Na Mwandishi Wetu-ZANZIBAR
HATUA ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kutangaza mabadiliko mapya ya kima cha chini cha mshahara, inaonekana kutikisa sekta ya utalii visiwani hapa.
Mabadiliko hayo yameitikisa sekta hiyo, huku ikiwamo hatari ya kupunguzwa kwa wafanyakazi kwenye hoteli za kitalii kutokana na wamiliki kushindwa kulipa kima kipya cha chini cha mishahara ambacho kimepandishwa kwa asilimia 109.
Akizungumza na MTANZANIA jana, mmoja wa wawekezaji wa sekta ya utalii Zanzibar, ambaye hakuwa tayari kutajwa jina lake gazetini, alisema hatua ya Serikali kupandisha mishahara kwa kima cha chini, imewafanya kwa sasa kulazimika kumlipa mfanyakazi mmoja zaidi ya Sh 500,000 kwa mwezi jambo ambalo ni gumu kwa biashara hiyo.
Alisema mabadiliko hayo yaliyofanywa na Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto, Maudline Cyrus Castico, hayakuzingatia hali halisi ya biashara ya uwekezaji ya utalii na badala yake sasa anakwenda kuwanyima fursa ya ajira Wazanzibari walioajiriwa kwenye hoteli za kitalii.
“Wakati wa Uchaguzi Mkuu Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, aliahidi kupitia ilani ya CCM kupandisha kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa Serikali kutoka Sh. 150,000 hadi 300,000.
“Lakini katika hali ya mshangao, sasa jambo hilo limebadilika, Waziri wa Kazi bila kushirikisha wadau wakiwamo waajiri wa sekta ya utalii, ameamua kwa utashi wake binafsi kupandisha viwango hivi na kufikia Sh. 300,000 kama ni mshahara ambao bado haujajumuisha kodi, nyumba na michango ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) ambao ukijumlisha malipo yote hayo, sasa kwa mfanyakazi mmoja anakwenda kulipwa zaidi ya Sh. 500,000,” alisema mdau huyo.
Licha ya hali hiyo, inaelezwa uamuzi huo wa Waziri Castico hajawashirikisha wawekezaji wa sekta ya utalii jambo ambalo limezua malalamiko.
Akizungumzia hali hiyo Rais wa Chemba ya Biashara Zanzibar, Toufiq Turuki, alisema kuwa hatua ya Serikali kufanya mabadiliko hayo inakwenda moja kwa moja kuumiza wananchi ambao ndio wamekuwa wakinufaika na ajira katika sekta ya utalii visiwani hapa.
“Tumetoa ajira zaidi ya 80,000 kupitia sekta ya utalii ambao humo wapo wahudumu wa hoteli, wafuaji, wasambazaji wa vyakula, hasa samaki, sasa leo unapokuja na mabadiliko haya bila kushirikisha, ni wazi sasa tunakwenda kuyumbisha uchumi wa Zanzibar.
“Mwaka jana baada ya kuwepo taarifa ya mabadiliko haya, tulikaa pamoja na Serikali, tena wao walitaka kupandisha tu, lakini baada ya kuonekana kuna ugumu ikabidi iundwe kamati maalumu ambayo ilishirikisha Jumuiya ya Wawekezaji wa Sekta ya Utalii Zanzibar (ZATI) na mwisho tulikubaliana ufanyike utafiti kwanza chini ya Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa (ILO).
“Ile ripoti ya utafiti imekamilika, lakini hadi leo hatujaambiwa nini kilichobainika zaidi ya kusikia kupandishwa kwa kima cha chini,” alisema Turuki.
Alisema sekta ya utalii inawagusa wadau mbalimbali wakiwamo wawekezaji katika maeneo ya hoteli, migahawa na watembeza wageni.
Naye Mwenyekiti mstaafu wa ZATI, Abdul Ahmed, alisema hatua hiyo ya Serikali kupandisha kima cha chini kwa sekta binafsi kitawaathiri kwa kiwango kikubwa.
AJIRA ZILIZOSHUKA
Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa za Serikali ya Zanzibar, kiwango cha ajira kimeshuka kutoka ajira 1,597 mwaka 2015 hadi 1,071 mwaka 2016.
Hayo yamebainishwa na Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi, ilipokuwa ikiwasilisha taarifa yake kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Serikali, mwelekeo wa uchumi na mpango wa maendeleo kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Kutokana na hali hiyo, inaelezwa kuwa mazingira ya kufanya biashara Zanzibar bado ni magumu na hayamshawishi mwekezaji.
RIPOTI YA ILO
Taarifa kutoka ndani ya SMZ zinaeleza kuwa baada ya kufanyika kwa utafiti wa upandishaji wa mishahara katika sekta binafsi ambayo hugusa utalii, ripoti ya Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa (ILO) ilipendekeza kima cha chini kipande na kuwa Sh 243,000.
Hata hivyo katika hali ya kushangaza, Waziri wa Kazi, aliamua bila kushirikisha wadau na kupandisha kiwango cha juu kuhusu mishahara.
Sekta ya Utalii Zanzibar imekuwa ikichangia uchumi wa Zanzibar kwa asilimia 7 kwa mwaka jambo ambalo sasa linaweza kuathirika na kushuka ikiwa wafanyakazi wa sekta hiyo watapungua.
MISHAHARA SEKTA BINAFSI
Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto, ilitangaza kima kipya cha mishahara kwa wafanyakazi wa sekta binafsi Zanzibar, kuanzia Julai Mosi mwaka huu.
Mabadiliko hayo yamefanyika kwa chini ya kifungu cha 97 (1) cha sheria ya ajira nambari 11 ya mwaka 2005.
Kima cha chini kwa wafanyakazi wenye mikataba ya maandishi kwa taasisi ndogo zitakazoainishwa kwenye kanuni kimeongezeka kutoka Sh 145,000 hadi 180,000.
Kwa wafanyakazi wenye mikataba ya maandishi imeongezeka kutoka kiwango cha sasa cha Sh 145,000 hadi 300,000.
Kwa vibarua wa kutwa wenye ujuzi, kimeongezwa kutoka Sh 10,000 hadi 30,000 kwa siku na kwa vibarua wa kutwa wasio na ujuzi, kimeongezwa kutoka Sh 7,000 na kufikia 25,000.
KAULI YA WAZIRI CASTICO
Akizungumza jana na MTANZANIA, Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto, Castico, alisema kwa sasa wanatafuta ufumbuzi wa suala hilo kwa kukutana na wawekezaji wa hoteli Zanzibar.
“Tutakaa nao ili kuweza kujua hoja yao ni nini na suala lao tayari tumeashaanza kulifanyia kazi. Kwa sasa siwezi kuzungumza lolote, nina wageni. Nakuomba uchukue hilo kwanza,” alisema Waziri Castico.
WAZIRI WA BIASHARA
Kutokana na mtifuano huo, gazeti hili lilimtafuta Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Balozi Amina Salum Ali, ambaye alisema kuwa ni vema wawekezaji hao warudi kwenye meza ya mazungumzo kuliko kupunguza wafanyakazi kwenye mahoteli jambo ambalo linaweza kuathiri uchumi wa Zanzibar.
“Hili jambo lipo chini ya Waziri wa Kazi ambaye ndiye anasimamia na alifuata taratibu zote, nimesikia matamko mbalimbali juu ya suala hili, ila ninachowaomba warudi ili tuweze kuzungumza kwenye utatu kwani sekta binafsi tunatambua ina mchango mkubwa kwa uchumi wa nchi yetu.
“Niliwasilisha na watu wa Chemba ya Biashara na wao walisema kuwa watapunguza wafanyakazi na hata kufunga mahoteli, lakini wamesema wataandika barua nami ikija kwangu nitaifikisha kwa waziri mwenye dhamana ili tuweze kukaa chini na kutafuta ufumbuzi wa pamoja,” alisema Balozi Amina.