NA MWANDISHI WETU
KWA muda mrefu wanawake nchini Saudi Arabia wamekuwa wakikatazwa kufanya mambo mbalimbali ikiwamo kuendesha magari.
Jambo hili lilikuwa likiwatatiza lakini hawakuwa na namna zaidi ya kufuata masharti yaliyowekwa na mamlaka.
Sasa hivi mambo yanaonekana kuanza kubadilika, ambapo yale yalikuwa yakikatazwa sasa yanaanza kuruusiwa kufanywa na wanawake.
Juni mwaka jana walianza kuruhusiwa kuanza kuendesha magari baada ya kupigania haki hiyo kwa miongo kadhaa.
Sheria na taratibu zinazoongozwa na wanaume zinaendelea kuathiri maisha yao ya kila siku.
Awali wanawake walikuwa hawaruhusiwi hata kuhudhuria mpira wa miguu uwanjani.
Hata hivyo, kutokana na mabadiliko kadhaa yaliyofanywa nchini humo, waliweza kuruhusiwa na kuwapa uhuru wanawake.
Miongongoni mwa mambo ambayo waliweza kufanya ni pamoja na kuhudhuria mchezo wa mpira wa miguu na kufanya kazi za jeshi na intelijensia na hata kushiriki mashindano ya baiskeli, shughuli ambazo awali ilikuwa ni marufuku.
Mambo ambayo wanawake walikatazwa kuyafanya
Kufungua akaunti benki bila mwanamume:
Wanawake nchini humo hawawezi kufungua akaunti benki bila ruhusa ya walezi au waangalizi wa kiume.
Mfumo huo umekuwa ukikosolewa vikali na watetezi wa haki za binadamu ambao wanasema wanawake wanashindwa kufanya uamuzi wenyewe.
Kupata pasi ya kusafiria au hata kusafiri nje ya nchi
Huu ni mfano mwingine wa mfumodume.
Wanawake wa Saudia wanalazimika kuwa na ridhaa ya kiongozi wa kiume mfano katika familia ili kupata pasi ya kusafiria au kuondoka nchini.
Mfumo huu pia umekuwa ukipewa nafasi kwenye maeneo mengine ya maisha ya wanawake mfano masomo, kazi na hata kwenye kupata baadhi ya huduma za kiafya.
Kiongozi anaweza kuwa baba wa mwanamke, kaka au ndugu wa kiume-kwa mwanamke mjane wakati mwingine mtoto wa kiume anaweza kuombwa ridhaa.
Kuolewa au kutalikiana
Ruhusa kutoka kwa kiongozi wa kiume inahitajika kwa ajili ya kuolewa au kutalikiana.
Ni vigumu kwa wanawake kuwapata watoto aliowazaa akiwa kwenye ndoa, kama watoto hao wanaumri wa zaidi ya miaka saba kwa watoto wa kiume na miaka tisa kwa watoto wa kike.
Walezi hao pia wako huru kukataa kutoa ridhaa kwa wanawake.
Wanawake wamekuwa wakilalamikia haki zao kukiukwa, wakilazimishwa kutoa mishahara yao kwa wanaume, wakizuiwa kuolewa au kulazimishwa kuolewa.
Kunywa kahawa na wanaume mgahawani
Migahawa yote inayowahudumia wanawake na wanaume hugawanyika katika sehemu mbili.
Hivyo, sehemu ya familia na watu wasio na familia (ambao huchukuliwa kuwa wanaume).
Wanawake wote wanapaswa kukaa sehemu ya familia.
Kuvaa unachotaka
Hadharani hauna haja ya kufunika uso, lakini unapaswa kuvaa kufunika kichwa hadi vidole vya miguu.
Vazi hili huitwa Abaya. Wanawake ambao hawafuati sheria hii huadhibiwa na viongozi wa kidini.
Ni kwenye maeneo machache ya maduka makubwa ambayo wanawake wanaweza kuvua Abaya.
Mwanzoni mwa mwaka jana, kiongozi wa kidini alisema: ”Wanawake hawana haja ya kuvaa Abaya”-kauli ambayo ilitabiriwa huenda ikawa msingi wa sheria za Saudi.
Wanawake wasio wa Saudi wanaweza kuwa huru. Kisheria wanaruhusiwa kuvaa mavazi ya kiliberali na kama si Waislamu, wanaruhusiwa kutofunika nywele zao.
Ruksa kutumia mlango mmoja migahawani
Hivi majuzi, Serikali iliwapa uhuru wanawake ambapo sasa hakuna haja ya migahawa kuwa na milango tofauti ya kuhudumia wateja kulingana na jinsia na familia.
Awali, ilikuwa lazima kuwa na mlango mmoja kwa ajili ya familia na wanawake na mwingine wa wanaume.
Sharti hilo kwa sasa limeondolewa huku migahawa mingi pamoja na maeneo mengine ya kufanyia mikutano ikifuata mkondo huo.
Hata hivyo, mabadiliko ambayo yamejitokeza katika miaka ya hivi karibuni nchini Saudi Arabia yamekuwa yakiponzwa vikali na wapinzani.
Mapema mwaka huu, agizo kutoka kwa mfalme lilihitaji wanawake wa Saudia kuruhusiwa kusafiri hadi mataifa ya nje bila ya kupata ruhusa ya msimamizi wa kiume.
Marufuku hii iliondolewa pamoja na ile ya wanawake kujiendesha wenyewe iliyofikia ukomo wake mwaka jana.
Hata hivyo, wanaharakati wanalalamika kwamba sheria nyingi zinazobagua wanawake bado zinaendelezwa na watu wengi mashuhuri wanaotetea haki za wanawake wamekamatwa hata wakati ambapo serikali inafanya mabadiliko haya.
Jumapili iliyopita, mamlaka ya serikali ya mitaa ya Saudia ilisema migahawa haitokuwa na ulazima wa kuwa na mlango unaotenganisha wanawake na wanaume badala yake uamuzi wa suala hilo umeachwa mikononi mwa mmiliki wa biashara.
Hadi kufikia sasa, ndani ya migahawa ya Saudia, familia na wanawake hutenganishwa na wanaume kwa kutumia skrini au vioo vikubwa.
Tangu Mohammed bin Salman alipotawazwa na kuwa mfalme mwaka 2017, amefanya mabadiliko katika jamii ambayo imekuwa ikikumbatia tamaduni zake za tangu jadi.
Mabadiliko yake yameungwa mkono na jamii ya kimataifa lakini yamekuwa yakikandamizwa.
Hata hivyo, kifo cha mwanahabari mashuhuri Jamal Khashoggi, mwaka 2018 katika ubalozi wa Saudi Arabia huko Istanbul, ulikosolewa vikali na jamii ya kimataifa japo viongozi wakuu duniani akiwamo Rais Donald Trump wameendelea kuiunga mkono Saudi Arabia.
Maafisa wa Saudi Arabia wanasema Khashoggi, aliyekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Riyadh, aliuawa katika oparesheni iliyotekelezwa na timu ya majasusi. Hata hivyo, wakosoaji wengi wanaamini vyenginevyo, huku mtaalam wa Umoja wa Mataifa akitoa ripoti iliyosema kuwa kifo cha Khashoggi kilitekelezwa na ‘maafisa wa serikali.’
Ruksa kusafiri bila uangalizi
Agosti mwaka huu, ilitangazwa sheria mpya ya mwanamke mwenye umri wa miaka zaidi ya 21 kwamba anaweza kutuma maombi ya paspoti bila idhini ya mlezi wa kiume.
Watu wazima wote sasa wanaomba paspoti na kusafiri hatua inayowapatia haki sawa na wanaume.
Agizo hilo la ufalme pia liliwapa wanawake haki ya kuwasajili watoto wao wanapojifungua, kufunga ndoa au talaka.
Pia sheria hiyo ilizungumzia sheria za ajira zinazopanua fursa kwa wanawake.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, raia wote wana haki ya kufanya kazi bila kukabiliwa na ubaguzi wowote kwa misingi ya jinsia, ulemavu au umri.
Awali wanawake hao walikuwa wakiomba ruhusa kutoka kwa mlezi wa kiume, mume, baba au ndugu mwingine wa kiume kuomba paspoti au kibali chochote cha kusafiri nje ya nchi.
Mwaka 2016, Mtawala wa Saudia Mwanamfalme Mohammed bin Salman, alifichua mpango wa kufanya mageuzi ya kiuchumi ifikapo 2030, kwa lengo la kuongeza ushiriki wa wamawake kwa asilimia 30 kutoka asilimia 22.
Hata hivyo, kumekuwapo kesi kubwa za wanawake wanaotaka uhamiaji katika nchi kama vile Canada, kutokana na madai ya unyanyasaji wa kijinsia.
January mwaka huu, Canada ilimpa hifadhi ukimbizi msichana Rahaf Mohammed al-Qunun mwenye umri wa miaka 18 aliyeikimbia Saudi Arabia na kujaribu kutorokea nchini Australia.
Msichana huyu alisababisha hali ya sintofahamu katika chumba cha hoteli iliyopo katika uwanja wa ndege, Mji Mkuu wa Thailand Bangkok, ambako alikuwa akiomba msaada wa kimataifa.
Mashirika ya kimataifa mara kwa mara yamekuwa yakidai kwamba wanawake wanachukuliwa kama raia wa daraja la tatu nchini humo.