26.1 C
Dar es Salaam
Friday, December 9, 2022

Contact us: [email protected]

Samia kufungua rasmi maonyesho ya Nanenane Simiyu

 GRACE SHITUNDU -DAR ES SALAAM

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufungua maonyesho ya Nanenane kitaifa leo katika viwanja wa Nyakabindi wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu yatakayofanyika kuanzia Agosti 1 hadi 8 mwaka huu.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi , Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Mariam Mmbaga alisema katika maonyesho hayo yanayofanyika kitaifa mkoani humo wanatarajiwa kujumuika na viongozi mbalimbali wa kitaifa.

“Siku ya kesho (leo), Mgeni wetu rasmi ambaye atatufungulia maonyesho haya atakuwa ni Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan ambaye atatembelea mabanda mbalimbali na kuzungumza na wananchi wa Mikoa mitatu ya Mara, Simiyu na Shinyanga,” alisema Mmbaga.

Alisema pia wanatarajiwa kuwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye atatembelea mabanda Agosti 3 na pia kuzungumza na wananchi.

“Agosti 3 mwaka huu katika maonyesho haya tutakuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye naye atatembelea mabanda mbalimbali ya wadau na kuzungumza na wananchi mbalimbali watakaokuwa wametembelea viwanja hivyo,” alisema.

Mmbaga alieleza kwamba maonesho hayo yataambatana na uhamasishaji wa matumizi ya teknolojia bora za kilimo, ufugaji na uvuvi na yatashirikisha wadau mbalimbali zikiwemo Wizara, Taasisi za umma na binafsi, wabia wa maendeleo, wakulima na vyama vya wakulima, wafugaji na wavuvi. 

 Kutokana na maonyesho hayo kuwa elimu kubwa, Mmbaga alitoa wito kwa wananchi wa mikoa inayounda Kanda ya Ziwa Mashariki kujitokeza kwa wingi katika viwanja hivyo.

“Wananchi wajitokeze kwa wingi kwani maonyesho haya yana faida kubwa katika nyanja za kilimo, ufugaji na uvuvi,” alisema.

Aidha aliwataka wananchi wanaozunguka viwanja vya Nyakabindi kutumia fursa mbalimbali zitakazojitokeza katika maonyesho hayo kwa kufanya kazi, biashara ili kujiongezea kipato. Kuhusu mgeni rasmi katika ufungaji wa maonyesho hayo Katibu Tawala huyo alisema wanatarajia atakuwa Rais Dk. John Magufuli.

“Katika ufungaji wa maonyesho mgeni rasmi endapo hakutakuwa na mabadiliko tunatarajia atakuwa Rais wa Tanzania Dk. John Magufuli”alisema Mmbaga.

Alisema sambamba na viongozi hao pia wanatarajia kutembelewa na mawaziri na manaibu waziri wa wizara tofauti nchini sambamba na wakuu mbalimbali wa taasisi za kilimo, mifugo , uvuvi, fedha na wadau mbalimbali wa maonyesho hayo.

Akizungumzia kuhusu kauli mbiu ya mwaka huu Mmbaga alisema ni “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua Viongozi Bora 2020’.

Alisema kaulimbiu hiyo inatoa hamasa kwa wananchi kuchagua viongozi bora watakaokuwa chachu ya kuleta mapinduzi kwa ajili ya maendeleo ya sekta za kilimo ili kuinua ustawi wa maisha ya wakulima, wafugaji na wavuvi.

 “Huu ni mwaka wa uchaguzi hivyo kauli mbiu hii inatoa hamasa kwa wananchi kuchagua viongozi watakaosaidia kutatua changamoto za wakulima, wafugaji na wavuvi ambao ndio asilimia kubwa ya watanzania,” alisema Katibu Tawala huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,734FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles