29.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

Sasa ruksa wananchi kujipima Ukimwi

Na MWANDISHI WETU-KATAVI

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema kuwa Bunge limerasimisha sheria ya wananchi kuweza kujipima wenyewe maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

Waziri Ummy amesema hayo jana katika ziara ya kukagua hali ya utoaji wa huduma za Afya na ujenzi wa miundombinu ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi, ikiwa ni jitihada za Serikali za kuboresha huduma za Afya nchini.

“Napenda kuwapa habari njema kuwa Bunge la Mwezi wa 11 limepitisha Sheria, kwahiyo sasa ni rasmi Tanzania mtu kujipima maambukizi ya VVU mwenyewe, kwahiyo hivi vitendanishi (vifaa) vitakuwa vinauzwa kwenye maduka, pia kugawa bure baadhi ya maeneo kwa sababu wakati mwingine watu wanaona unyanyapaa kwenda kupima wenyewe,”alisema Waziri Ummy.

Alisema kuwa, Serikali imeweka angalizo kuwa, kujipima mwenyewe sio majibu ya mwisho, hivyo kuwataka wananchi kuwa, baada ya kujipima wanatakiwa kwenda katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya kuthibitisha na ushauri zaidi wa jinsi ya kuishi.

Aidha, Waziri Ummy ameagiza kuendelea kutoa elimu ya afya kwa wananchi, hususan watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi kutumia dawa kwa usahihi kulingana na maelekezo ya watoa huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

“Tuendelee kuhakikisha watu wote waliobainika na ugonjwa wa Ukimwi, waendelee kutumia dawa kwa usahihi kama walivyoelekezwa na wataalamu wetu katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini,” alisema 

Pamoja na hilo alisema kuwa kuna changamoto ya maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi kwa vijana wenye umri kati ya miaka 15 mpaka 24, huku akiweka wazi kuwa kitaifa hali ya maambukizi mapya kwa vijana hao ni asilimia 40, huku vijana wa kike ikiwa ni asilimia 80 na wakiume ikiwa ni asilimia 20.

Kwa upande mwingine Waziri Ummy amewatia moyo wanaoishi na maambukizi ya VVU kwa kuwakumbusha kuwa, kuhudhuria katika vituo vya Afya na kufuata maelekezo kama walivyopewa na watoa huduma, pia kuishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi sio mwisho wa maisha.

“Niendelee kuwatia moyo kuwa na maambukizi ya Ukimwi sio mwisho wa Dunia, sio sentensi ya kifo, siku hizi watu wanaishi vizuri, kwahiyo nawahimiza kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya, kupima na kuanza kutumia dawa,” alisema Ummy.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,905FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles