27.5 C
Dar es Salaam
Sunday, December 3, 2023

Contact us: [email protected]

Sendiga aicharukia kampuni ya YI SEN kwa kunyanyasa wafanyakazi Mufindi

Na Raymond Minja, Iringa
 
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Queen Sendiga amekipa siku 30 kiwanda cha kuchakata mazao ya misitu cha YI SEN International Investment Co. Ltd kuhakikisha kinashughulikia changamoto zote zikiwemo za wafanyakazi na kwamba iwapo kitakiuka kufanya hivyo ataagiza mamlaka zikifunge.

Sendiga ameyasema hayo leo Jumanne Septemba 21, baada ya kutembelea kiwanda hicho kilichoko Mufindi na kubaini ujanja ujanja huo unaofanywa na wamiliki wa kiwanda hicho.

“Ndani ya mwezi mmoja, Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya nikute ripoti ya maandishi inayoonesha jinsi changamoto hizo zilivyoshughulikiwa. 

“Hatua itakayofuata ni kuwasiliana na mamlaka zinazotoa vibali vya uwekezaji na biashara ili kukifunga kisiendelee na uzalishaji na biashara,” amesema Sendiga.
 
Aidha, Sendiga amekipiga marufuku kiwanda hicho kununua magogo kwa njia ya mnada akisema mtindo huo unawanyonya wakulima wa malighafi hiyo na hatari kwa makusanyo ya serikali.

Awali, baadhi ya wafanyakazi waliomba kiwanda hicho kifungwe hadi pale kitakapotimiza matakwa yote ya kisheria katika uwekezaji wake.

Wafanyakazi hao walisema wanashindwa kuelewa nguvu waliyonayo Ongozi wa kiwanda hicho hadi kuwafanya wapuuze baadhi ya sheria za uwekezaji nchini hatua inayominya upatikanaji wa haki zao na uwezekano wa serikali kupoteza baadhi ya kodi zake.
 
Aidha, wamezilalamikia baadhi ya mamlaka zinazotakakiwa kuhakikisha kiwanda hicho kinazingatia sheria za uwekezaji na za nchi wakisema haziwachukulii hatua stahiki na ndio sababu yanayoendelea kiwandani hapo yanawaumiza.
 
Hivi karibuni Mkuu wa mkoa huyo alitembelea kiwanda hicho kwa lengo la kupata taarifa ya kiwanda hicho na kutoa pole baada ya mmoja wafanyakazi wake (hakutajwa jina) ambaye hakuwa na kofia ya usalama kuvutwa na moja ya mashine kiwandani hapo na kufariki dunia.
 
Mbali na baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hicho kutopewa vifaa vya usalama wawapo kazini, katika ziara hiyo,Sendiga alielezwa na wafanyakazi hao changamoto nyingine zinazokikabili kiwanda hicho.

Changamoto hizo zilizothibitishwa na Afisa Utumishi wa kampuni hiyo, Loveness Myovella baada ya kuulizwa kama kweli anazitambua ni pamoja na maslahi duni ya wafanyakazi, kutolipwa malipo ya muda wa ziada na baadhi yao kutosajiliwa katika mifuko ya jamii.
 
“Pamoja na kufanya kazi kwa muda mrefu katika kiwanda hiki, hatujasaliwa katika Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) lakini pia hatujasajiliwa kwenye Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), watendaji wa mifuko hiyo wamekuwa wakija lakini hakuna hatuna zinazochukuliwa,” alisema mmoja wao kwa jina la Siwonike.
 
Siwonike alisema wana hofu hata mfanyakazi mwenzao aliyefariki kiwandani hapa hivi karibuni hakuwa amesajiliwa katika mifuko hiyo.
 
“Kuna haja NSSF na WCF wakafanya ukaguzi wa pamoja katika kiwanda hiki ili wajionee ni wafanyakazi wangapi wamesajiliwa katika mifuko yao na kwanini wengine hawana usajili huo,” alisema.
 
Alisema iwapo itabainika mfanyakazi huyo aliyefariki akiwa kazini hakuwa amesajiliwa katika mifuko hiyo (NSSSF na WCF), ni muhimu sheria za nchi zikatumika kukipeleka mahakamani kiwanda hicho kinachozalisha marine board zinazotumika katika ujenzi wa ghorofa na madaraja ili haki iweze kutendeka.
 
Mfanyakazi mwingine, Kiteve Kiteve alisema umasikini wao umewafanya wafanye kazi katika mazingira magumu na hatari kwa afya zao katika kiwanda hicho chenye vumbi kali la udongo na mbao na akasisitiza pamoja na maelekezo mazuri ya mkuu wa mkoa, kifungwe ili kiweze kutimiza taratibu, kanuni na sheria zote za nchi.
 
“Kiwanda kinajulikana kwa jina la YI SEN International Investment Co Ltd. Tunaomba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Viwango (TBS), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) waje wajiridhishe kama shughuli zake za uzalishaji na biashara zinazingatia taratibu,” alisema na kuliomba pia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) wafike wajionee mazingira ya kiwanda hicho yasivyo rafiki.
 
Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Saad Mtambule
alisema baada ya tukio la kifo cha mfanyakazi huyo, yeye na kamati yake ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya walikitembelea na kubaini kuwapo kwa changamoto nyingi.
 
“Tulichokiona hapa kinatakiwa kushughulikiwa kwa kasi kubwa, mbali na malalamiko mengi ya wafanyakazi na uendeshaji wa kiwanda, mazingira ya kiwanda hiki sio rafiki,” alisema huku akipokea maelekezo ya Mkuu wa mkoa yanayotaka mamlaka zinazohusika kuchukua hatua.
 
Aidha, amemtaka Afisa Utumishi wa kiwanda hicho na wakalimani wake akiwataka wafanye kazi na kampuni hiyo ya kichina huku wakitambua kwamba wao bado ni watanzania kwahiyo wana wajibu wa kutetea maslai ya nchi yao na watanzania wenzao.
 
Mmoja wa wakalimani hao ambaye hakutaka kutaja jina lake alijitetea akisema wao wameajiriwa kiwandani hapo kurahisha mawasiliano kati ya wawekezaji hao, wafanyakazi na mamlaka zingine.
 
“Hapa wakulaumiwa ni mamlaka zenyewe zinazotakiwa kuchukua hatua, sisi kama wakalimani hatuhusiki. Nimekuwa nikishauri mara kwa mara mamlaka hizo zinapokuja kukagua kiwanda hiki, ziangalie pia uwezekano wa kuja na wakalimani wao ili kuondoa hofu ya kupewa tafsiri potofu,” alisema.

 
Juhudi za kupata ufafanuzi wa tuhuma hizo hazikuzaa matunda baada ya Meneja wa Kiwanda hicho, Lin Xin Zong kusema hawezi kuongea kwa kuwa yeye si msemaji wa kampuni hivyo wasubiri mpaka mwenye kampuni hiyo atakapowasili ambako haikujulikana anatoka wapi jambo ambalo lilifanya waandishi waondoke kwa kuwa muda ulikuwa unekwenda na kuahidi kurudi kesho yake lakini walipofika wahusika wakisema hawana muda wa kuongea na wanahabari.
 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles