30.8 C
Dar es Salaam
Thursday, November 14, 2024

Contact us: [email protected]

SEKTA YA MADINI YACHANUA TANZANIA

waziri-mkuu

Na Shermarx Ngahemera,

INGAWA hakuna uwekezaji mkubwa wa bayana katika miaka kumi iliyopita, biashara ya madini Tanzania imeendelea kukua na kushamiri kwenye uchumi wa  nchi na kuifanya kuwa ya pili kuleta fedha za kigeni kwa ajili ya uwekezaji kutoka nje (FDI).

Tanzania ni tajiri kwa kubahatika kuwa  na madini ya kila namna na hivyo uchimbaji  na uwekezaji wake umekuwa ukiongezeka kila mwaka kwa upanuzi wa shughuli ingawa bei ya bidhaa za madini katika soko la kimataifa zimekuwa zikianguka.

Hali hiyo hupunguza ari ya uchimbaji na uwekezaji kwenye sekta ya madini na hasa kwenye mafuta na gesi.

Lakini cha ajabu mahitaji ya saruji ambayo huhitaji madini ya viwanda yanaongezeka na wawekezaji wengi wanataka kuwekeza katika kujenga viwanda vya saruji.

Madini ya metali

Hivi basi uchimbaji nchini Tanzania unahusu madini ya metali kama dhahabu, chuma, nikeli, shaba, kobati na fedha. Madini ya viwanda ni yale ya almasi, tanzanite, yakuti (ruby), ganeti, chokaa, magadi soda. Jasi, chumvi, fosfeti, kokoto, mchanga, mawe mkato (dimension stone) na grafaita na madini ya nishati ya makaa ya mawe, urani na gesi.

Shughuli za uchimbaji madini na ukokotaji  nchini Tanzania zinachangia  pato la Taifa kwa kiasi cha asilimia 3.7 ambacho kilifikia dola bilioni 1.78 mwaka 2014 kutoka dola milioni 598 mwaka 2009 ikiwa ongezeko kwa thamani ya asilimia 200 kiasi ambacho kama nchi inaona ni kidogo kutoka kwenye lengo la

Malengo ya Maono ya Maendeleo ya 2025 ya kuwa na asilimia 10 ya pato la Taifa itokane na sekta hiyo.

Mwaka jana, 2015 mapato ya nje kutokana na sekta hiyo yalifikia dola  bilioni 1.37 zikiwa ni asilimia 24 ya mauzo ya nje ya nchi na dhahabu ikiwa ni asilimia 90 ya mauzo madini hayo nje ya nchi.

Mauzo ya almasi yalifikia dola milioni 61.7 wakati yakilingana na mauzo mengine ya madini ya dola milioni 61.7.

Masoko makubwa ya madini ya Tanzania ni Afrika Kusini, India, Uswisi na Australia kwa mauzo ya dhahabu na almasi huuzwa nchi moja tu Luxemburg.

Hazina ya dhahabu ya nchi ni Tanzania inakisiwa kuwa milioni 45, nayo dhahabu nyingi inachimbwa ukanda wa ziwa kwenye greenstone kuzunguka Ziwa Victoria amabako machimbo kadhaa yamegundulika na kuendelezwa na kampuni kubwa za Acacia na Ashanti AngloGold na uzalishaji wa dhahabu ni wastani wa tani 50 kwa mwaka na hivyo kuifanya nchi hii kuwa ya nne kwa kuzalisha dhahabu katika Afrika nyuma tu ya Afrika Kusini, Ghana na Mali.

Uzalishaji wa dhahabu katika Afrika Kusini na Tanzania una sura tofauti kwani wakati Tanzania uzalishaji umeongezeka kwa asilimia 700 katika miaka 25 iliyopita kutoka tani 5 hadi 40 -50 kwa mwaka, Afrika Kusini imepungua kutoka takribani tani  500 mwaka 1990 hadi tani 140 mwaka jana (2015) na hivyo kuporomoka kwenye uzalishaji na kuwa namba 8 kutoka namba moja duniani.

Ukitazama kuyumba kwa uchumi nchini humo hali hiyo lazima izingatiwe kwani anguko la asilimia 200 si mchezo.

Hazina ya Chuma nchini Tanzania iko hasa Liganga, Milima ya Uluguru, Mbabala karibu na Ziwa Tanganyika, Karema, Manyoro Gondite na Itewe.

Liganga ndiyo hazina kubwa kwani kuna hazina iliyothibitishwa ya tani milioni 126.

Tanzania China International Mineral Resources Ltd (TCIMRL), ni kampuni ya ubia wa China na Tanzania yaani Sichuan Hongda Group na National Development Corporation (NDC) ambazo zimepanga kuwekeza dola bilioni 1.8 hapo Liganga kuanzisha machimbo ya chuma na chuma cha pua kutengeneza tani milioni moja kwa mwaka ya chuma na Chuma cha pua na mazao yake ya vanadium pentoxide na titanium diodide.

Huu ni mradi wa siku nyingi na unasusasua kwa sababu soko la chuma la dunia limejaa na China ndiyo inaongoza katika mauzo na uzalishaji.

Habari kutoka NDC zinasema ujenzi wa kiwanda utaanza mwaka 2018 na bajeti ya Serikali inasoma mahitaji hayo kuanzia bajeti ya mwaka huu hadi 2018 na usafirishaji nje utaanza mwaka 2018 -2019.

Tatizo kubwa lilikuwa kupata uwekezaji katika ujenzi wa reli Njombe hadi bandari ya Mtwara na amepatikana na inasemekana chuma itakayozalishwa itatumika sana kwa ujenzi wa reli ya kati.

Madini viwanda

Almasi nchini Tanzania inapatikana katika mgodi wa zamani kuanzia 1948 katika mgodi unaoitwa Williamson Diamonds Mine ambao uko Kusini mwa miji ya Mwanza na Shinyanga. Petra Diamonds na kampuni yake tanzu ya Williamson Diamonds Limited, inahisa asilimia  75 na nyingine 25 ni mali ya Serikali ya Tanzania.

Uzalishaji si mbaya sana kwani unaongezeka baada ya kufanyiwa ukarabati na upanuzi wa kutosha  kwani kampuni hiyo mwaka 2015, ilizalisha karati 202,265 na ina mpango wa kufikia karati 350,000 kwa mwaka huu.

Kwa maelezo ya Petra Diamonds, mgodi wa Williamson una almasi kubwa zenye hazina ya inayokisiwa kuwa ya karati milioni 38.1.

Madini ya vito

 Kuna madini mbalimbali ya vito nchini  ambapo yanahusisha madini aina ya amethyst, aquamarine, ganeti, yakuti, zafarali (sapphire), tanzanite na tomalini, (tourmaline).

Tanzanite ni  madini ya taifa ambapo akiba ya taifa itawekezwa humo kwani madini hayo huchimbwa sehemu moja tu duniani ambapo ni kwenye vilima vya Mererani Mkoa wa Manyara Wilaya ya Simanjiro na inafikiriwa kuwa kwa kufanya hivyo yataheshimika na kuongeza thamani ya shilingi ya Tanzania.

Katika kipindi cha miaka mitano 2008 hadi 2013 uzalishaji wa Tanzanite uliongezeka kutoka tani 768 na kufikia tani 900 ikiwa ni ongezeko la asilimia 17 kila mwaka wakati hazina yenyewe ni karati milioni 500.

Madini ya nishati

Madini ya nishati ya makaa ya mawe yanaakisiwa kuwa na hazina ya tani bilioni 5 kutoka tani bilioni 1.9 za  awali ambazo asilimia 25 yamethibitishwa kuweko kwake.

Machimbo yenye uhakika ni yale ya Ketawaka -Mchuchuma kwenye bonde la  Ruhuhu, Shamba la Ngaka  liliko Kusini Magharibi ya Tanzania  na lile la Songwe Kiwira Coal Field .

Makaa ya mawe yanachimbwa kwa kiasi kidogo na mengi ni miradi inayoendelea kujengwa na ilikuwa kwa ajili ya kutengeneza umeme ingawa sasa Serikali imeamua itumike kama madini ya kiwandani kwenye viwanda vya saruji na kupiga marufuku uagizaji wa madini hao kutoka nje nchini Zimbabwe na Afrika Kusini.

State Mining Corporation (STAMICO) na TanCoal Energy Limited Mine pale Ngaka mkoani Ruvuma.

Uzalishaji wa makaa ya mawe aina ya ‘bituminous coal”  nchini Tanzania uliongezeka sana kati ya miaka ya 2010 hadi  2013 kutoka tani 179 hadi tani 128,920 na mtazamo ni kuongezeka zaidi kwenye miaka ya karibuni kwa ajili ya nishati na malighafi ya viwanda vya saruji.

Urani imethibitika kuwa iko kwa wingi nchini Tanzania na hasa katika maeneo ya Namtumbo kwenye Mto (Mkuju) mkoani Ruvuma, Bahi, Galapo, Minjingu, Mbulu, Simanjiro, Lake Natron mkoani Manyara , Manyoni (Singida), Songea, Tunduru, Madaba and Nachingwea (Mtwara).

Mradi wa Urani wa Mto Mkuju uko kwenye matayarisho na wawekezaji wa Kirusi, Uranium One Inc, walionunua mradi kutoka kwa Waaustralia na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Urusi, Denis Manturov, anasema nchi hiyo itaanza kazi ya uchimbaji wa mgodi huo mwaka 2018. Wanamazingira wanaupinga mradi huo kwa nguvu zote wakidai kuwa uharibifu wake kwa mazingira ni mkubwa na unatishia uwepo wa Mbuga ya Wanyama ya Selous ambayo iko kwenye mkondo wa chini wa Mto Rufiji.

Gesi inapatikana kwa wingi nchini Tanzania na nyingi iko kwenye kina kikuu kilomita 120 bahari kuu na mafuta yako mkoa wa Pwani lakini si kiwango kukubwa cha kibiashaara. Gesi nchi kavu inapatikana mkoani Pwani kilomita 30 Magharibi ya Dar es Salaam  eneo la Ruvu kiasi  cha futi za ujazo trilioni 2.7 na zilizoko baharini ni futi za ujazo trlioni 55.17 katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Mwelekeo

Uzalishaji wa dhahabu nchini Tanzania unaendelelea vizuri kwani hadi kufikia Oktoba 30, mwaka huu kwa Mgodi wa North Mara iliongezeka kwa asilimia 66 katika kipindi cha tatu na kufikia wakia 112,523 kutoka wakia 67,738

Almasi toka Tanzania 2016 iliongezeka kwa asilimia  23 katika kota ya 3  na kufikia karati  53,034 kutoka karati 43,155  kutoka Williamson Diamonds Mine.

Gredi ya Juu ya Grafaita imegunduliwa huko Mahenge na Kampuni ya Afrika Kusini ya Armadale Capital kwenye eneo la Liandu Graphite

Kwa ujumla sekta ya madini Tanzania  iliongezeka kwa kiasi cha asilimia 20.5 katika kota ya 2 mwaka huu na kufikia shilingi bilioni 434 ukifananisha na shilingi bilioni 361 mwaka uliopita na kuongezeka kwa asilimia 6.5.

Grafaita iliyochimbwa Tanzania eneo la Epanko imethibitishwa kuwa una ubora wa hali ya juu sana na Kampuni ya Kiaustralia Kibaran Resources inayochimba huko Mahenge. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Stephen Kebwe, alisema amefurahia taarifa hiyo na kuwaomba wahusika wajenge kiwanda cha betri mkoani humo ili kutumia malighafi hiyo.

Ripoti nyingine inasema ukubwa wa hazina hiyo kutokana na utafiti wa kampuni ya Black, imeongezeka kwa asilimia 25 na kufikia tani milioni 203.

Wizara ya Nishati na Madini imetoa leseni ya uchimbaji ya miaka kumi kwa kampuni ya Australia ya Graphex Mining kwa ajili ya Chilalo Graphite Project kule Rwanga Mkoa wa Lindi.

Ni ushahidi tosha kuwa suala la madini ni rasilimali tosha ya kutuletea maendeleo kama tutakuwa makini kwenye matumizi yake kwa wakati mwafaka. Kila kitu kipo kinachotakiwa sasa ni oganaizesheni ya mambo.

Grafaita  inahitajika sana ulimwenguni kutengeneza betri za simu na zile za magari ya umeme ambapo mahitaji yake yanapanda kila siku.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles