22.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

Sefue: Serikali inapita katika kipindi kigumu

Ombeni-SefueNa Jonas Mushi, Dar es Salaam

KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amesema Serikali inapitia kipindi kigumu kutokana na mfululizo wa vifo vya mawaziri wake.

Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana baada ya kuupokea mwili wa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda uliowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 9.00 alasiri kwa ndege ya Emirates kutoka New Delhi   India.

Alikuwa ameongozana na viongozi wengine akiwamo Spika wa Bunge, Anne Makinda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Janeth Mbene na Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli.

“Huu ni msiba mkubwa sana na Serikali inapita katika kipindi kigumu ukizingatia ni hivi karibuni tulimpoteza Celina Kombani (aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma) na sasa tumempoteza waziri mwingine, msiba huu nao umetushitua sana,” alisema Sefue.

Alisema msiba huo ni pigo kubwa kwa sababu Dk. Kigoda amekuwa waziri  kwa muda mrefu na kifo chake kimeleta pengo katika utumishi.

Akimzungumzia Dk. Kigoda, Dk. Magufuli, alisema anamfahamu kama waziri mwenzake na rafiki yake.

Dk. Magufuli alisema tukio analolikumbuka kwa Dk. Kigoda ni siku aliyompigia simu kabla hajapelekwa chumba cha wagonjwa wenye uangalizi maalumu (ICU) na kumshauri kuhusu wafanyabiashara wa ndani.

“Aliniambia niwakumbuke na kuwawezesha wafanyabiashara wa ndani waweze kukua na kuwa wawekezaji wakubwa wa ndani, hayo ndiyo yalikuwa maneno ya mwisho kuyasikia kutoka kwa Dk. Kigoda,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema kilichomshangaza na kumfanya amkumbuke zaidi ni kitendo cha kutoka hospitali kwa siku moja na kuhudhuria kampeni zake   Handeni Mjini   alikomkabidhi ilani ya chama.

“Akiwa hospitalini hajazidiwa sana alisikia ninakwenda jimboni kwake kufanya kampeni akatoka kwa siku ile moja akaja kuniunga mkono na nikamkabidhi ilani ya chama kesho yake akarudi hospitalini kwa matibabu,” alisema Dk. Magufuli.

Jana, mwili wa Dk. Kigoda ulipelekwa  katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo na utaagwa leo kuanzia saa 2.00 asubuhi katika Viwanja vya Karimjee na viongozi mbalimbali wa Serikali watahudhuria kuuaga.

Baada ya kuagwa, mwili utasafirishwa   kwenda nyumbani kwake Handeni, Tanga kwa maziko ambako unatarajiwa kuwasili saa 7.00 mchana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles