26.7 C
Dar es Salaam
Thursday, September 21, 2023

Contact us: [email protected]

SEKTA YA UTALII ZANZIBAR YAGUSA UCHUMI WA MUUNGANO

Na MWANDISHI WETU

-ZANZIBAR

KATIKA siku za hivi karibuni Sekta ya Utalii nchini imekumbwa na mtikisikio mkubwa, hasa baada ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kutangaza nyongeza ya mishahara kwenye sekta binafsi, jambo ambalo lilizua mjadala mkubwa visiwani pamoja na wadau wa sekta hiyo Tanzania Bara.

Hatua ya kutangazwa kwa mabadiliko hayo kwa asilimia 109 ilifanywa na Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Wazee, Vijana Wanawake na Watoto, Maudline Cyrus Castico, jambo ambalo lilizua malalamiko kutoka kwa wadau, hasa wawekezaji wa mahoteli ambao wanaajiri wafanyakazi wengi visiwani hapa.

Hata hivyo, uchumi wa Zanzibar unategemea kwa kiasi kikubwa mapato yatokanayo na utalii, ambapo Zanzibar hupokea watalii wengi wa moja kwa moja kutoka nchi ya Italia, ambao ni karibu asilimia 40 ya watalii wote wanaotembelea Zanzibar hutokea huko Italia.

Asilimia 60 ya watalii wanaotembelea Zanzibar huletwa na kampuni kubwa za utalii ambazo zina makao makuu yake  Arusha na hawa baada ya kutembelea mbuga hizo, watalii hao huishia kwa mapumziko kwenye fukwe Zanzibar pamoja na kutembelea Mji Mkongwe, ambao ni moja ya sehemu za urithi wa dunia.

Kimsingi au kwa maneno rahisi, utalii wa Zanzibar unategemea sana soko la utalii la kaskazini ya Tanzania ambapo kuna mbuga kama za Serengeti, Manyara, Ngorongoro pamoja na Tarangire.

Hivi karibuni wawekezaji hao wa kampuni kubwa zinazojishughulisha na utafutaji wa watalii kwenye masoko ya Ulaya na Marekani wamekuwa wakilalamikia hatua ya Serikali za Zanzibar kuongeza kima hicho cha chini, hasa kwa sekta binafsi, jambo ambalo linaweza kuleta hatari ya wananchi wengi, hasa wa visiwani hapa kupoteza ajira.

Hatua hiyo inaweza pia kuathiri uchumi wa Zanzibar, huku visiwa kama Shelisheli pamoja na Mauritius vikijikuta vikinufaika na idadi ya watalii wanaotembelea visiwani vya huko.

Kutokana na sintofamu hiyo, MTANZANIA ilizungumza na Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Dk. Ibrahim Mussa, aliyesema atafuatilia kwa kina kujua kiini cha suala hilo na kulipeleka kwenye Kamati ya Majadiliano, ambayo huhusisha Zanzibar na Tanzania Bara.

“Ni kweli Utalii wa Bara hutegemeana na Zanzibar na katika hili lililotokea na kuzua hayo malalamiko nitalifuatilia na kisha kwenda kulijadili kwenye kamati ya majadiliano ambayo huhusisha pande zote za Muungano.

“Tunajua wapo watalii ambao wakishatoka kutembelea mbuga kwa ajili ya kuona wanyama hutaka kwenda kutalii kwenye fukwe, hasa Zanzibar na kisha kurejea nchini mwao,” alisema Dk. Mussa.

Kwa mujibu wa takwimu mbalimbali, ikiwamo za Serikali, zinaonyesha kwamba kati ya asilimia 100 kuna watalii zaidi ya asilimia 40 ambao huingia Zanzibar moja kwa moja  ambao hununua likizo zao kwenye makampuni yanayouza mapumziko katika visiwa tofauti duniani huko Ulaya.

Wengi kati yao, wakiwamo raia kutoka Italia, Hispania, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza na nchi nyinginezo za mataifa ya Ulaya, hupata bei za utalii kwa urahisi, lakini mara nyingi ndege hujazwa kutokana na wingi wa watu.

Watalii hao huenda Zanzibar kwa wiki moja na bei huku wanayolipa huwa moja kwa moja na usafiri wa ndege, chakula, vinywaji pamoja na usafiri wa kutoka uwanja wa ndege kwenda hotelini na kurudi tena uwanjani kwa ajili ya safari ya kurudi nchi walizotoka.

Kutokana na aina hiyo ya wageni, Zanzibar hushindana na nchi kama Thailand, Tunisia, Morocco, Spain, Visiwa vya Ugiriki kama Crete, Mexico, Cuba, St. Lucia pamoja visiwa vingine.

Na wanaouza Zanzibar huko Ulaya tayari wanasema kuwa Zanzibar ni bei ghali, sasa ikiwa mishahara itapanda kupindukia na hao itawafanya wapandishe bei, ina maana katika mapumziko ya mwaka 2018 wataiondoa Zanzibar katika mabango ya kuitangaza, hasa kwenye mitandao ya kununua likizo za mapumziko.

Kwenye kundi la kuuza hilo linaweza kusababisha pigo katika hilo kwa asilimia 45 ya wageni, hasa Waitaliano  wanaokuja Zanzibar moja kwa moja.

“Msione wazungu hawa Waitaliano mkaona ni matajiri, hawa wengi ni watumishi wa umma na mafundi, ni watu wa kawaida na hujipanga miezi nyuma kununua hizo likizo,” Nassor Khalfan Ally, ambaye ni mmoja wa wawekezaji wa utalii visiwani hapa, anasema.

Inaelezwa kuwa, makampuni hayo makubwa yanapenda kuuza Zanzibar kwa wazungu kutoka Ulaya, hasa hawa wa bei nafuu, lakini ikiwa bei itakuwa ya kupindukia na wao wanaweza kuamua kupeleka ndege zao maeneo mengine na si Zanzibar, maana nguvu wanayo wao wa kuamua kuiweka Zanzibar katika orodha za visiwa kwa ajili ya mapumziko.

Ndiyo maana hata ukienda kwenye taarifa zao kwenye mitandao na ukienda kwenye hoteli za Waitaliano, aina ya vyakula na vinywaji ni vya kawaida na kila kitu wanaweka mahesabu ili kubana matumizi.

Zanzibar wakipungukiwa na aina ya wageni hao kuna hatari ya kupoteza kodi kama za visa, matumizi na manunuzi ya huduma kama chakula, umeme, usafiri wa matembezi.

Kutokana na hali hiyo, ajira kubwa kupotea, maana wingi wao kuja Zanzibar unawapatia Wazanzibari biashara tofauti ya huduma na manunuzi ambapo mmoja wa vijana wanaojishughulisha na uchongaji wa vinyago katika Mtaa wa Gizenga, Joseph Mgaya, alisema hatua hiyo ya Serikali inawaathiri pia.

“Ni kweli hawa hawatumii sana, lakini wana nafasi yao kubwa sana katika uchumi na wakianza kuwasili mwezi wa saba, hawasimami kuleta wageni mpaka mwaka unaofuata mwezi wa Aprili kabla ya msimu wa mvua kubwa na husimamisha kwa miezi mitatu.

“Na kwa hili la kutangaza hicho kima cha chini, athari kubwa unaiona, hivyo ni lazima Serikali itambue, wanaotangaza, kuuza pamoja na kuwaleta hawa Waitaliano ni wazungu wenyewe wa kundi hili la package tourists,” alisema Mgaya.

Naye mwekezaji wa hoteli, Nassor Khalfan Ally, alisema: “Kwa hiyo wenye maamuzi ni wao wenyewe. Wanauza bei rahisi ili wajaze ndege, ukiwachezea kwenye hesabu yao basi na wao wanaweza kuhama kama njiwa. Na kuwarudisha inakuwa juhudi za ziada.”

Ikiwa Serikali itabariki uamuzi wa Waziri Castico, kuna hatari nayo ikakwama kwenye mikakati yake iliyotangazwa kwa muda mrefu ya ukuzaji wa utalii visiwani humo na SMZ.

Akizungumza na MTANZANIA, mwekezaji mmoja raia wa nchi za Ulaya, alihoji kwa hasira huku akisisitiza kutoandikwa jina lake: “Inakuwaje uchumi wa Zanzibar ambao unategemea utalii anaachiwa waziri mmoja tu kufanya maamuzi makubwa, huku imeshaleta ufa na sintofahamu katika biashara zetu.

“Sisi ndio tunaojua hii biashara ya utalii na ndio tunaohangaika, lakini vikwazo vya aina hii vinatufanya wakati mwingine kuvunjika moyo,” aliongea kwa sauti kubwa ya huzuni.

Kutokana na utalii kuwa tegemeo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilianzisha Programu ya Maabara ya Utalii katika juhudi za kujua na kuondoa changamoto zinazoikabili Sekta ya Utalii, ili kuendelea kuchangia pato la nchi na kuinua hali ya uchumi na kijamii sambamba na kuimarisha sekta zote zilizopo nchini.

Lengo kuu la programu hiyo ni kuimarisha utalii wetu na kufikia utalii wa daraja la juu kama inavyoelezwa katika Sera ya Utalii na Mipango Mikuu ya Serikali kwa madhumuni ya kuongeza wigo wa masoko ya utalii.

Kamisheni ya Utalii kwa kushirikiana na wadau wa utalii ilifanikisha safari mpya za ndege za utalii kutoka nchini Ukraine na Poland kuja Zanzibar.

Mbali ya ndege hizo, Kamisheni ya Utalii imetilia mkazo zaidi katika kuyafikia masoko ya utalii ya China, India, Urusi na Israel, bila kuathiri harakati zetu za kujitangaza katika masoko yetu ya zamani, ikiwamo Italia, Ujerumani, Uingereza na Ufaransa.

Na kwa mujibu wa takwimu, zinaonesha kuwa wageni kutoka katika masoko mapya ya Urusi, India, China na Israel wameongezeka kutoka 22,106 mwaka 2014 hadi kufikia 29,070 mwaka 2015, sawa na ongezeko la asilimia 39.

Kamisheni ya Utalii kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, wamefanya utafiti wa siku za ukaazi kwa mgeni na matokeo yanaonesha kuwa wastani wa siku za ukaazi kwa mgeni zimeongezeka kutoka 7.7 mwaka 2014 hadi kufikia 8.5 mwaka 2015 na kama nyongeza hiyo itafanyika, kuna hatari ya kuyumba kwa Zanzibar, ikiwamo kukosa na wageni ambao wanaweza kukaa zaidi ya siku tano.

Sekta ya utalii ndiyo inayochangia maendeleo kwa kiasi kikubwa, kwa vile mbali ya kutoa ajira kwa vijana hapa Zanzibar, imekuwa ikichangia kwa asilimia 80 fedha za kigeni ambazo hutumika katika masuala mbalimbali ya maendeleo.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, katika mwaka 2010 jumla ya watalii wapatao 132,836 walitembelea Zanzibar, ambapo hadi kufikia mwaka 2014 idadi ya watalii iliongezeka na kufikia 31,189, ambapo kwa ujumla wageni waliotembelea Zanzibar hadi kufikia mwaka jana 2015 walikuwa 294,243.

Na malengo yaliyowekwa na SMZ hadi kufikia mwaka 2020 Zanzibar itakuwa na uwezo wa kupokea jumla ya watalii 500,000 kwa mwaka, huku idadi ya hoteli zenye hadhi ya nyota tano zikiongezeka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles