25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

SBL mkombozi wetu Kibaigwa

Mradi wa maji Kibaingwa
Mradi wa maji Kibaingwa

* Yajenga visima vya maji kuepuka adha hiyo

Na MWANDISHI WETU, KIBAIGWA 

MIONGONI mwa matatizo makubwa yanayowasumbua Watanzania leo ni tatizo la maji safi na salama. Kwa Kibaigwa tatizo hilo lilikuwa kubwa hasa wakati wa kiangazi. Kwa kutambua umuhimu wa maji katika maisha ya kila siku ya binadamu, Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) ilibuni na kuja na wazo la kusaidia kuchimba visima vya maji katika maeneo mbalimbali yenye shida hiyo.

Kampuni hii imekuwa ikichimba visima katika vijiji mbalimbali nchini na hivyo kufanikiwa kwa asilimia kubwa kuwakomboa wakazi wa Kibaigwa mkoani Dodoma.

Tafiti zinaonesha kuwa hata katika maeneo ya vijijini ambako  kuna maji, jamii inayoishi katika maeneo hayo hulazimika kutembea kilomita mbili hadi tatu kutafuta bidhaa hiyo ama kutoka kwenye mabomba ya umma au kwenye maeneo yaliyo na chemichemi na mito.

Miongoni mwa maeneo yaliyo na hali hiyo mwaka nenda mwaka rudi yakiwa yanataabika kwa uhaba wa maji ni Mkoa wa Dodoma. Mkoa huo ndio eneo ambalo SBL imeamua kutupia jicho katika mtazamo wa kampuni hiyo ya bia wa kuisaidia serikali  katika juhudi zake za kutoa mahitaji muhimu ya kijamii kwa wananchi wake.

Licha ya serikali kufanya  mabadiliko makubwa ya sera katika sekta ya maji mwaka 2002 upatikanaji wa maji na mazingira safi, mabadiliko hayo yamebakiwa kuwa ni madogo katika maeneo mengi.

SBL inafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa inachimba visima vya maji vijijini ikianza na  wakazi wa Kata ya Kibaigwa, Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.

Mradi huo wa maji kwa maisha unaofadhiliwa na SBL kwa gharama ya Sh milioni 82 unataraji kunufaisha zaidi ya wakazi 25,000 katika kata mbalimbali, ambapo kila kisima kilichochimbwa kina uwezo wa  kutoa lita 21 za maji kwa saa sita.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Meneja Miradi Endelevu wa SBL, Hawa Ladha, anasema lengo la SBL ni kufikia hatua ya kuchimba na kukabidhi visima hivyo na mkakati wa kampuni binafsi katika kuleta maendeleo hasa vijijini ili kuboresha huduma za maji safi.

Ladha anaeleza kuwa miradi kama hiyo ina lengo la kuboresha huduma za afya za wilaya na kupunguza vifo vya mama na watoto vitokanavyo na matumizi ya maji yasiyo safi na salama ili kupunguza kama si kuondoa kabisa magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu, kuhara, kuhara damu na homa ya matumbo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Bituni Msangi, anasema mradi huo ni faraja kubwa kwa wananchi wa Kibaigwa.

Anabainisha kuwa ni vizuri ili kuhakikisha kwamba visima hivyo na miundombinu vinalindwa kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Naye Meneja Mauzo wa SBL, Samuel Nyaki, anasema mradi huo utasaidia kurahisisha shughuli za uzalishaji hususani kwa akina mama.

“Visima hivi vitasaidia usambazaji na upatikanaji wa uhakika wa maji ya kutosha kwa wakazi na hivyo kupunguza muda na umbali mrefu ambao waathirika wakubwa ni akina mama na wanafunzi. Wa kike kupata muda zaidi wa kusoma,” anasisitiza Nyaki.

Mmoja wa wakazi Kibaigwa,  Faudhia Yusuph, alitumia fursa hiyo kuipongeza SBL kwa hatua hiyo yenye kuleta faraja kwao ambayo itawaepusha wakazi wa Kibaigwa na majanga mbalimbali ikiwamo vitendo vya ubakaji na mimba zisizotarajiwa kwa watoto wa kike ambao hivi sasa watapata maji katika maeneo ya karibu na haraka zaidi.

Naye Evarist Makeke, anasema sasa wataondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji itakuwa ni ndoto, hivyo anaishukuru SBL kwa kutambua thamani yao.

Kwa upande wake Maimuna Shabani, anasema tatizo la maji lilikuwa kubwa kiasi kwamba aliwahi kupigwa na mumewe kwa kosa la kuchelewa kurudi nyumbani akitokea kisimani.

“Niliwahi kupigwa na mume wangu kisa tu nilichelewa kurudi nyumbani nikitokea kisimani. Tulikuwa tunafuata maji umbali mrefu, kijiji cha tatu kutoka hapa.

“Ujio wa visima hivi utatusaidia pamoja na mambo mengine kuepuka vipigo kutoka kwa waume zetu,” anasema Maimuna.

Hii si mara ya kwanza kwa SBL kusaidia jamii katika sekta ya maji, mwaka 2014 SBL ilikabidhi mradi wa maji katika zahanati ya Mkamba iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam yenye uwezo wa kuzalisha lita 4,000 kila siku.

Miradi mingine ya maji ni ule wa Frelimo katika Hospitali ya Iringa, Hospitali ya Mawenzi mkoani Kilimanjaro, Sekou Toure – Mwanza, Hospitali ya Mletele Mkoa wa Ruvuma na Hospitali ya Temeke jijini Dar es Salaam. Miradi hiyo yote kwa pamoja imelenga kuhudumia zaidi ya watu 800,000.

Mradi mwingine wa maji unaofadhiliwa na SBL ni ule wa Hospitali ya Mkuranga  unaohudumia watu 250,000 ambao ulifunguliwa na Mama  Salma Kikwete.

Hali ilivyo

Mwaka 2014 Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) yalitoa ripoti iliyoonyesha tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama Tanzania.

Katika ripoti hiyo, ilionyesha jinsi ambavyo mtu mmoja kati ya watu sita nchini Tanzania hawapati maji safi na salama ya kunywa.

Moja ya mambo yanayosababisha hali hiyo kwa mujibu wa taarifa hiyo ni pamoja na ongezeko la watu, matumizi ya kiwango cha juu ya maji, mabadiliko ya tabianchi ambayo yamesababisha  kupungua kwa vyanzo vya maji  pamoja na  kuchunga mifugo mingi katika maeneo ya vyanzo vya maji katika maeneo ambayo shughuli zake za kiuchumi ni ufugaji.

Pengo lililo wazi  ambalo linatokana na uhaba wa maji ndilo ambalo Kampuni ya Bia ya Serengeti  Tanzania(SBL) inajaribu kuliziba kwa kuchimba na kukabidhi msaada wa visima  vya maji katika maeneo yenye uhaba huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles