Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KAMPUNI ya Saruji Dangote, imepunguza bei ya saruji yake kuongeza ushindani kwenye soko la saruji nchini.
Hayo yalisemwa jana katika taarifa ya kampuni hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Dangote, Alhaj SadaLadan-Baki.
Alisema bei ya saruji aina ya 32.5R imeshuka hadi Sh 10,000 kwa mfuko wa kilo 50 wa saruji, wakati saruji ya 42.5R ikishuka hadi Sh 10,500 kwa mfuko wa kilo 50 kutoka kiwandani hadi popote Dar es Salaam.
Hatua hii inafanya saruji ya Dangote kuwa ya bei nafuu kuliko saruji zote nchini.
Sada alisema hatua hiyo itasaidia maendeleo ya miundombinu na kutilia mkazo mpango wa taifa wa kukabili tatizo la makazi nchini.
Kwa takwimu nchini ina uhaba wa nyumba milioni tatu.
Uwekezaji wa Kampuni ya Dangote utatoa mchango mkubwa katika mipango endelevu ya uboreshaji miundombinu, kupunguza tatizo la ajira kwa vijana na kuboresha uchumi kwa ujumla.
“Tunatambua uhitaji mkubwa wa miundombinu bora, na moja ya njia ya kulikabili tatizo hili ni kumfanya kila mtanzania kuweza kuwa na uwezo wa kununua rasilimali za ujenzi kwa kuweka bei mbadala kwa kila mtanzania.
“Uwekezaji wa zaidi dola za Marekani milioni 600 utaongeza kasi ya ukuaji na uboreshaji wa miundombinu, ajira na kuisaidia serikali katika jitihadi zake za kukuza uchumi wa nchi,” alisema Sada.
Alisema Kampuni ya Saruji Dangote inajihusisha na utayarishaji, uzalishaji, utafiti wa sayansi na ugavi wa saruji na bidhaa nyingine za ujenzi.
Kampuni hiyo iko Nigeria, Benin, Ghana, Congo, Senegal, Tanzania, Afrika Kusini na Zambia na inaongoza kwenye mauzo ya hisa katika soko la hisa Nigeria, alisema.