30.4 C
Dar es Salaam
Saturday, December 2, 2023

Contact us: [email protected]

SCHIZOPHRENIA: UGONJWA WA AKILI UNAOTESA WENGI BILA KUJIJUA


Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

SCHIZOPHRENIA ni miongoni mwa magonjwa makubwa ya akili. Jina hilo limetoholewa kutoka katika lugha ya Kilatini ambayo ni maneno mawili – Schizo na Phrenia.

Tafsiri rahisi kwa Kiswahili humaanisha akili iliyogawanyika au iliyotawanyika, yaani huwa haziendi sawa sawa… huwa hakuna muunganiko kati ya mtu na akili yake.

Yapo magonjwa mengi ya akili ambayo kati yake yapo yanayohusisha kuchanganyikiwa akili kama huu wa Schizophrenia.

Akizungumza na MTANZANIA Daktari Bingwa wa Afya na Magonjwa ya Akili wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Said Kuganda anafafanua vema kuhusu ugonjwa huu.

“Huwa haziendi sawa sawa, yaani hakuna muunganiko kati ya mtu na akili yake, kuna magonjwa mengi ya akili ambayo kati yake yapo yanayohusisha kuchanganyikiwa akili kama huu wa Schizophrenia.

“Lakini pia yapo ambayo hayahusishi kuchanganyikiwa akili, watu wengi wanaugua magonjwa ya akili lakini huwa hawachanganyikiwi isipokuwa wapo wachache ambao wakiugua huchanganyikiwa,” anabainisha.

Dk. Kuganda anasema wale ambao huchanganyikiwa nao kuna kipindi katika maisha yao huwa wanakaa sawa na kuna kipindi huonesha ile hali ya kuchanganyikiwa. 

Kuchanganyikiwa akili

Anafafanua: “Kuna maeneo matano ambayo ni muhimu katika mwili wa binadamu, yanayoashiria akili kuchanganyikiwa.

“Eneo la kwanza ni kuwa na imani ambayo si halisi (potofu) iliyopitiliza katika ule uhalisia wake wa kawaida,” anasema.

 Utajuaje?

Daktari huyo anasema ili kubaini jambo hilo ni lazima mgonjwa apimwe katika nyenzo zote muhimu zinazohitajika.

“Kwa mfano, mila na desturi zake, tunaangalia kwao wanaamini nini kuhusu hicho anachokiamini, elimu yake inamweleza nini kuhusu kitu anachokiamini na je, dini yake inaeleza nini  kuhusu jambo analoliamini.

“Wakati mwingine unakuta ana imani sahihi lakini huenda imepitiliza, sasa kujua iwapo imepitiliza kile kiwango au la lazima tulete vigezo muhimu na tujadiliane pamoja naye ili kujiridhisha.

“Tukibaini kuna ambavyo ameviruka tunamuuliza sababu ya kuviruka na kuangalia vigezo vingine kwa mfano, mtu anaweza kusema yeye ni Mungu kwamba hiyo ndiyo imani yake na anashughulikia viumbe vyote.

“Inabidi muhojiane naye katika upande huo huo wa kuzungumzia Mungu na uwezo wake tofauti na Mungu ambaye wengine wote tunamfahamu,” anasema.

Anasema huwa wanapima imani ya mgonjwa, wakiona hana uwezo wa kurudi nyuma katika kile anachokiamini na historia yake ipo tofauti na anachozungumza basi hugundua amechanganyikiwa.

“Matokeo ya mgonjwa wa aina hii ni kwamba mambo yake huwa hayafanikiwi kwa sababu anakuwa anaendeshwa na imani potofu aliyonayo,” anabainisha.

Daktari huyo anasema yapo mambo mengine ambayo yanadhihirisha kuwa fulani ana tatizo la Schizophrenia.

Anatoa mfano wa watu ambao huwa na hisia kwamba nje ya nyumba yake kuna watu wanamsubiri wakiwa wamebeba silaha wakitaka kumdhuru.

Anasema mtu huyo anaweza kulalamika kabisa akidai kuna watu wanamfuatilia wamdhuru, lakini ukifuatilia kwa kina hata kwa kukaa nje ya nyumba yake huwaoni watu hao, lakini yeye atang’ang’ania kwamba wapo.

Dk. Kuganda anasema hali hiyo huweza kumsababishia muhusika kuogopa kabisa kutoka nje ya nyumba yake akiamini kuna maadui wanamsubiri.

Daktari Bingwa wa Afya na Magonjwa ya Akili wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Said Kuganda

 

“Kwa mtu anayefanya kazi hali hiyo inaweza kuathiri utendaji wake wa kazi, anaweza kuamua asiende kazini, akafukuzwa kazi bila ofisi kujua kama ana tatizo la akili.

Anasema eneo jingine linaloashiria akili kuchanganyikiwa ni kuwa na hisia potofu tofauti na zile za kawaida anazokuwa nazo binadamu.

Anasema kwa kawaida binadamu huwa na hisia tano muhimu, ambazo ni za kuona, kugusa, kuonja, kusikia na kunusa.

Anasema mtu aliyechanganyikiwa anaweza kuona, kuhisi, kunusa, kugusa au kusikia vitu ambavyo wengine hawaoni, kuhisi wala kusikia.

Anatoa mfano: “Mhusika anaweza kusema anaona nyoka anapita eneo ambalo mmekaa naye, lakini nyie msimuone au anasikia sauti na watu wanazungumza habari zake, wanamshurutisha au wanamtisha lakini nyie hamuoni wala hamsikii chochote.

 

“Wakati mwingine anaweza kudai anasikia sauti yake mwenyewe, kwamba yale anayowaza na kutafakari anasikia yakizungumzwa redioni.

“Wakati mwingine anaweza kuhisi kuna vitu vinatambaa mwilini mwake (hii ni hisia ya kugusa)  lakini kila anacholalamika kwamba kinamsumbua unakuta nyie wengine hamkioni ila yeye kinakuwa kweli kinamsumbua na mambo yake yanakuwa hayaendi sawa sawa,” anasema.

Anasema wakati mwingine mnaweza kula naye chakula aina moja, lakini yeye akalalamika kupata ladha tofauti na ile mnayoipata nyie.

Anaongeza: “Anaweza hata akadai chakula chake kimetiwa sumu lakini si kweli, au wakati mwingine akanusa harufu ambazo hazipo.”

Anasema ingawa hayo wakati mwingine huwa ni mambo ya kawaida, yakipitiliza huashiria kuwapo kwa tatizo hasa la kuchanganyikiwa kwa muhusika.

Anasema hali hiyo husababisha tabia na mienendo ya muhusika kubadilika.

“Mnaweza kumbaini pia kwa maneno yake, anaweza kuzungumza vitu vingi ambavyo havina uhusiano na kile alichokizungumza mwanzo.

“Kwa mfano, anaweza kuanza kusimulia amezaliwa lini, kisha hapo hapo akahamia stori nyingine labda kuhusu mambo ya barabarani kisha akaunganisha na mambo ya Marekani.

“Tunasema anazungumza ovyo, ambako ni dalili ya kuchanganyikiwa hata kama hajawaambia kama anaumwa,” anasema. 

Kumtambua kwa matendo

Dk. Said anasema kuna mgonjwa mwingine unaweza kumtambua kwa urahisi kutokana na matendo yake.

“Kuna kuchanganyikiwa kwa matendo yake kwa mfano, wale wanaotembea barabarani utaona wanaanza kubeba mizigo mikubwa, wanavaa nguo zaidi ya moja wakati mwingine hadi nane, hiyo huashiria kwamba kile kiwango cha kuchanganyikiwa kimekuwa kikubwa zaidi.

“Yaani hata kama hujaambiwa kitu, ukimtazama tu unajua kwamba mtu huyo amechanganyikiwa.

“Wakati mwingine wagonjwa wa aina hii hupenda kujitenga na jamii, hujitengenezea ulimwengu wa peke yao. Unakuta mtu anatabasamu mwenyewe, anazungumza mwenyewe na mambo mengine kama hayo.

“Huwa hawahitaji kuingiliwa au kuwaingilia wengine, ndiyo maana hujitenga, hivyo ni viashiria vya kuchanganyikiwa,” anasema.

Anasema mgonjwa huweza kuonesha mambo mawili au matatu na wakati mwingine yote kati ya hayo aliyoeleza hapo juu.

Anasema huu ni ugonjwa ambao dalili zake huanza kuonekana kuanzia miezi sita tangu mhusika aupate, lakini wakati mwingine unaweza kuibuka ghafla. 

Idadi ya wanaougua

Anasema kuwa kati ya magonjwa yote ya akili yanayofahamika, huu ni ugonjwa ambao katika kundi kubwa la watu, chini ya asilimia moja huugua.

Anasema kiwango cha kuathirika kipo sawa kwa jinsi zote (wanaume na wanawake) lakini kuna vitu ambavyo huchangia mtu kuugua. 

Visababishi

Anasema ugonjwa huu mara nyingi hurithiwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

“Ikiwa katika kizazi chenu kuna mtu amewahi kuugua, basi kuna uwezekano wa mmoja wenu kurithi kwa sababu shida ipo katika akili,” anasema.

Anataja mambo mengine yanayochangia mtu kupata ni changamoto za kimaisha.

Kwamba, hali ya umaskini, kutokuwa na kazi na iwapo mtu aliwahi kupata majanga mbalimbali wakati wa makuzi yake huwa na uwezekano wa kuugua Schizophrenia.

Hata hivyo, anasema kuwa hivyo si visababishi vya moja kwa moja lakini mara nyingi humuweka mtu katika hatari ya kuugua.

 Wenye akili nyingi hatarini

Yapo madai kwamba baadhi ya watu huzaliwa wakiwa na akili nyingi kuliko wengine, hivyo hali hiyo husababisha wachanganyikiwe.

Dk. Kuganda anafafanua madai hayo kwa kusema: “Si kweli, hakuna uhusiano wowote kati ya mtu kuzaliwa akiwa na akili nyingi na kuchanganyikiwa.

“Isipokuwa kuna ugonjwa mwingine ambao si Schizophrenia, ambao mtu akiugua akili zake huwa zinafanya kazi vizuri, lakini akipona hurejea katika hali yake ya kawaida.

“Schizophrenia hauhusiani kabisa na akili ya mtu, kwamba aliyesoma kupita kiasi anaweza kuugua ugonjwa huu na wale wasiosoma huwa hatarini.

“Usiposoma kabisa maana yake hujaelimika, hapo vitu vingi hujipanga na vingi huwa ni changamoto hali inayosababisha akili kuwa na uwezekano mkubwa wa kulipuka.

“Tunasema kuchanganyikiwa ni mlipuko wa akili, hata wale waliopo barabarani jamii huwatenga bila kujua kwamba ile hali hujitokeza tu na wakipata matibabu sahihi wanaweza kurejea katika hali ya kawaida,” anasema.

Anasema lakini mgonjwa akichelewa kutibiwa anaweza aispone haraka kama atakapowahi kufika hospitalini.

 Jinsi ya kutibu

Anasema huwa wanatumia njia tatu kuwatibu wagonjwa wa akili ambazo ni za kibaiolojia, kisaikolojia na kijamii.

“Kibaiolojia huwa tunawapatia dawa za kuondoa dalili, lakini yapo ambayo huwa hayahitaji dawa bali mazungumzo maalumu (kisaikolojia) na matibabu ya kijamii.

“Huwa tunazungumza kitaalamu na mgonjwa juu ya namna ya kupunguza msongamano wa mawazo katika ubongo wake, ule msongamano ukipungua basi anaweza kutafakari vizuri na kufanya uamuzi sahihi.

“Kwa upande wa matibabu ya kijamii huwa tunakaa na kuzungumza na watu wanaomzunguka mgonjwa, hii ni kwa sababu unaweza kukuta shida haipo kwake bali kwa jamii inayomzunguika.

“Wakati mwingine matibabu huhitaji kufanya kazi, hapo huwa tunamtibu mgonjwa kitaalamu kwani si kila kazi anapaswa kufanya ili kutibu akili yake,” anasema na kuongeza:

“Kuna wakati huwa tunalazimika kuchanganya matibabu yote kwa wakati mmoja ili kupata matokeo mazuri zaidi.”

 Vijana hatarini

Anasema mara nyingi tatizo la Schizophrenia hutokea mtu anapokuwa katika hatua ya ujana hasa kuanzia miaka 18 hadi 25.

Anasema kwa sababu huo ndiyo umri wenye changamoto nyingi kuliko makundi mengine, kwamba mtu anaweza kurithi lakini mlipuko wa kwanza wa akili ukatokea akiwa na umri wa miaka 25.

Anasema sababu kubwa ni kwamba katika kipindi hicho mtu hukutana na changamoto nyingi za kimaisha kuliko kipindi kingine katika maisha yake. 

Uelewa duni

Daktari huyo anasema bado jamii haina uelewa wa kutosha kuhusu magonjwa hayo, hivyo hawampeleki mgonjwa hospitalini badala yake humfungia chumbani.

“Wengine huachwa wakirandaranda mitaani, wanawapeleka katika nyumba za ibada au hata kwa waganga wa kienyeji wakiamini kuwa wamerogwa.

“Wengi hufikishwa hospitalini miaka miwili hadi mitatu baadaye, wengine wakiletwa wanachukuliwa mapema kabla hawajapona na hivyo wanakwenda kuzidiwa wakiwa nyumbani,” anasema.

 Rai kwa jamii

Anaiasa jamii kuwawahisha wagonjwa wa aina hii hospitalini ili wapate tiba sahihi kwa kuwa magonjwa yote ya akili huwa yanatibika.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles