22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 18, 2021

SEKTA BINAFSI INAHITAJI KULELEWA VIZURI

Na LEONARD MANG'OHA


SEKTA binafsi ni nguzo muhimu katika ukuaji wa uchumi katika Taifa lolote duniani kutokana na ushiriki na mchango wake mkubwa katika utoaji huduma, uzalishaji mali  na hata ajira.

Kwa kuelewa hilo, wataalamu na Serikali huiita sekta hiyo kuwa ni injini ya kukuza uchumi.

Kwa kawaida Serikali ndiyo yenye jukumu la kuhakikisha wananchi wanapata huduma zote za msingi kama vile elimu, huduma bora za afya, maji nishati, mawasiliano na miundombinu. Kwa kifupi Serikali huweka mazingira mazuri ya kufanikisha uwekezaji wa sekta binafsi.

Lakini kutokana na kuongezeka kwa uhitaji katika jamii kunakochagizwa na ongezeko la watu, Serikali hulazimika kushirikiana na sekta binafsi kusaidia utoaji wa huduma hizo katika maeneo yenye mahitaji zaidi au pemebezoni mwa nchi amabapo watu  binafsi hushindwa kutokana na kukosekana kwa faida ya kiuchumi kwao.

Mfumo huu haupo Tanzania pekee bali hata katika mataifa yote yale yanayoendelea na yaliyoendelea ambapo sekta binafsi imekuwa chachu ya maendeleo katika mataifa hayo.

Kwa mfano katika nchi ya Marekani, sekta binafsi ndiyo imekuwa kinara wa kuzalisha nishati ya kuendeshea viwanda na maeneo yote yenye mahitaji makubwa ya huduma hiyo.

Kwa mantiki hiyo ni wazi kuwa sekta hiyo haiwezi kuepukika katika Taifa kama Tanzania linalojaribu kuanza safari kuelekea uchumi wa viwanda na kwa kuzingatia kuwa upatikanaji wa huduma nyingi bado ni kizungumkuti.

Sekta hii imekuwa msaada mkubwa katika elimu ambako tumeshuhudia shule binafsi  zikishamiri na kufanya vema katika mitihani mbalimbali ya kitaifa zikilinganishwa na zile za umma. Ni faraja kuona ushirikiano huo ukinawiri.

Imesaidia vilevile kutoa huduma za kuaminika za afya katika ngazi zote kuanzia hospitali za chini hadi za rufaa kama Bugando, KCMC na nyinginezo.

Licha ya sekta hii kuwa muhimu katika utoaji huduma na ukuaji wa uchumi wa nchi, kwa siku za karibuni kumekuwapo na taarifa zinazoelezea kuzorota kwa uendeshaji wa sekta hiyo, hali inayosababisha biashara nyingi kuendeshwa kwa hasara na hata nyingine kufungwa.

Kinachotajwa na wengi ni mazingira magumu ya kufanya biashara, ushirikiano mdogo kutoka sserikalini na mfumuko wa bei na kuporomoka kwa sarafu ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani. Nini ukweli wa suala hili?

Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya, anasema kwa sasa wafanyabiashara hususani wa ndani wanapungua kutokana na Serikali kushindwa kutoa ushirikiano wa kina kwa sekta hiyo ambayo inapaswa kuwa mwajiri mkuu.

Anasema hali hiyo imekuja ghafla kutokana na mtazamo kuwa fedha za umma zimekuwa zikielekezwa kwa wajanja wachache, dhana iliyosababisha Serikali kuanzisha juhudi za makusudi za kutojihusisha na sekta hiyo.

Anasema madhara ya kusitisha mikutano ya idara za Serikali katika kumbi za watu binafsi imefifisha biashara ya hoteli ambazo zilitegemea mikutano hiyo kama moja ya vyanzo vyake vya mapato.

Kuelekezwa kwa fedha zote za umma Benki Kuu (BoT), mishahara na miamala mbalimbali kufanyika kupitia NMB pekee ambako Serikali ina hisa,  ni pigo kwa benki binafsi zilizotegemea fedha hizo kujiendesha ambapo kupitia ukopeshaji zingeweza kulipa kodi kwa Serikali.

"Hii inasababisha biashara kufungwa au waajiri kuamua kupunguza wafanyakazi, lakini pia PPP inapaswa kuzingatiwa na Serikali ijali mikataba baina yake na sekta binafsi," anasema Nyamhokya.

Anasema pia Serikali imekuwa chanzo cha sekta binafsi kuyumba kutokana na kuwakopa sana kwenye fani mbalimbali na kushindwa kulipa madeni hayo kwa wakati  na hivyo kuvuruga mwenendo wa fedha yao. Alitolea mfano wa makandarasi ambao wamekuwa wakitekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu nchini kutolipwa ipasavyo.

Anasema kutokana na hali hii, tatizo la ukosefu wa ajira limeendelea kuwa kubwa na linaongezeka kwani hata wale waliokuwa katika ajira wameachishwa kazi kutokana na kuyumba kwa biashara kukosa mtiriko sahihi wa fedha zake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye, anasema mzunguko wa fedha  umebinywa na umekuwa mdogo kiasi cha kutowafikia wafanyabiashara wengi. Serikali imepunguza matumizi mengi ili ijitegemee, kinyume na matarajio ya wengi.

Anasema hali imesababisha baadhi ya viwanda vikubwa kama TBL kupunguza uzalishaji kwa karibu asilimia 30 na imeathiri hadi wafanyabiashara wa kati na wadogo.

Anasema mzunguko hafifu wa fedha umesababishwa zaidi na kuondolewa kwa fedha  zilizopatikana kwa njia ya haramu ya uramali, hivyo biashara zinazoendeshwa kwa njia halali pekee ndizo zitakazoweza kusimama imara wakati huu.

Anasema kuongezeka kwa ukusanyaji kodi kunakofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni miongoni mwa mambo yanayosababisha biashara nyingi kutetereka kutokana na wafanyabiashara wengi kuendesha biashara kwa kukwepa kodi, hivyo baada ya kubanwa kulipa madeni yao wamekuwa katika wakati mgumu wengi wakilazimika kufunga biashara.

Anasema anashindwa kuelewa nia ya Serikali kwa sasa ni kurejea kwenye ujamaa au kuendelea na mfumo wa ubepari kutokana na ushirikiano mdogo kutoka serikalini. Tubadilike.

Simbeye anadai kuwa jina lao kama sekta binafsi limeharibiwa kutokana na kuonekena kuwa ni ‘wapiga dili’, jambo linalosababisha rais kuamua kuelekeza shughuli zote za maendeleo kufanywa na taasisi za umma.

"Utaona kwa sasa miradi mingi ya ujenzi inafanywa  na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Shirika la Nyumba la Taifa na Shirika la Maendeleo la Jeshi la kujenga Taifa (SumaJKT).

"Hata alipotembelea ujenzi wa uwanja wa ndege Terminal III, alishangaa gharama zilizotumika kujenga anaona kila mradi wanaojenga sekta binafsi wanapiga dili, hivyo haamini kama sekta hiyo inaweza kutekeleza miradi mikubwa bila ‘kupiga dili,” anasema Simbeye.

Anasema tatizo la upigaji dili si la sekta binafsi pekee, bali hufanywa na watumushi wa Serikali wasio waaminifu kwani hakuna mfanyabiashara anayekwenda kujipa mkataba wa kujinufaisha.

Anasema pamoja na juhudi za dhati anazozichukua rais kupambana na wapiga dili, bado hajaweza kudhibiti mianya ya rushwa hususani katika ngazi ya halmashauri ambako anasema urasimu umekithiri katika utoaji zabuni mbalimbali.

Anasema kuelekezwa kwa fedha nyingi katika miradi ya maendeleo kumeathiri mzunguko wa fedha kutokana na miradi mingi kutekelezwa na kampuni za kigeni zenye uwezo  na kusababisha kupungua kwa fedha katika mzunguko wa kawaida.

Kuondolewa kwa fedha za umma zaidi ya Sh bilioni 600 katika benki binafsi zimeathiri mfumo wa biashara katika sekta hiyo ambayo ni ndogo ukilinganisha na Kenya ambayo kiasi kama hicho kikiondolewa haiwezi kutetereka kwa sababu tayari iko imara, kwani kama nchi haikuwahi kupita katika mfumo wa ujamaa tangu uhuru.

Anasema hata katika sakata la usafirishaji mchanga wa dhahabu nje ya nchi, taasisi husika zilipaswa kufanya utafiti wa kina kwani minong'ono ya urasimu katika eneo hili imekuwapo kwa muda mrefu.

Anasema wameamua kufanya utafiti kubaini nini sababu hasa ya kuyumba kwa biashara nyingi ili kubaini kama kweli upigaji dili ndiyo  chanzo. 

Anaamini rais anapaswa kusaidia viwanda vilivyopo kuhakikisha vinaimarika na kuzalisha ajira za kutosha, ikiwa atashindwa kuhakikisha viwanda hivyo vinazalisha kama inavyostahili asitegemee kupata mafanikio ya viwanda.

Anasema watakapopata nafasi ya kukutana na rais watamweleza hali halisi ya biashara na athari wanazokumbana nazo kutokana na kukosa ushirikiano wa kutosha.

Hivyo basi, raisi anapaswa kuhakikisha mamlaka zote husika zilizo chini yake zinawajibika kuhakikisha sekta binafsi inaimarika na kushirikisha wafanyabiashara na wawekezaji wazawa zaidi ili kuimarisha pato la ndani.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,220FollowersFollow
521,000SubscribersSubscribe

Latest Articles