23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

SEKONDARI OMUMWANI ZAO LA USHIRIKA LILILOVURUGWA NA SIASA

Na Deogratias Kishombo, BUKOBA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mkuu wa mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu wakitoka kwenye ukaguzi wa shule ya Sekondari Omumwani mkoani Kagera.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mkuu wa mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu wakitoka kwenye ukaguzi wa shule ya Sekondari Omumwani mkoani Kagera.

OMUMWANI kwa lugha ya wenyeji wa Mkoa wa Kagera maana yake ni “mti wa mbuni au mkahawa”. Jina hili kwa ajili ya shule hii lilitokana na juhudi za wakulima wa kahawa (Wahaya) ambao walijitolea kuiunga mkono serikali ya awamu ya kwanza chini ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Sekondari ya Omumwani kwa mujibu wa takwimu za shule za awali za sekondari zilizoanzishwa kwa nguvu za wananchi ndiyo ya kwanza kujengwa mwaka 1966 miaka mitano baada ya uhuru chini ya wanaushirika wa Kagera.

Ushirika katika Mkoa wa Kagera una historia ndefu. Hadi nchi hii inapata Uhuru, ushirika katika mkoa huu ulikuwa wenye nguvu kuliko maeneo mengi ya Tanzania Bara. Ushirika ulikuwa umeanza tangu katikati mwa miaka ya 1930 ambapo mwaka 1935 chama cha kwanza cha ushirika (Bugufi Coffee Cooperative Union) kilianzishwa katika Wilaya ya Ngara.

Mwaka 1939 chama kingine cha Ushirika cha Buhaya (BCU) kilianzishwa ambapo kilihudumia wilaya za Bukoba, Muleba, Karagwe na Biharamulo.

Chama hiki kilikua na hatimaye kusajiliwa kama chama kikuu cha ushirika cha Bukoba (Native Coffee Cooperative Union (BNCU Ltd)) katika Mwaka 1960 BNCU na vyama vya ushirika vya msingi 74 vilinunua kiwanda cha kukoboa Kahawa cha BUKOP kutoka kwa Kampuni ya BCCCO Ltd iliyokuwa inamilikiwa na wafanyabiashara wa Kihindi.

 

Mara baada ya uhuru kulikuwa na ongezeko kubwa la vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS) katika maeneo ya Ibwera, Izigo, Bugandika, Itawa, Kanyigo na Kamachumu. Ongezeko la vyama hivi vya kuweka na kukopa lilitokana pia na uhamasishaji wa Mhashamu Kardinali Laurian Rugambwa, alioufanya mara baada ya kurudi nchini kutoka Canada mwaka 1961.

Kiujumla wakati wa Uhuru mkoa ulikuwa na jumla ya vyama vya ushirika 89 na chama kikuu kimoja cha BNCU Ltd.

Mwaka mmoja baada ya Uhuru, yaani mwaka 1962, chama kingine cha usambazaji cha ushirika-Tanganyika (COSATA) kilianzishwa ambacho kilikuwa ndiyo muuzaji mkuu na msambazaji wa bidhaa kwa wanachama wake na wananchi kwa jumla.

Kutungwa kwa sheria ya kwanza ya vyama vya ushirika mwaka 1968 kuliimarisha zaidi harakati za ushirika katika mkoa huu ambapo pamoja na matukio mengine ya kukua kwa ushirika kiwanda cha Kahawa cha TANICA kilianza uzalishaji.

Kama ilivyokuwa kwa vyama vingine vya ushirika katika Tanzania Bara, vyama vya ushirika vya mkoa wa Kagera vilivunjwa na Serikali mwaka 976 ambapo wakulima wa kahawa, pamba na mazao mengine ya biashara walihudumiwa na bodi za mazao ambazo zilianzishwa kwa ajili ya kuchukua nafasi ya vyama vya ushirika.

Hata hivyo miaka miwili baadae, mwaka 1978 jumuiya ya wanaushirika nchini (UCS) ilianzishwa na mwaka 1979 washirika (UCS) walitambuliwa kama Jumuiya ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Taarifa zinaonyesha ni miaka hiyo hiyo Omumwani ilikuwa chini ya Jumuiya ya wazazi. Omumwani iliwahi kuwa na idadi ya wanafunzi 1000 hivyo kuzidisha uwezo wake kwa mwaka ambao ni wanafunzi 520 wa kutwa na bweni.

Inasemekana kwamba Omumwani ilikuwa ikipokea wanafunzi kutoka pembe zote za Tanzania waliofika pale kusaka elimu ya wakati huo lakini taarifa zinadokeza kwamba pamoja na kuwa na miundombinu bora bado ufaulu wake kwa wanafunzi ulikuwa ni wa wastani.

“Ni shule ya kwanza ya wazazi na ninasikia huko nyuma ilikuwa inafanya vizuri zaidi na ilikuwa inapokea wanafunzi wengi sana” anasema Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Godfrey Nestory.

Nestory anasema kwamba baada ya biashara huria kuingia nchini na watu wakaanza kuwekeza kwenye elimu hapo ndipo wanafunzi walipoanza kupungua kutokana na ushindani wa shule binafsi.

“Unajua kipindi cha nyuma shule hazikuwapo nyingi za sekondari lakini watu walipowekeza kwenye elimu na shule zikaongezeka wanafunzi walianza kuondoka taratibu na kupungua lakini kipindi ambacho nimekuwa Mkuu wa shule yetu suala la kuondoka wanafunzi tumelithibiti hakuna mwanafunzi yeyote ambaye ameondoka hapa tangu 2015 na shule yetu ufaulu ni wa wastani,” anasema

Aidha, taarifa kutoka ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Kagera, mmoja wa viongozi waandamizi ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini anasema kwamba sekondari ya Omumwani imekuwa ikikabiliwa na changamoto lukuki lakini kubwa ni mtivuano wa viongozi wa CCM ngazi ya mkoa huo

“Naweza kusema kwamba tatizo kubwa linaloikumba shule yetu inatokana na migogoro kwenye chama chetu. Mivutano, malumbano, magomvi inasababisha hasa walimu wetu kukata tama” anasema

Anasema kumekuwapo maelekezo tofauti au ya kuchanganya kutoka viongozi wa CCM kwenda kwa bodi na menejimenti ya shule hiyo

“Unakuta Katibu wa Wilaya anaelekeza hiki, mwenyekiti kile na wakati mwingine hata wabunge wa CCM kuna baadhi walikuwa wanaelekeza vinginevyo siku za nyuma” anasema

Kabla ya Raisi John Magufuli hajaibadilisha shule hiyo kuwa ya serikali ilkuwa na wanafunzi 85 tu kati ya idadi inayotakiwa ya wanafunzi 520. Omumwani ndiyo shule pekee iliyopokea wanafunzi wengi kutoka shule mbili za Ihungo na Nyakato ambazo ziliharibiwa na tetemeko

Kwa sasa wanafunzi hawa wanasoma pale Omumwani na menejimenti za shule hizo mbili zinafanyia shughuli zake hapo. Kwa sasa kuna menejimenti tatu ambazo ni menejimenti ya Omumwani, Ihungo na Nyakato. Ila kinachofurahisha wanafunzi 85 wa Omumwani waliokuwepo kwa sasa hivi wametawanywa katika shule za kata ya shule za Maruku, Nshambya na Rugambwa ili kupisha kaka zao wa kidato cha tano na sita kutoka Ihungo na Nyakato.

Mathalani, shule ya Omumwani pamoja na kuwa ni kongwe haina watu wengi maarufu waliosoma pale. Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya Mwalimu Mkuu taarifa za watu wengi waliopita pale hazipo. Aidha, mwandishi wa makala haya amekuatana na majina ya Wilson Masilingi aliyekuwa Mbunge wa Muleba na Abdalah Bulembo mwenyekiti wa wazazi (CCM Taifa) wamesoma shuleni hapo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles