30.4 C
Dar es Salaam
Monday, December 16, 2024

Contact us: [email protected]

SAMIA: RUSHWA INAHITAJI SULUHISHO LA KIMATAIFA

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM



MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amesema rushwa ni tatizo la kimataifa ambalo linahitaji suluhisho la kimataifa.

Amesema hakuna nchi ambayo inaweza kujitenga na rushwa lakini nchi zinazoendelea na hasa Bara la Afrika limeendelea kuteseka kwa miongo kadhaa kutokana na madhara ya rushwa.

Alikuwa akizungumza jana kwenye mkutano wa kimataifa kuhusu mageuzi katika mapambano dhidi ya rushwa ulioandaliwa kwa ushirikiano wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Benki ya Dunia (WB).

“Rushwa hudhoofisha utawala wa sheria, husababisha kukosekana uaminifu wa umma kwa serikali, kukosekana usawa baina ya walionacho na wasionacho, kuhamasisha uhalifu na kuwapo fedha chafu mtaani,” alisema Suluhu.
Alisema rushwa inapaswa kushughulikiwa kutoka kwenye mizizi ambayo imeendelea kuathiri nyanja zote za maendeleo ya binadamu.

Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki, alisema Sh 30 katika Sh 100 zinazotengwa kwa ajili ya bajeti zimekuwa zikipotea kwa sababu ya rushwa.

“Kwa kiasi kikubwa rushwa imepungua lakini tungependa tusiwe na rushwa kabisa, hatutavumilia rushwa katika huduma zetu,” alisema Kairuki.

Mkurugenzi wa Takukuru, Valentino Mlowola, alisema awamu ya tatu ya mkakati wa mapambano dhidi ya rushwa (2016 – 2022) utaelekeza nguvu katika sekta za mkakati ambazo ni ununuzi, ukusanyaji wa mapato, utalii, ardhi na elimu.

“Rushwa ni tatizo la jamii hivyo kama wananchi watakuwa tayari kushiriki katika mapambano haya sekta zinazolalamikiwa zitadhibitiwa.

“Jamii inaendelea kuona kama rushwa ndiyo njia ya maisha na watumishi wa umma wanaendelea kutumia vibaya madaraka yao kwa masilahi yao,” alisema Mlowola.

Alisema mfumo wa sasa wa uendeshaji mashitaka una upungufu kwa sababu karibu kesi zote zinashughulikiwa na mtu mmoja na kusababisha ucheleweshaji wa kesi.

Kupitia mkutano huu nchi ambazo zimefanikiwa duniani katika mapambano ya rushwa kama vile Madagascar, Georgia, Romania, Uingereza, Botswana na Switzerland zitaeleza uzoefu wao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles