24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

SAMIA: KERO YA MAJI MUSOMA SASA BASI

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, akimsikiliza Mkurugenzi wa Muwasa, Said Gantala (kulia), alipotembelea mradi mkubwa wa maji mjini Musoma.

Na SHOMARI BINDA,

SIKU zote Serikali husisitiza juu ya suala la utunzaji wa mazingira. Hii ni kwa sababu uharibifu wa mazingira ni chanzo cha uhaba wa maji nchini.

Wananchi wamekuwa wakielimishwa kutunza vyanzo vya maji na kuacha kufanya shughuli za kilimo pembezoni mwa vyanzo hivyo.

Katika ziara ya siku tatu ya Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan mkoani Mara, pamoja na mambo mengine alitembelea mradi mkubwa wa maji safi na salama Musoma.

Mradi huu upo kwenye eneo la Bukanga nje kidogo ya mji wa Musoma ambao unagharimu kiasi cha Sh bilioni 45 fedha ambazo zimetolewa na Serikali na Shirika la Misaada la Ufaransa (NFP).

Katika mradi huu mkubwa wa maji unaosimamiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (Muwasa), Samia alipokea taarifa juu ya mradi unaotarajiwa kukamilika Juni 30 mwaka huu.

Akitoa taarifa hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk. Vicent Naano alisema kukamilika kwa mradi huo kutawezesha asilimia 97 ya wakazi wa mji wa Musoma kupata maji.

Alisema mradi huo baada ya kukamilika utazalisha lita 34,000 za maji kwa siku ambapo mahitaji ni lita 20,000 hivyo kubaki na lita za ziada 10,000 ambazo zitatumika kusambaza kwenye vijiji 21 katika Halmashauri ya Musoma Vijijini na Wilaya ya Butiama.

Anasema mradi huo ni wa kipekee kwa kuwa maji ambayo yatazalishwa yana uwezo wa kuchotwa na kunywa kutoka kwenye bomba bila ya kuchemshwa kutoka na kuchujwa na kuwekwa dawa ya kutosha ya kutibu maji.

“Ujenzi wa tenki kubwa lenye ujazo wa kujaza maji lita milioni tatu  katika Mlima Balili litakalohudumia wananchi wa pembezoni mwa Manispaa ya Musoma na vijijini, limeanza kujengwa ili kutimiza lengo la usambazaji maji,” anasema Dk. Naano.

Akizungumzia mradi huo, Makamu wa Rais anasema kazi iliyofanywa ni kubwa na kwamba ahadi ya Serikali ni kupunguza au kuondoa tatizo la maji hivyo kwa sasa shida ya maji Musoma na vijiji jirani itakuwa historia, kilichobaki ni kusambaza miundombinu ya maji kwa wananchi.

“Maji yapo ya kutosha, kilichobaki ni ugawaji kwa wananchi. Naomba niwaambie kwamba fedha za kufanya hivyo kwa awamu ya kwanza zipo na zitaletwa.

“Utekelezaji wa mradi huu ni mzuri nimeuona na ahadi yetu kwenye suala la maji kwa hapa Musoma tumelikamilisha, wananchi mtapata maji lakini muyatunze, msifanye uharibifu wa miundombinu,”anaonya Samia.

Naye Mkurugenzi wa Muwasa, Said Gantala anasema wapo tayari kusambaza maji lakini kama wananchi wanaharaka wanapaswa kutoa ushirikiano kama kuchimba mitaro kwa ajili ya kusambaza mabomba.

Anasema kwa sasa bado hawajapata fedha za kupeleka maji kwenye nyumba za wananchi, kikubwa ni kufanya mawasiliano na viongozi kwenye maeneo husika ili kukubaliana kuchimba mitaro hatimaye waweze kuwawekea mabomba.

Kwa mujibu wa Gantala, mabomba wanayo ya kutosha kwa ajili ya kusambaza maji lakini wameshindwa kufanya hivyo mapema kutokana na kukosa fedha.

Tatizo la maji katika Mji wa Musoma limelalamikiwa kwa muda mrefu, sasa kinachofanyika ni kuondoa kero hiyo.

Muwasa inasisitiza ushirikiano kati ya wananchi na mafundi ili yale malengo ambayo yanakusudiwa yaweze kukamilika hatimaye tatizo la maji liwe historia kama ilivyo adhma ya Serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles