22.1 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Samike: Viongozi wa Dini toeni elimu ya Sensa kwa waumini

Na Clara Matimo, Mwanza

Viongozi  wa Dini nchini wameaswa kushirikiana na serikali kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa Sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti 23, mwaka huu huku wakitakiwa kusaidia kuondoa upotoshaji kuwa zoezi hilo ni haramu na linapingwa na maandiko matakatifu.

Wito huo umetolewa leo Jumanne Juni 28, 2022 jijini Mwanza na Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Ngusa Samike wakati akifungua kikao cha mafunzo kwa wajumbe wa kamati ya amani ya viongozi wa dini mkoa wa Mwanza juu ya umuhimu wa sensa.

Baadhi ya viongozi wa kamati ya amani ya viongozi wa dini Mkoa wa Mwanza wakiwa katika picha ya pamoja na Katibu Tawala Mkoa wa mkoa huo, Ngusa Samike(wa nne mstari wa kwanza) baada ya kufungua kikao cha mafunzo kwa wajumbe wa kamati hiyo leo Juni 28, 2022.

Samike amesema Serikali itaendelea kushirikiana na viongozi wa dini katika kutoa elimu endelevu kuhusu sensa ili waweze kutoa taarifa sahihi kwa waumini wao huku akiwahimiza kuweka mabango na matangazo yenye ujumbe wa sensa kwenye nyumba za ibada na kutenga muda wa kuwapa elimu waumini wao.

“Zoezi hili lionekane ni la jamii yote na siyo la serikali tu, tuache kusikiliza wanaopotosha yanapotokea maboresho tujitokeze tuyasemee tuwe wa kwanza kuielimisha jamii tusiache wapotoshaji wachukue nafasi tuwaelimishe watu tuondoe hisia potofu zinazojengeka katika jamii,” amesema Samike.

Kwa upande wake Mwenyekiti Mwenza wa kamati hiyo, Askofu Charles Sekelwa, amesema dini ya kikiristu inaitambua sensa kwani hata  maandiko  yaliyoandikwa katika Biblia Takatifu yanaeleza umubhimu wa jambo hilo hivyo ni halali siyo haramu wala ushetani.

“Ukisoma Biblia Takatifu kitabu cha Luka 2:1 -7 anaeleza kuhusu sensa na umuhinu wake sasa kama maandiko matakatifu ambayo ni ya Mungu mwenyewe yanaiunga mkono sensa sisi wanadamu ni akina nani hata tupinge maagizo ya aliyetuumba? Alihoji na kuongeza

 “Lazima  tushirikiane na serikali kama mlezi wetu, sisi viongozi wa kiroho tuwape elimu waumini wetu na tuache upotoshaji kuwa sensa ni mambo ya shetani maana bila kuwa na idadi ya watu wako hauwezi ukapanga bajeti ya mahiyaji yao,” amesema Askofu Sekelwa.

Nae Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Hasani  Kabeke,  ambaye ni mwenyekiti mwenza wa kamati hiyo, amesema viongozi wa dini ni daraja muhimu la kuwafikia wananchi na kuwapa taarifa muhimu ambapo amesisitiza kuwa sensa siyo jambo haramu na wanaosambaza upotoshaji huo ni watu waliochanganyikiwa akili.

Mratibu wa sensa Wilaya ya Nyamagana, Ruhinda Costantine, amesema sensa huiwezesha serikali kupanga bajeti inayokidhi mahitaji ya wananchi na maeneo wanayoishi  kwa kuzingatia umri, jinsia, elimu, ajira zao na maisha yao kwa ujumla pia hutumika kupanga na kufuatilia utekelezaji wa mipango ya maendeleo endelevu katika sekta zote ikiwemo  kiuchumi, kijamii na mazingira.

Sensa ya mwaka 2022 itakuwa ni ya sita kufanyika nchini baada ya muungano wa Zanzibar na Tanganyika ya kwanza ilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 20002 na 2012.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles