29.6 C
Dar es Salaam
Saturday, May 21, 2022

Sarakasi za udiwani CCM Dodoma

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

NI SARAKASI tupu ndivyo unavyoweza kusema kufuatia wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Chang’ombe kuandamana hadi ofisi za chama hicho Wilaya ya Dodoma Mjini kutaka waelezwe chama kimempitisha nani kugombea udiwani katika Kata ya Chang’ombe.

Hatua hiyo ilikuja kufuatia CCM Wilaya ya Dodoma Mjini  kudaiwa kumtangaza aliyeshika nafasi ya pili, Juma Ikaba kuwa mgombea wa nafasi ya udiwani wa kata hiyo na kukata jina la aliyekuwa wa kwanza kwenye kura za maoni, Bakari Fundikira.

Sintofahamu ilitokea mara baada ya Ikaba kufika katika Ofisi za CCM Wilaya ya Dodoma Mjini kufuata barua ya kuteuliwa na chama kugombea udiwani katika Kata hiyo ambapo alielezwa kuwa yeye si mshindi na vikao vya juu bado havijaamua nani atakiwakilisha chama katika Kata ya Chang’ombe.

MTANZANIA ilikuwepo eneo la tukio  ambapo mara baada ya wafuasi wa CCM kufika katika ofisi hizo walianza kuhoji aliyepitishwa na chama ni yupi kati ya  Ikaba ama Fundikira kwani wamechanganyikiwa.

Kutokana na usalama kuwa mdogo katika eneo hilo, ilibidi ipigwe simu polisi ambapo baada ya dakika kadhaa walikuja askari katika ofisi hizo na kuwataka wafuasi hao   kuondoka katika eneo hilo.

Wafuasi hao waliendelea kugoma kuondoka katika eneo hilo wakidai wao ni wachache na katika eneo husika wamepanga kuandama ili kujua ukweli upo wapi.

Kutokana na hali hiyo ilibidi kiongozi wa askari waliofika katika eneo hilo (ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini) kuingia ndani na kuzungumza na Katibu wa CCM Wilaya ya Dodoma, Elirehema Nassari, ambapo baadaye  alitoka na kuwaomba wafuasi hao kusubiri maamuzi ya vikao vya juu vya chama hicho.

“Mtulie jamani hizi kasoro zilizojitojitokeza zitatatuliwa, chama ndio kitatoa maamuzi hivi tunavyofanya tutaharibu, tusitafute suluhu kwa kutenda vurugu na kusababisha kutenda makossa ya jinai.

 “Tumemwelekeza katibu afuatile jambo hili tumeelewana, kwahiyo hapa tutawanyike tuendelee na shughuli zingine,”alisema.

Akizungumza na wafuasi hao, Ikaba aliwataka kutulia na kusubiria vikao vya juu ambavyo vitatoa maamuzi.

“Naomba tusikilizane kwenye hili, tumekubaliana kwamba haitatoka fomu kwa mtu yoyote hadi itakapofanyika mabadiliko mengine,”alisema Ikaba.

Akizungumza na MTANZANIA mgombea aliyekuwa wa kwanza  katika kinyang’anyiro hicho, Fundikira alisema hana cha kuzungumza na anaziachia mamlaka husika ambazo ndio zitakuwa na majibu ni nani ambaye atapeperusha bendera ya CCM katika Kata ya Chang’ombe.

MTANZANIA ilimtafuta Katibu wa CCM Wilaya ya Dodoma Mjini, Nassari ambaye alisema yeye hana mamlaka ya kuzungumza jambo hilo kwani hakuwepo kwenye vikao vilivyotoa maamuzi.

“Nendeni CCM Mkoa mimi sina jibu, nitawajibu nini wakati kwenye vikao vilivyofanya maamuzi sikuwepo,”alisema.

MTANZANIA ilifunga safari hadi katika Ofisi za CCM Mkoa wa Dodoma ambapo Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Pili Mbaga alisema bado vikao vinaendelea hivyo hawezi kulizungumzia jambo hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
191,701FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles