5 ikiwa na maana kuwa shilingi bilioni 66.8 hazikuweza kukusanywa kama ilivyotarajiwa.

Malengo ya makusanyo kutoka katika vyanzo visivyo vya kikodi yalikuwa ni shilingi bilioni 226.7 huku makusanyo halisi yakiwa shilingi bilini 97.6 ikiwa na maana kuwa kiasi cha shilingi bilioni 129.1 hakiweza kukusanywa.

Serikali pia ililenga kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 91.8 kupitia vyanzo vingine vya kodi lakini iliweza kukusanya shilingi bilioni 86.7 huku shilingi  5.1 zikishindwa kukusanywa.

Kwenye vyanzo vyote vitano ambavyo Serikali ililenga kukusanya mapato kulingana na ripoti hiyo, ni chanzo kimoja tu ambacho kimeweza kufanya vizuri kwa kufikia malengo. Chanzo hicho ni makusanyo kupitia bidhaa za ndani na huduma ambapo malengo yalikuwa ni kukusanya shilingi bilioni 250.0 lakini makusanyo halisi yalikuwa ni shilingi bilioni 256.3 ikimaanisha shilingi bilioni 6.3 zilikusanywa juu ya lengo.

Sehemu nyingine ambayo serikali ilikuwa ikitarajia kupata fedha ni ruzuku ambapo lengo lilikuwa ni kupata shilingi bilioni 146.2 lakini illiweza kupata shilingi bilioni 14.2 huku kiasi cha shilingi bilioni 132 kikishindwa kupatikana.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa Serikali imeshindwa kufikia malengo ya makusanyo karibu kwa kila chanzo. Kushindwa kufikiwa kwa malengo ni kiashiria kibaya kwa Serikali kwa kuwa kama ambavyo ripoti inaonyesha, fedha za wafadhili kwa maana ya ruzuku upatikanaji wake umekuwa mgumu zaidi na pengine itakuwa ni jambo la busara kama Serikali itaamua kutafuta chanzo kingine.

Kwa upande mwingine, deni la taifa nalo linaendelea kukuwa kwa vile Serikali inalazimika kukupa ili kupata fedha za kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo. Kukuwa kwa kasi kwa deni la taifa si jambo zuri sana na tayari taasisi za kimataifa kama Benki ya Dunia (WB) pamoja na Shirika la Fedha Duniani (IMF) zimeionya Tanzania kuhusiana na suala la ukopaji.

Naibu Mkurugenzi wa IMF Tao Zhang ambaye aliitembelea Tanzania hivi karibuni alisema ni muhimu kwa nchi kuwa na deni ambalo inaweza kulimudu .

Mkurugenzi huyo alisisitiza Serikali  kufanya jitihada za kuhamasisha upatikanaji wa fedha kutoka ndani ya nchi kupitia ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.

Ushauri huu wa IMF unaweza kuwa na changamoto ya utekelezaji kwa kuwa kwa sasa biashara nyingi kwa maana ya sekta binafsi hazifanyi vizuri na ndiyo sababu mapato ya Serikali kupitia kodi yameshuka pia.

Ili kujitoa kwenye hali hii, ni muhimu kwa Tanzania kutengeneza sera ambazo zitawavutia wawekezaji. Wawekezaji wamekuwa wakilalamika kuwa Tanzania kwa mfano imekuwa haina sera za kikodi zinazotabiriki. Leo mwekezaji anaweza kutakiwa kulipa kiasi fulani na kesho ikabadilika.

Kama alivyowahi kusema Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ukitaka kula ni lazima na wewe ukubali kuliwa kidogo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here