Sekta binafsi yalalamikia matamko ya serikali yanavyokwamisha uwekezaji nchini

0
499

Mwandishi Wetu, Morogoro

Wadau wa sekta binafsi nchini wamesema Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) bado una changamoto nyingi za kibiashara ikiwamo matamko yanayozuia usafirishaji wa mazao nje ya nchi.

Wakizungumza wakati wa warsha ya kujadili ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa ASDP II iliyoandaliwa na Baraza la Kilimo Tanzania mkoani Morogoro, wamesema ni muhimu mpango huo ukawa jumuishi si tu kwenye makaratasi bali kwenye utendaji.

Akizungumza katika warsha hiyo, Joseph Masimba kutoka kampuni ya Sugeco, amesema katika maamuzi ya kila siku ya kisera sekta binafsi iweze kushirikishwa vema zaidi katika mpango huo.

“Tumekuwa tukiathiriwa sana na  matamko mengi hasa ya ufungaji wa mipaka, mfano Sumri alikuwa na tani 5,000  za mahindi ghafla likatoka tamko la kuzui kuuza nje, unaweza kuona namna tamko la mtu mmoja linavyoathiri, unakuta mtu mmoja anatoa tamko ambalo athari yake ni kubwa sana kiuchumi kwa mtu mmoja na jamii nzima.

“Lakini pia unakuta mtu ana mkataba wake wa kuuza mazao nje ya nchi katafuta wakulima amewapa mbolea, mbegu mwisho wa siku mavuno yanakomaa na muda huo huo unakutana na tamko,” amesema.

Kwa upande wake mfanyabiashara wa bidhaa kusindika za mchele na mahindi, Sifa Gerana amesema changamoto ni nyingi hasa ya mazuio ya usafirishaji wa mazao nje ya nchi ambayo yanaathiri sana biashara zao.

“Sisi tunategemea masoko ya nje sasa unapozuiwa unajikuta unabaki na mzigo mkubwa sana ambao soko la ndani haliwezi kuumudu mzigo ulipo, lakini pia ni muhimu tuwe tunashirikishwa kama sekta binafsi,” amesema.

Naye Mtafiti Mshauri aliyefanya utafiti kuhusu changamoto zinazoikabili sekta binafsi kushindwa kushiriki kikamilifu katika ASDP II, Apromius Mbilinyi amesema ni wakati mwafaka kwa sekta binafsi kuanza kuwekeza katika Sekta ya Kilimo kwani kuna fursa nyingi hasa katika uongezaji wa thamani.

“Asilimia 70 ya mbegu zinaagizwa nchi ya nje, hii ni fursa kwa sekta binafsi kuwekeza lakini pia lazima wajitokeze kuwekeza katika ujenzi wa maghala ya kuhifadhia chakula kwa sababu asilimia 30 ya mazao nchini yanaharibika baada ya kuvunwa kwa hivyo ni muhimu Sekta binafsi ikazitazama fursa hizi pia,” amesema.

Kwa upande wake Ofisa Sera Mwandamizi kutoka Baraza la Kilimo Tanzania ambao ndiyo waandaaji wa mkutano huo, Laetitia William amesema waliamua kufanya utafiti huo baada ya kuona wadau wengi wa sekta binafsi wakiwa na ukakasi katika kushiriki katika utekelezaji wa mpango huo ambapo sekta binafsi inatarajiwa kutoa asilimia 59 huku serikali ikitoa asilimia 41 katika kukamilisha mpango huo.

“Ni kweli ndani ya ASDP II kuna fursa nyingi sana, ila kuna vikwazo vya kisheria na kikanuni ambavyo vinaleta changamoto kidogo kiutekelezaji hasa kwa sekta binafsi , lakini sisi kama Baraza baada ya mkutano huu tutaandika andiko letu la kisera ilikuweza kuishauri serikali ili iweze kufanyia kazi changamoto hizo kwani tumekuwa tukifanya hivyo na serikali imekuwa ikifanyia kazi,” amesema Laetitia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here