27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

Samia: UWT chujeni wagombea bila aibu

Na RAMADHAN HASSAN – DODOMA

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amelitaka Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuchuja wagombea kwa haki bila kumwonea mtu aibu.

Kauli hiyo aliitoa jijini hapa jana, wakati akifungua  baraza  hilo ambalo ni maalumu kwa uchaguzi wa wabunge wa viti maalumu waliopitishwa kwenye kura za maoni kwenye mikoa.

Samia alisema baadhi ya maeneo kumetokea kasoro kadhaa za uchaguzi na baraza hilo linatakiwa kusahihisha changamoto hizo kwa kufanya mchujo wa haki bila kumwonea mtu aibu.

 “Matumaini yangu kuwa baraza hili kuu litasahihisha changamoto na ukiukwaji wa taratibu uliotokea kwa kufanya mchujo wa haki bila kumwonea mtu aibu au haya, mkumbuke moja ya ahadi za chama chetu inasema ‘nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko’.

“Basi mkishindwa kujipanga wenyewe, vikao vya ngazi za juu ikiwemo Kamati Kuu vitalazimika kuwapanga,” alisema Samia.

Alisema vikao vitafanya hivyo ili kuhakikisha viongozi watakaokiwakilisha chama kwenye Uchaguzi Mkuu ni waadilifu.

“Tutafanya hivi ili kuhakikisha viongozi watakaokiwakilisha chama chetu ni waadilifu, wachapakazi na wenye kuendana na maadili ya chama na dhima yetu ya Hapa Kazi Tu inayolenga kumwinua Mtanzania mnyonge kutoka kwenye dimbwi la umasikini,” alisema Samia.

Alisema anaamini waliopita katika mchakato wa kura za maoni na kupitia ngazi mbalimbali za uchujaji, ni viongozi wazuri ambao hawakukiuka taratibu na kanuni za uchaguzi, ikiwemo kutoa rushwa.

 “Kiongozi mzuri ni yule aliye na uwezo wa kuongoza wenzie kwa kujiamini na kushirikisha wengine na si mtoa rushwa au mpokea rushwa, siku zote kiongozi ni yule anayechaguliwa kwa kura nyingi na kwa ridhaa ya wananchi, na siyo kwa nguvu ya fedha,” alisema Samia.

Aliwataka wanawake wote wa CCM kujiandaa na kujipanga kwa uchaguzi wa dola ili kuhakikisha CCM inashinda kwa ushindi mkubwa.

Alipongeza umoja huo kwa kuongeza idadi ya wanachama wapya kutoka 1,752,145 mwaka 2018 hadi kufikia 1,934,744 mwaka huu.

Samia pia alikemea na kutaka kuvunjwa makundi ya uchaguzi na wale watakaobainika kujihusisha nayo chama kitawachukulia hatua hali.

Mwenyekiti wa UWT, Gaudencia Kabaka aliwataka wanawake hao kuungana kwa pamoja kuhakikisha wanakamilisha dhana ya mafiga matatu katika sanduku la kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28.

Katibu Mkuu wa CCM Bara, Rodrick Mpogolo aliwataka wanawake kuwa wamoja na kuzingatia mshikamano kama silaha ya ushindi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles