SAMIA: UJENZI HOSPITALI SERENGETI UKAMILISHWE

0
618

 

 

NA SHOMARI BINDA-SERENGETI

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ameuagiza uongozi wa Wilaya ya Serengeti mkoani Mara kukamilisha haraka awamu ya kwanza ya ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo ili kuondoa adha ya wananchi kusafiri kwenda mikoa mingine kupata huduma ya afya.

Agizo hilo alilitoa jana mjini hapa wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Mugumu wilayani Serengeti mara baada ya kutembelea ujenzi wa hospitali hiyo ya wilaya na kuweka jiwe la msingi.

Alisema Wilaya ya Serengeti hupata wegeni wengi kutoka nje ya nchi, ambao wanakwenda kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, hivyo ni muhimu kwa viongozi wa wilaya na mkoa kwa ushirikiano na wadau wa maendeleo kukamilisha ujenzi huo haraka ili wananchi waweze kupata huduma za afya za uhakika katika wilaya yao.

“Kukamilika kwa ujenzi huo wa awamu ya kwanza kutaondoa tabu kubwa wanayopata wananchi wa Wilaya ya Serengeti katika kupata huduma ya afya karibu na maeneo yao,” alisema Samia.

Katika kuunga mkono jitihada hizo za ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Serengeti, Makamu wa Rais aliahidi kuchangia kiasi cha Sh milioni tano na amewaahidi wananchi wa Serengeti kuwa atahakikisha fedha kutoka serikalini ambazo zinatakiwa kupelekwa wilayani humo zinapelekwa haraka ili kukamilisha ujenzi huo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here