Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na Sera Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama (Mb) Peramiho amesema Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI itajenga vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Msingi Muungano iliyopo Halmashauri ya Songea.
“Tunataka kufanya ukarabati Madarasa na kujenga mengine ili shule ya Msingi Muungano iwe miongoni mwa shule za mfano kwa kuwa na Miundo Mbinu Bora ya Elimu,” amesema Mhagama.
Kauli hiyo ameitoa Julai 9, mwaka huu katika Kijiji cha Namatuhi Kata ya Ndongosi Halmashauri ya wilaya ya Songea wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa vinavyomaliziwa kujengwa.
Waziri Mhagama, ameelekeza watendaji wa Halmashauri ya wilaya kuhakikisha hatua ya umaliziwaji wa ujenzi wa vyumba hivyo viwili vya madarasa uwe imekamilika ndani kipindi cha wiki mbili.
Akizungumzia kuhusu uharibifu wa Misitu na vyanzo vya maji Waziri Mhagama amewaomba wananchi wa kijiji cha Namatuhi kuendelea kuhifadhi mazingira na kuepuka tabia ya ukataji wa miti.
Amesema chanzo cha maji cha Kitinginyi ndio chanzo pekee kilichobaki, kinapaswa kulindwa ili kuepusha shughuli nyingine za kibinadamu zinazoweza kuharibu chanzo hicho cha maji.
“Tuendelee kutunza chanzo hicho cha maji kwa kupanda miti ili huduma ya maji iweze kunufaisha vijiji vingine vya jirani,” alisema Waziri Mhagama.
Kwa upande wake Mkugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Mwalimu Neema Magembe amesema gharama za ujenzi wa Vyumba Viwili vya Madarasa mpaka ujenzi ulipofikia ni Sh millioni 34.
Ameongeza kusema, halmashauri tayari imeshaweka fedha za umaliziaji wa vyumba hivyo madarasa kwa kuweka Marumaru.
Awali Diwani wa Kata ya Ndongosi, Zakaria Mbilinyi amemshukuru Waziri Mhagama kwa kutuma Mhandisi wa maji ambaye alifanya utafiti na kugundua chanzo cha maji katika kitongoji cha Muungano kilichopo katika Kijiji cha Namatuhi kata ya Ndongosi.
“Wananchi wanamatumaini Makubwa, kwamba watapata huduma ya maji safi na salama alisema,” Mbilinyi.